Mkuu
wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba ameuelekeza Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya
ya Itigi Wilayani Manyoni kuitafutia ufumbuzi changamoto ya wananchi zaidi ya 2,978
walioomba kumilikishwa kipande cha ardhi, katika kijiji cha Rungwa baada ya
kuishi kwenye eneo hilo kwa miaka 14.
Katika
mkutano wa hadhara na wananchi wa kitongoji cha Mauki, kijiji na Kata ya
Rungwa, Halmashauri ya Itigi Wilaya ya Manyoni alipokutana nao tarehe
(21/11/2023) kwa ajili ya kusikiliza kero Serukamba ametaka mchakato huo mapema
ili kuwezesha wananchi hao kuwa sehemu ya walinzi wa hifadhi ya Rungwa.
Awali
wananchi hao, ambao wengi wao wanatoka katika jamii ya wafugaji, walimweleza
Mkuu wa Mkoa kuwa wamekuwa wakiishi kwenye eneo hilo kwa miaka 14 lakini pamoja
na juhudi zao katika shughuli za uzalishaji mali Serikali haiwatambui hali
inayokwamisha maendeleo yao kiuchumi.
“Hatuna jinsi, Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya naomba muanze mchakato wa kuifanya sehemu hii kuwa Kitongoji…hawa ndio watakaokuwa walinzi wa msitu huu..,” alisisitiza Serukamba.
Baadhi ya wananchi hao waliolazimika kuomba eneo lao kutambuliwa na Serikali ni Paulina Shija, Uzenza Ndaki na Machia Machembe, na walisisitiza kuwa changamoto hiyo imekuwa kikwazo katika kujenga makazi ya kudumu na hivyo kuzorotesha maendeleo.
Hata hivyo alipotakiwa kujibu hoja hiyo Afisa Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, John Makotta, alisema eneo hilo lipo chini ya kitalu cha mwekezaji wa shughuli za uwindaji.
Makotta alifafanua kuwa, sehemu hiyo ni Kitalu cha uwindaji kinachojulikana kwa jina la ‘North Rungwa open area, huku mwekezaji akitarajiwa kuanza shughuli zake hivi karibuni baada ya kuingia mkataba na Serikali.
Pamoja na maelezo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Singida Serukamba, amesisitiza kuanza kwa mchakato wa kuwamilikisha wananchi hao, kutokana na uzembe uliofanywa katika kuwatoa wananchi hao kwa miaka yote 14, hivyo ni lazima liwe sehemu ya Kitongoji cha Kijiji cha Rungwa.
Kwa mujibu wa hifadhi ya Rungwa, wananchi hao walivamia eneo la Mwauki miaka 14 iliyopita lakini pamoja na kuwatoa kwa nguvu mara kadhaa, wamekuwa wakirejea hivyo kusababisha usumbufu kwa mamlaka husika.
No comments:
Post a Comment