Tuesday, February 27, 2024

RAS Singida awataka Maafisa Biashara kuwawezeshaji wafanyabiashara kukuza biashara zao

KATIBU Tawala Mkoa wa Singida Dk. Fatuma Mganga, amewataka Watumishi wa umma wasiwe kikwazo cha kuwakwamisha wafanyabiashara na badala yake wawe wawezeshaji wa kuwasaidia kutatua changamoto zinazowakabili ili biashara zao ziweze kukua.

Alisema hayo jana (Februari 26, 2024) wakati akifungua mafunzo ya fursa za masoko na biashara kwa Maafisa biashara kutoka mikoa ya Dodoma, Singida, Manyara na Tabora yanayofanyika mjini Singida ambayo yameandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara.

“Sisi tuliopo katika ofisi za umma tuwe wawezeshaji wa wafanyabiashara tusiwe wakwamishaji kwasababu sisi hatufanyi biashara, tukajifunze hao wafanyabiashara wanakumbana na changamoto gani kwasababu sisi tupo maofisni hatujui changamoto wanazopata badala yake tunakuwa maofisa hatuwi wawezeshaji,” Dk. Mganga alisema.

Dk. Mganga alisema Maafisa biashara lazima watambue kuwa walengwa wasipopata kile kilichoandaliwa fursa za kibiashara zilizopo nchini hazitatumika na badala yake zitatumiwa na watu wachache wa nje na hivyo wananchi watashindwa kujikwamua na umaskini wataendelea kuvunjwa moyo.

Dk. Mganga alisema wafanyabiashara kufanyabiashara katika mazingira yasio rafiki kwake kunasababisha wengi kuchukua uamuzi mgumu wa kufunga biashara zao.

Alisema Wizara ya Biashara na Viwanda kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikifanya mafunzo ya uwezeshaji biashara na fursa za masoko zinazotokana na majadiliano mbalimbali baina ya nchi na nchi na kikanda na kimataifa.

Aliongeza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kujengeana uwezo katika taratibu za ufanyaji biashara na kujulishana fursa za kibiashara na uwekezaji ndani na nje ya nchi.

Aidha, alisema Serikali imekuwa ikishiriki katika majadiliano mbalimbali ya kibiashara katika ngazi ya kimataifa, kikanda na baina ya nchi na nchi kwa lengo la kutafuta fursa nafuu za biashara, masoko na uwekezaji.

“Kupitia majadiliano hayo fursa nafuu za masoko zilizopatikana ni pamoja na fursa za masoko ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) na Soko la Marekani kupitia Mpango wa African Growth and Opportunity Act (AGOA),” alisema Dk. Fatuma Mganga.    

Aliongeza kuwa pamoja na Tanzania kuwa na fursa na nafuu za masoko na biashara bado kumekuwa na changamoto kadhaa zikiwamo uelewa mdogo wa wadau mbalimbali nchini hususani wafanyabiashara kuhusu fursa hizo na mahitaji ya soko ikiwemo vya uasili wa biashara na ubora ambavyo ni muhimu katika kuyafikia masoko muhimu.

Katika Tawala wa Mkoa huyo alimalizia hotuba yake kwa kuwasisitiza Maafisa biashara pamoja na wafanyabiashara nchini kutumia kikamilifu fursa za ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Dk. Samia Suluhu Hassan, anazozifanya katika nchi mbalimbali ili kuwezesha mahusiano ya kibiashara baina ya Tanzania na wawekezaji wa  Nchi nyingine.



No comments:

Post a Comment