MKUU wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba
ametangaza rasmi msako wa kutembelea miradi yote ya maendeleo
inayotekelezwa na Serikali katika Mkoa huo kwa lengo la kujiridhisha na
utekelezaji wa miradi hiyo bila kuchaguliwa mradi wa kukagua.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Singida amesema hayo jana tarehe 25 Oktoba,
2023 mara baada kuhitimisha ziara yake ya ukaguzi wa miradi katika Wilaya ya
Singida, hatua hiyo ya kutembelea mradi mmoja baada ya mwingine kila Wilaya ni
kutaka kuhakikisha utekelezaji wa miradi hiyo unafanyika kwa kiwango
kinachotakiwa pamoja na ubora kwa thamani ya fedha iliyotolewa katika mradi husika
ili wananchi wapate huduma bora na ya kiwango kinachostahili.
Akizungumza na Watendaji wa Mkoa huo Serukamba amesema Serikali
inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikitoa fedha nyingi na
kwa wakati kwa ajili ya maendeleo hivyo ni lazima ikatekelezwa kwa muda
uliokusudiwa kwa manufaa ya Watanzania.
"Nitangaze kuwa baada ya wiki moja nitaanza ziara ya
kutembelea mradi mmoja baada ya mwingine na sitahitaji kupangiwa ni mradi gani
wa kutembelea nitahakikisha nafika kwenye kila mradi ambao unatekelezwa na
nitatembelea miradi yote katika Halmashauri zote za Mkoa wa Singida”
"Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa huu
na Waandisi hakikisheni mnajipanga vyema ni lazima miradi yote itekelezwe kwa
wakati na nyie Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Waandisisi nawaeleza msipende
kukaa maofisini na kusubiria taarifa fikeni kwenye maeneo ya kazi kwa lengo la
kuona kazi zinaendeleaje”
"Na wakati mwingine siyo kufika tu na kukagua kagua na mpango
kazi wa Mkandarasi anayefanya kazi na ikitokea ukarudi ukakuta hajatekeleza
makubaliano unaweza kubadilisha Mkandarasi mwingine na mafundi wengine lengo
kubwa ni kazi kufanyika kwa kiwango na kwa ubora unaohitajika ili ikamilike kwa
wakati" ameeleza Serukamba.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Singida ameeleza kuwa kwa hatua ya sasa
miradi ya afya inaendelea vizuri na inaridhisha lakini miradi ya elimu
inatakiwa kuharakishwa zaidi na ifikapo mwezi Desemba mwaka huu iwe imekamilika
kwa lengo la wanafunzi watakaoingia shule ya awali na kidato cha kwanza wawe na
uhakika wa miundombinu yote ya shule.
Singida ni kati ya Mkoa ambao umepokea fedha nyingi za miradi ya maendeleo na ni miongoni mwa Mikoa ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amefurahishwa na utekelezaji wa miradi hiyo.
No comments:
Post a Comment