Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba ametoa wito kwa viongozi na watendaji wa Serikali kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kusimamia miradi yote inayotekelezwa katika halmashauri za mkoa huo kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma stahiki.
Wito huo umetolewa leo Februari 28, 2024 wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano ofisi ya Mkuu wa Mkoa kilichohusisha Katibu Tawala wa Mkoa huo, Dkt Fatuma Mganga, Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi, Wakuu wa Sehemu na Vitengo kutoka mkoani na wilayani.
Serukamba, amesema haiwezekani fedha zilizoletwa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maendeleo ikiwemo majengo ya shule, vituo vya afya, barabara halafu kuna baadhi ya watendaji wanachelewesha utekelezaji wake, kwahatua hiyo ameahidi hatomvumilia yeyote atakayehusika kuchelewesha au kukwamisha miradi kukamilika kwa wakati na hatimaye atachukuliwa hatua za kinidhamu.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amewahimiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa huo kwenda kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa mapato kutoka katika kila chanzo ikiwemo minada, mazao ya biashara na kuhimiza kutotumia fedha za mapato ya ndani kwa miradi iliyoletewa fedha na Serikali.
Akimalizia hotuba yake Serukamba amewasihi Wakuu wa Wilaya Mkoani humo kwenda kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara katika maduka kuhusu bei za sukari na endapo wakiwabaini wafanyabiashara wanaouza bei ambayo ni kinyume na bei elekezi iliyotolewa na Serikali wawakamate ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Agizo hilo limetokana na operesheni aliyoifanya jana Februari 27, 2024 Wilayani Manyoni ya kuwakamata walanguzi wa sukari ambapo alimkamata mfanyabiashara akiuza mfuko wa sukari wenye kilo 50 kwa bei Sh. 189,000 ambayo ni kubwa ukilinganisha na bei elekezi ya Serikali.
“Tumepata baahati ya kuwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan mwenye maono na anayejali wananchi wake kwa mtu
mmoja mmoja analetea fedha nyingi za miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani
kwetu hivyo hakuna sababu ya kutokamilisha na kutotekeleza wajibu wetu ipasavyo”.
RC Serukamba amesema
Kwaupande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt. Fatuma
Mganga, amewasisitiza watendaji hao wa Serikali hususan Wahandisi wa
halmashauri, maafisa mipango pamoja na maafisa manunuzi kuwa wazalenda wakati
wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi kwa kutumia fedha kulingana na
mahitaji halisi ya fedha sambamba na kuwa na dhamira ya dhati ya ukamilishaji
miradi.
MATUKIO KATIKA PICHA
No comments:
Post a Comment