MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba ameiagiza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) mkoani hapa kusimamia ujenzi wa daraja la Minyughe lililopo Wilayani Ikungi linalojengwa na kampuni ya JP Traders Limited ili liweze kukamilika haraka na wananchi waanze kusafiri kutoka upande wa kata ya Minyughe kwenda upande wa kata ya Makilawa.
Serukamba ametoa agizo hilo jana
(Februari 26, 2024) alipotembelea daraja hilo ambalo lilikatika tangu Oktoba
mwaka jana kulikagua kuangalia maendeleo ya ujenzi wake ikiwa ni mfululizo wa
ziara yake ya kukagua miradi ya ujenzi na matengenezo ya barabara, madaraja na
vivuko katika Wilaya zote za mkoani
hapa.
Alisema pia daraja hilo
litakapokamilika TARURA ihakikishe barabara inachongwa vizuri ili iweze
kupitika muda wote na katika bajeti ijayo ifikirie namna ya kulinda Mto Saiwa
ili usiweze kuathiri daraja baadaye hasa kutokana na mwenendo wake wa kupanuka
kila mara.
“Mto huu unasogea kila wakati
na kupanuka, hivyo tusipofanya jitihada za kuulinda itafika wakati daraja
litaelea pekee yake na kuhatarisha hatimaye likabomoka wakati limejengwa kwa
gharama kubwa,”alisema RC Serukamba.
“Utaona gharama za ujenzi wa
daraja hili ni takribani Sh.bilioni mbili ambalo linahudumia kata tatu tu pesa
kama hizi pengine zingeweza kutumika kujenga barabara za kuunganisha Wilaya kwa
Wilaya au Mkoa kwa Mkoa lakini Rais wetu Samia Suluhu Hassan ameona angalau kila
kijiji kwa kijiji kiweze kupitika, wananchi tumshukru sana Rais huyu wa awamu
ya Sita.” alisisitiza.
Aidha, Mkuu wa Mkoa aliwataka
wananchi kuongeza juhudi katika kilimo kwani daraja na barabara itakuwepo kwa
ajili ya kuwarahisishia kusafirisha mazao yao kwa ajili ya kuyapeleka kwenye
masoko kwaajili ya biashara mbalimbali zikiwemo za mazao ya biashara.
Hata hivyo aliwasihi wananchi wabadilike
katika kilimo kwa kuhakikisha wanaongeza matumizi ya mbolea ili kuongeza
uzalishaji wa mazao wenye tija kwao na halmashauri husika.
“Wanasayansi wanasema ekari
moja ya mahindi ukiweka mifuko mitano miwili ya kupandia, mitatu ya kukuzia unapata
maguni 30 hadi 35 kwa ekari moja lakini leo nyie mkipata zaidi ni maguni mawili
au matatu, lazima tutoke huko na namna ya kutoka ni kuongeza matumizi ya
mbolea,”alisema Serukamba.
Awali Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida, Mhandisi Ibrahimu Kibasa, alimweleza Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, kuwa daraja hilo limeanza kujengwa na utekelezaji wake umefikia asilimia 60 na linatakiwa kukamilika Mei 18, 2024.
Alisema hadi sasa kazi
zilizofanyika ni kutengeneza njia ya mchepuko, kupanga mawe na kusuka nondo, kumwaga
zege la chini na la juu na ulindaji wa daraja kwa kutumia mawe ambapo Mkandarasi
wa kampuni ya Mzava M/S JP Traders Limited aliyepewa kazi hiyo kwa kulijenga
kwa Sh, Milioni 556.140, hadi sasa ameshalipwa Sh. Milioni 224.770 sawa na
asilimia 40.4 ya thamani ya mkataba wote.
“Barabara ya Mtamaa - Minyughe
hadi Mtavira ambayo daraja hili lipo ni la muhimu sana kwa wananchi wa kata za
Minyughe na Makilawa kwani maji yakijaa katika daraja wanafunzi wanashindwa
kwenda shule au wananchi kushindwa kufuata huduma za matibabu.” alisema.
Kibasa alitoa mchanganuo kuwa
gharama za kununua vyuma vitakavyowekwa juu ya daraja hilo vinagharimu
Sh.milioni 939 hivyo jumla ya mradi ni Sh.bilioni 1.4 ambapo zikijumlishwa
gharama za kodi bandarini na usafirishaji kutoka Dar es Salaam kuja Singida
gharama zote za mradi zitafikia takribani Sh.bilioni 2 kasoro.
MATUKIO KATIKA PICHA WAKATI WA ZIARA YA UKAGUZI WA UJENZI WA DARAJA
No comments:
Post a Comment