Bi Ester Jonas Mama mzazi wa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi Yohana Bahati aliyeuwawa Mkoani Geita.
Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesikitishwa na mauaji ya kikatili ya mtoto Yohana
Bahati aliyetekwa nyara hivi karibuni katika kijiji cha Ilelema, Chato Mkoani
Geita.
Pia Tume
inalaani kuumizwa kwa mama yake, Ester Jonas wakati anatetea uhai wa mwanae wakati
wa tukio lililotokea Februari 15, 2015.
Tume inapenda
kuwakumbusha wananchi kwa ujumla kuwa vitendo vya ukatili wanaofanyiwa watu
wenye ulemavu wa ngozi, ni matukio ya ukiukwaji wa Sheria na haki za
kibinadamu. Matukio haya yanaonesha yamekuwa yakichagizwa na imani za
kishirikina hivyo Tume inakemea matendo haya na kutaka yapigwe vita.
Chini ya Katiba
na Mikataba ya Kimataifa ya Haki za Binadamu Serikali inao wajibu wa kulinda
raia wake. Tume inaiomba Serikali kuwatafuta wale wote wanaohusika na vitendo
hivi na kuwafikisha mbele ya vyombo vya Sheria.
Aidha, Tume
inaungana na wananchi, wadau mbalimbali na Serikali kulaani vikali mauaji ya
mtoto Yohana Bahati na kujeruhiwa vibaya mama yake wakati akitetea haki ya
mwanae kuishi katika jamii huru, na inakemea vikali vitendo hivyo vya kikatili
dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi kwa ujumla.
Tume
inaikumbusha Serikali kuwa wakati umefika wa kufanyia marekebisho makubwa Sheria
ya Uchawi (Sura ya 18 ya 1928) au kutunga Sheria mpya ili kupiga marufuku
vitendo vyote vinavyoendeleza imani za uchawi na ushirikina.
Tume inashauri
pia Serikali kupitia upya Sheria inayowatambua waganga wa jadi (Sheria ya Tiba
Asili na Tiba Mbadala).
Tume inatoa
wito kwa wananchi na jamii yote kwa ujumla kuachana na imani potofu zenye
mtizamo hasi kwamba mafanikio yoyote yanaweza kupatikana kwa njia za
kishirikina. Tume inakumbusha wananchi kuwa mafanikio yoyote yatapatikana kwa
kufanya kazi zote halali kwa bidii, na siyo kwa njia za kishirikina ikiwemo kutumia
viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Tume inaungana
na wananchi na Serikali kupiga vita vitendo hivi vya kikatili.
Pia Tume inatoa
pole kwa mama aliyeumizwa akitetea uhai wa marehemu mwanae.
Mwisho Tume iko
mbioni kwa kushirikiana na wadau wengine kutekeleza mpango wa kitaifa wa
kuelimisha wananchi ili kuepusha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini. Tume
inaomba wananchi wote kushirikiana katika jukumu hili.
Imetolewa na:
Mhe. Bahame Tom Nyanduga
Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
No comments:
Post a Comment