“Tunaweza kuongeza
wingi na ubora wa mazao mara dufu bila kuongeza ukubwa wa shamba, kama wakulima
wetu watafuata kwa dhati masharti na kanuni za kilimo bora, Aidha Viongozi na
Wataalam waendelee kutoa huduma
zinazotakiwa ili shughuli za uzalishaji mali zilete tija kwa wananchi wa Mkoa
wa Singida”, Dkt. Kone.
Mkuu wa Mkoa wa Singida
Dkt.Parseko V. Kone akifungua kikao cha Ushauri cha Mkoa (RCC).
Rai hiyo
imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Parseko V. Kone katika kikao cha
ushauri cha Mkoa wa Singida wakati wajumbe wakijadili utekelezaji wa malengo ya
kilimo na hali ya chakula Mkoani hadi mwezi februari, 2014.
Dkt. Kone
amesema Mkoa wa Singida unajitosheleza kwa chakula kutokana na mvua
zilizonyesha vizuri na uhamasishaji uliofanyika kwa wakulima hasa katika mazao ya kipaumbele
ya Uwele, Mtama, Viazi vitamu na Muhogo kwa upande wa chakula na Alizeti,
Vitunguu, Pamba na Asali kama mazao ya biashara tangu mwaka 2006.
Wakuu
wa Wilaya mbalimbali za Mkoa wa Singida wakifuatilia Kikao cha Kamati ya
Ushauri ya Mkoa (RCC), Wa kwanza ni Mkuu wa Wilaya ya Singida Queen Mlozi,
anayefuata ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba Yahya Nawanda, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi
Manju Msambya, Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Fatma Toufiq, na Mkuu wa Wilaya ya
Mkalama Edward Ole Lenga.
Aidha Dkt. Kone amesema suala la ujasiriamali linapaswa
kuwekewa mkazo na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kutenga fedha za kuwakopesha wanawake na vijana kupitia vikundi vyao.
Ameongeza kuwa mamlaka
hizo zinapaswa kutenga maeneo ya kufanyia shughuli kwa vikundi hivyo na kuwezesha miradi midogo na
ya kati kama vile miradi midogo midogo ya umwagiliaji, ufugaji wa kuku
wa asili kibiashara na ufugaji nyuki.
Wajumbe mbalimbali wakifuatilia Kikao cha Kamati ya
Ushauri ya Mkoa (RCC), Wa kwanza ni Mbunge viti Maalum (Chadema) Christowaja Mtinda, anayefuata ni Mbunge Iramba Mashariki Salome Mwambu na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida Iddi Mpanda.
Akisoma taarifa ya
maendeleo ya elimu Katibu Tawala Msaidizi Elimu Mkoa wa Singida Fatma Kilimia amesema matokeo ya mtihani wa kidato cha nne 2013 Mkoa umepata ufaulu wa asilimia 56 ikiwa ni asilimia 4 zaidi ya malengo ya
Matokeo Makubwa na Bayana.
Kilimia ameongeza kuwa
licha ya ufaulu huo Mkoa umefanya ufutiliaji na kubaini kuwa bado baadhi ya walimu hawajitumi kabisa katika suala la
ufundishaji, wengine hawana ujuzi wa baadhi ya mada, jamii kutokua na mwamko
wa elimu hivyo kusababisha utoro na baadhi ya walimu kuandaa masomo kwa
mtindo wa kizamani.
Ameongeza kuwa kutokana na changamoto hizo mafunzo ya
Wawezeshaji ili kuwajengea uwezo yametolewa kwa Wawezeshaji 232 kwa Halmashauri
zote.
Naye Dkt Kone ameagiza kuwa wanafunzi wote waliofaulu waweze kwenda shule na wazazi watakaokaidi wachukuliwe hatua za kisheria.
Katibu Tawala Msaidizi Elimu Mkoa wa Singida Fatma Kilimia akisoma taarifa ya
maendeleo ya elimu Mkoa wa Singida.
Hongera Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida kwa kutuhabarisha maendeleo ya mkoa wetu, tuko pamoja katika kuleta maendeleo pongezi kwa Mkuu wa Mkoa DK Kone.
ReplyDelete