Thursday, March 07, 2024

SINGIDA NA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI MACHI, 8, 2024

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga, ametoa wito kwa Wafanyakazi wa Serikali, wadau wa maendeleo, taasisi na wana Singida kwa ujumla kushiriki katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mwanammke Duniani yatakayofanyika kimkoa katika viwanja vya standi ya zamani Wilayani Ikungi Machi 8, 2024 ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mhe. Mama Tunu Pinda Mke wa waziri Mkuu Mstaafu Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda.

Aidha Dkt. Fatuma Mganga ametoa rai kwa jamii mkoani humo kuchukua hatua za makusudi kushughulikia masuala ya ubaguzi wa kijinsia, mifumo kandamizi na uonevu kwa Wanawake.

Akiizungumzia siku ya Wanawake Dunia amesema kila (Tarehe 8 Machi) Dunia inaadhimisha Siku ya Wanawake. Hivyo kwa kuzingatia umuhimu wa mwezi Machi na maadhimisho hayo, Mkoa wa Singida kwa kushirikiana na Taasisi za Umma, Asasi za Kiraia, Wadau wa Maendeleo na Mamlaka za Serikali za Mtaa wamekuwa wakifanya mijadala yenye lengo la kuongeza idadi ya wanawake wa kuchaguliwa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024.

Aidha Halmashauri mkoani hapa zimefanya maonyesho ya bidhaa za wajasiriamali haswa wanawake kama vile utengenezaji wa Batiki, Makongamano ya kuelimisha jamii kuhusu mmomonyoko wa maadili haswa Mashuleni.

Pia Serikali ya Mkoa imefanya matendo ya huruma katika kituo cha Malaika wa Matumaini kilichopo Singida Mjini kwa kuwatembelea na kuwapatia zawadi watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu, imefanya maonyesho ya bidhaa zinazotengenezwa na vikundi vilivopatiwa mikopo ya Wanawake kwa Ngazi za Halmashauri.

Sambamba na hayo mkoa umehamasisha elimu kutoka kwa wanawake waliofanikiwa, pamoja na kutoa vyeti kwa vikundi vya wanawake vinavyofanya vizuri katika marejesho ya Mikopo.

Dkt. Fatuma Mganga, amemalizia kwa kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa kuwatia moyo na kuwapa kipaumbele Wanawake kwa nafasi mbalimbali za Uongozi wa juu kwa Mkoa wa Singida na Taifa kwa ujumla, mikopo nafuu kwa Wanawake vijana na watu wenye ulemavu ili kujikwamua kiuchumi kuhakikisha wanatimiza ndoto zao za kuleta maendeleo binafsi na nchi kwa ujumla.

Kauli Mbiu ya Maadhimisho kwa huu wa 2024 ni:

 ‘Wekeza kwa Wanawake Kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii’












No comments:

Post a Comment