Wednesday, October 29, 2014

MKOA WA SINGIDA WAVUKA LENGO LA CHANJO YA KITAIFA YA SURUA-RUBELA KWA ZAIDI YA ASILIMIA MIA MOJA.

Mkoa wa Singida umevuka lengo kwa zaidi ya silimia mia moja katika chanjo ya kitaifa ya Surua-rubela na utoaji wa matone ya Vitamini A huku malengo ya utoaji wa dawa za matende, mabusha na minyoo yakifikiwa kwa asilimia 64.

Lengo la Mkoa kwa chanjo ya surua-rubela kwa watoto wenye umri wa miezi tisa hadi chini ya miaka 15 ilikuwa watoto 631,139 lakini wamefanikiwa kuchanja watoto 672,625 sawa na asilimia 107, utoaji wa matone ya Vitamini A kwa watoto wa miezi sita hadi miaka minane umefanikiwa kwa watoto 292,295 sawa na asilimia 113.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Parseko V. Kone.
Kwa upande wa utoaji wa dawa za minyoo, matende na mabusha Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Parseko Vicent Kone hakuridhishwa na idadi ya wananchi 916,970 sawa na asilimia 64 waliopata dawa hizo.

Dokta Kone amesema amefurahishwa na idadi ya watoto waliopata chanjo lakini kwa upande wa watu wazima, wanaume walikuwa wazito kwenda kupata dawa hizo ijapokuwa alionyesha mfano kwa kunywa dawa za minyoo, mabusha na matende hadharani wakati wa uzinduzi wa chanjo hizo Wilaya ya Ikungi.

Aidha amewashukuru wananchi wote na viongozi kwa kufanikisha zoezi hilo la kitaifa huku akisisitiza kuwa dawa hizo hazina madhara yoyote kwa kuwa sserikali haiwezi kutoa kitu cha kuwadhuru wananchi wake.
 
Kwa upande wake Msimamizi wa Chanjo kutoka wizara ya Afya Yohana Emanuel amesema zoezi la kitaifa la chanjo kwa Mkoa wa Singida limefanikiwa kutokana na ushirikiano wa wananchi na viongozi wa Mkoa wa Singida.

Emanuel amesema viongozi wamefanya kazi nzuri ya kuhamasisha wananchi akitoa mfano wa Viongozi wa Mkalama walioamua kuwachinjia nyama jamii ya wahadzabe ili waweze kuhamasika kupata chanjo hizo.

Ameongeza kuwa changamoto waliyokutana nayo wakati wa zoezi hilo ni mwitikio mdogo wa wanaume waliokuwa hawafiki katika vituo vya chanjo na hivyo kuwalazimu kutembelea nyumba hadi nyumba ili waweze kuwafikia.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Dorothy Gwajima.

No comments:

Post a Comment