Waendesha pikipiki (bodaboda) wakipita mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Singida Mwl. Queen M. Mlozi wakati wa mkutano wa kuvunga mafunzo ya usalama barabarani.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Parseko V. Kone amewashauri waendesha pikipiki Wilayani Singida kushiriki na kugombea katika uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Disemba mwaka huu ili kupata uwakilishi katika serikali za mitaa na vijiji.
Dokta Kone ametoa ushauri huo wakati akifunga mafunzo ya siku saba ya usalama barabarani kwa waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda ambapo aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Singida Mwl. Queen M. Mlozi.
Mkuu wa Wilaya ya Singida Mwl. Queen M. Mlozi akifunga mafunzo ya usalama barabarani kwa waendesha pikipiki Wilayani Singida kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Parseko V. Kone.
Amewaasa kutumia mafunzo hayo ili kujiongezea uwezo wa kuendesha shughuli zao kiujasirimali na kufuata sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali zinazotokana na uzembe au kutokujua sheria za usalama barabarani.
Aidha amemshukuru Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na kuondoa umaskini na utunzaji wa mazingira (APEC), Respicius Timanywa kwa kuendesha mafunzo hayo kwa waendesha bodaboda na kumpa heshima ya jina la Chifu Senge wa bodaboda.
Waendesha pikipiki (bodaboda) wa Wilaya ya Singida waliopatiwa mafunzo ya usalama barabarani.
Akisoma risala ya wahitimu wa mafunzo ya usalama barabarani katibu wa mafunzo hayo Maulid Hamis Mpondo amesema shirika la APEC limetoa mafunzo kwao juu ya alama na sheria zote za usalama barabarani, upatikananji wa leseni, faida za kulipa kodi, ujasiriamali, polisi jamii, ulinzi shirikishi na elimu ya Ukimwi.
Mpondo ameongeza kuwa changamoto wanazokutana naazo ni pamoja na kukabwa na kuibiwa pikipiki, upatikanaji wa leseni, maderva wa mabasi na malori kutokuwathamini na kuwachomekea.
Mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo Mchungaji Mariamu Thomasi Joseph amesema mafunzo hayo yametolewa na nadharia bila vitendo vya jinsi ya kuendesha vyombo hivyo.
Ameshauri shirika hilo kurudia mafunzo hayo wilayani Singida ili waendesha pikipiki wengine wanufaike, pia shirika hilo lijikite katika kutoa mafunzo hayo kwa vitendo hasa namna ya kuendesha vyombo hivyo vya moto.
Mhitimu wa mafunzo ya usalama barabarani kwa waendesha pikipiki Mchungaji Mariam Thomas Joseph.
Naye mwalimu wa mafunzo hayo Edrick Serapion amesema APEC wametoa mafunzo kwa njia ya nadharia kwakuwa vyuo vingi hutoa mafunzo ya kutumia vyombo vya moto na kusahau kutoa elimu ya usalama barabarani.
Serapion amesema APEC imetoa elimu kwa kina juu ya sheria na alama za barabarani, ujasiriamali, elimu ya ukimwi na polisi jamii kitu ambacho vyuo vingi havifanyi hivyo.
Waendesha pikipiki waliopatiwa mafunzo hayo wametoka katika vituo vya Makiungu, Mtinko, Itaja, Ilongero na Singida Vijijini.
Mkuu wa Wilaya ya Singida Mwl. Queen M. Mlozi akipokea zawadi ya mbuzi wakati wa kufunga
mafunzo ya usalama barabarani kwa waendesha pikipiki Wilayani Singida
kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Parseko V. Kone.
Mkuu wa Wilaya ya Singida Mwl. Queen M. Mlozi akitoa vyeti vya
mafunzo ya usalama barabarani kwa waendesha pikipiki Wilayani Singida
kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Parseko V. Kone.
No comments:
Post a Comment