“Asali ni chakula na
pia Asali ni dawa, Asali inatakiwa ibaki
na ubora uleule toka kwenye mzinga mpaka kwa mtumiaji, unapochemsha asali au
unapoiweka katika chupa zilizotumika mfano chupa za Konyagi unaharibu ubora wa
asali hiyo”, Hassan.
Katibu Tawala Mkoa wa
Singida Liana Hassan ametoa angalizo hilo wakati akifungua warsha ya mafunzo
kwa wafugaji nyuki na wajasiriamali wa mazao ya nyuki mkoani Singida
iliyoandaliwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Hassan amesema
wajasiriamali na wafugaji hao wanapaswa kufuata taratibu na kanuni ambapo
wataelekezwa katika mafunzo hayo kwani asali ni rahisi kuharibika isipotunzwa
vizuri.
Ameongeza kuwa ufugaji
nyuki una hatua muhimu nne ambazo ni kupata mzinga, kuuweka mzinga sehemu
ambayo nyuki wataufikia na kuishi, kuvuna mazao ya nyuki na hatua ya nne ni
kuchakata na kufungasha mazao ya nyuki (asali na nta) hatua mbayo bado ina
changamoto hasa kwa wafugaji na wajasiriamali wadogo.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Liana Hassan akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake (hawapo pichani).
Kwa upande wake Meneja
Msaidizi Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kanda ya kati Joyce Chonge amesema
mafunzo hayo yametolewa kwa wajasiriamali na wafugaji 30 wa Mkoa wa Singida
ambao wameelimishwa juu ya usalama na ubora wa mazao ya nyuki, pamoja na nama
ya kupata masoko ya mazao hayo.
Chonge amesema
uhamasishaji juu ya ufugaji nyuki umefanyika vizuri hivyo hatua inayofuata ni
kutoa elimu juu ya sheria na kanuni za ufugaji nyuki na uuzaji wa mazao ya
nyuki kabla ya utekelezaji wa sheria hiyo miaka mitatu ijayo.
Amesema baada ya miaka
mitatu asali itakayokuwa na sumu, maji au imefungashwa katika chupa
zilizotumika kama za konyagi, itamwaga na mhusika atatozwa faini kati ya
shilingi elfu hamsini hadi milioni moja au kifungo cha mwaka mmoja au adhabu
zote mbili yaani kifungo na faini.
Aidha, Afisa Nyuki
Kanda ya kati Mathew Robert Kiondo amesema mtu yeyote akitaka kufanya biashara
ya mazao ya nyuki anatakiwa kujisajili kwanza ambapo anatakiwa kuwa na leseni
ya biashara, awe mlipa kodi ndipo afisa nyuki wa eneo alipo amkague kabla ya
kumruhusu kufanya biashara hiyo.
Kiondo ametoa rai kwa
watumiaji wote wa mazao ya nyuki kutokukubali kuuziwa asali katika chupa
iliyotumika akitoa mfano kuwa huwezi kukubali kununua maji ya kunywa katika
chupa ya soda iliyotumika hivyo hivyo katika asali.
Afisa Nyuki
Kanda ya kati Mathew Robert Kiondo akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani).
Baadhi ya washiriki wa
mafunzo hayo wameishukuru Wakala wa Huduma za Misitu kanda ya kati kwa kutoa
mafunzo hayo.
Mwenyekiti wa Kikundi
cha Rey Products cha Manispaa ya Singida Rehema Hamis amesema mafunzo hayo
yamewasaidia kufahamu juu ya sheria za ufugaji nyuki na uuzaji wa mazao ya
nyuki hivyo itawasaidia kufanya biashara hiyo kwa ufanisi na kwa kufuata
taratibu na sheria.
Mwenyekiti wa Kikundi
cha Rey Products cha Manispaa ya Singida Rehema Hamis akiwaeleza waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya mafunzo hayo.
Naye Mwenyekiti wa
kikundi cha Sombi na Maendeleo cha Msikii Singida Vijijini Sombi Jaksoni Sombi
amesema amejifunza jinsi ya uvunaji wa asali iliyokomaa na pia mafunzo hayo
atayafikisha kwa wanakikundi wenzake.
Sombi amesema wafugaji nyuki na wajasiriamali wa mazao ya nyuki hawanabudi kufuata taratibu na sheria walizofundishwa katika semina hiyo kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.
Mwenyekiti wa
kikundi cha Sombi na Maendeleo cha Msikii Singida Vijijini Sombi Jaksoni Sombi akimueleza mwandishi wa habari juu ya mafunzo hayo.
Mafunzo ya kuhusu
usalama, ubora na masoko ya mazao ya nyuki yamefanyika kwa siku mbili katika
ukumbi wa mikutano ofisi ya Mkuu wa Mkoa, mafunzo hayo yamejumuisha sheria na
kanuni za ufugaji nyuki na mfumo wa ufuatiliaji na udhibiti wa mabaki ya
kemikali katika asali.
Washiriki wamejifunza
pia sera ya TFS ya ugawaji wa vifaa vya ufugaji nyuki kwa wadau, vifaa vya
ufugaji nyuki na umuhimu wake katika kuboresha mazao ya nyuki, biashara na
masoko ya mazao ya nyuki na uzalishaji na utengenezaji wa nta.
Baadhi ya washiriki wakifuatilia mafunzo ya usalama, ubora na masoko ya mazao ya nyuki yaliyoandaliwa na TFS katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
No comments:
Post a Comment