Upatikanaji wa mbegu bora ya alizeti kwa bei ya ruzuku ya Serikali kwa miaka mitatu mfululizo mkoani Singida umeongeza uzalishaji wa zao hilo kutoka Tani 260,382.2 msimu wa 2021/2022 hadi zaidi ya Tani 400,000 msimu wa Kilimo uliopita wa 2022/2023.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter
Serukamba, alisema hayo wakati wa uzinduzi wa usambazaji wa mbegu za alizeti
zenye ruzuku ya Serikali uliofanyika kwenye viwanja vya Kanisa Katoliki mjini
Singida tarehe 3/1/2024.
Akitoa salamu kwa mgeni rasmi Naibu
Waziri wa Kilimo Mhe. David Silinde, Serukamba alisema mafanikio hayo yametokana
na Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuelekeza nguvu
kwenye Kilimo kwa kuwapatia Wakulima mbegu bora ya alizeti yenye ruzuku ya
Serikali.
"Uamuzi huu wenye busara nyingi uliofanywa na Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuwapatia Wakulima mbegu ya Alizeti yenye ruzuku ya Serikali, umesaidia sana wakulima wa Mkoa wetu kuwa na uhakika wa kupata mbegu bora na kwa bei nafuu, na hivyo kuwafanya kushiriki katika uzalishaji wa zao hili" alisema Serukamba
Aidha Serukamba alisema ili
kufikia malengo Mkoa umejiwekea mkakati wa kuongeza uzalishaji wa zao hilo
ambao msimu huu wa 2023/2024, Mkoa wa Singida unatarajia kulima Hekta
323,455.8, kwa ajili ya kuzalisha Tani 523,092.5 za alizeti.
“Ili kutekeleza kipaumbele hiki ambacho pia ni mkakati wetu, Mkoa unahitaji kupatiwa mbegu bora kiasi cha Tani 1,617.3, ambazo tumeziomba kutoka Wakala wa mbegu nchini (ASA), kupitia Wizara ya Kilimo,”alibainisha Serukamba.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. David Silinde, akizungumza na Wakulima, Wataalamu wa ugani na Viongozi katika uzinduzi huo alisema msimu huu Serikali itasambaza hapa nchini mbegu za alizeti Tani 2,045 ikijumuisha Tani 700 chotara kutoka nje ya nchi na zingine Tani 625.4 kutoka makampuni binafsi ya ndani ili kuongeza mavuno.
Naibu Waziri alisema, Mkoa wa
Singida msimu huu utanufaika kwa kupokea mbegu za alizeti Tani 600 ikijumuisha
Tani 315 chotara za thamani zaidi ya Sh. Bilioni 8.58 sawa na asilimia 42.8 ya
mbegu zinazosambazwa hapa nchini.
Aidha Silinde, aliupongeza
Mkoa wa Singida kwa kuongeza uzalishaji wa mbegu na mafuta ya kula ya alizeti
msimu uliopita wa 2022/23 kwa kulima eneo lenye ukubwa wa ekari 131,793.3 lililozalisha
Tani 55,335, za alizeti ghafi ambazo zitakazozalisha mafuta Lita 1,383,826 ambazo
zitapunguza tatizo la mafuta nchini.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa mbegu nchini, Dk. Sophia Kashenge, alisema lengo la wakala huyo ni kumsaidia mkulima kwa kumwezesha mbegu bora ili aweze kufikia malengo aliyojiwekea pia Serikali ilivyokusudia kumwinua mkulima nchini.
No comments:
Post a Comment