Thursday, June 06, 2024

SERIKALI YA MKOA WA SINGIDA YAZINDUA SIKU MAALUM YA KUSHUGHULIKIA KERO ZA WANANCHI.

Mamia ya Wananchi wa Mkoa wa Singida wamemiminika katika Ofisi ya Mkuu wa mkoa huo kwa ajili ya kutoa kero mbalimbali zinazowakabili kwa muda mrefu ili ziweze kupatiwa ufumbuzi kufutia Mkuu wa mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego, kuzindua rasmi siku ya Alhamisi kuwa ni siku maalum ya kusikiliza na kushughulikia kero za wananchi wa mkoa huo na kuzitafutia ufumbuzi.

Akizindua Kliniki hiyo ya kushughulikia kero za wananchi leo (6-Juni-2024) zoezi ambalo linajumuisha Wakuu wa Mashirika na Taasisi zote za mkoa wa Singida, Mkuu huyo wa mkoa amesema zoezi hilo litafanyika katika Halmashauri zote Saba za mkoa wa Singida nia ni kuona wananchi wanaishi maisha ya furaha kwa kuwaondolewa kero zinazowakabili.

Halima Dendego, amesema Ofisi yake itakuwa inafanya zoezi hilo kwa mwezi mara Moja na watagawana na Katibu Tawala wa mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga, kwenda kwenye kila Halmashauri kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za Wananchi kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alivyowaagiza.

Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego akizungumza katika uzinduzi wa Kliniki ya kushughulikia kero za wananchi wa mkoa wa Singida.

“Tunapokaa hivi tukawasiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowasumbua basi tutakuwa tumefanya jambo kubwa la kuwarejeshea wananchi furaha iliyopote kwa kuondoa kero zao zinazowasumbua kwa muda mrefu”, amesisitiza Halima Dendego.

Ameeleza kuwa katika maisha yetu ya kila siku mtu akiwa na manung’uniko, maumivu na malalamiko hata umpe zawadi yoyote nzuri hataifurahia lakini unapomtatulia kero inayomkabili basi unamrejeshea furaha yake.

Naye, Katibu Tawala wa mkoa wa Singida Dkta. Futuma Mganga amewahakikishia wananchi kuwa watakuwa bega kwa bega na Mkuu wa mkoa pamoja na Viongozi wengine wa Wilaya katika kuhakikisha kero za wananchi zinapatiwa majawabu haraka ili wananchi watumie muda wao kufanya kazi badala ya kila siku kuzunguka kwenye ofisi za umma kwa ajili ya kutafuta majawabu ya kero zinazowakabili.

Baadhi ya Wananchi wa mkoa wa Singida Elizabeth Machael na Hamisi Mneta waliojitokeza kutoa kero zao wamempongeza Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego kwa kutenga siku maalum ya kusikiliza kero za wananchi na wamesema wanaimani kubwa kuwa kero walizotoa zitapatiwa majawabu kwa wakati na ya uhakika.





No comments:

Post a Comment