WAHANDISI katika Mkoa wa Singida wanao simamia madarasa ya mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) wametakiwa kuhakikisha wanawasimamia Wakandarasi wanaojenga miradi hiyo ili ikamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Maagizo hayo yametolewa leo tarehe 19 Septemba, 2023 na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa hatua za kukamilika miradi hiyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Manyoni na Itigi mkoani humo.
Serukamba amesema kuwa inawezekana Wahandisi wa baadhi ya halmashauri husika wanaweza kuwa ni chanzo cha kuchelewesha kukamilika kwa miradi hiyo kutokana na kutokuwa na desturi ya kwenda kwenye maeneo ya kazi kwa lengo la kukagua shughuli mbalimbali za ujenzi wa miundombinu ya kazi zinazofanywa na Wakandarasi waliopewa kazi hizo.
Amesema kuwa kazi za Waandisi wa halmashauri ni kuhakikisha wanatembelea maeneo ya kazi kwa nia ya kuwakagua Wakandarasi, kuwasimami, kuwashauri, kuwapangia majukumu na kuona hatua za utendaji kazi zinavyoendelea pamoja na kiwango cha utendaji ili kuharakisha ujenzi wa miundombinu hiyo ya shule kutekelezeka kwa ufanisi.
Serukamba akiwa kwenye ziara hiyo ya kikazi kwenye halmashauri mbalimbali ndani ya Mkoa huo amewataka Wahandisi wa halmashauri ambako miradi hiyo inatekelezwa kuhakikisha ifikapo tarehe 30 Septemba mwaka huu miradi yote iwe imekamilika.
Sambamba na hilo amewataka Watendaji wa halmashauri kuhakikisha wanatembelea miradi hiyo kila siku na kukusanya taarifa kila jioni ili kuona ni Mkandarasi gani ambaye anakwamisha miradi hiyo na ikibidi anyang'anywe mradi na kupewa mtu mwingine ambaye anaonesha nia ya kumaliza kazi mapema.
Serukamba amesema Mkandarasi ambaye anafanya kazi kwa kusuasua na kufanya kazi chini ya kiwango hatavumiliwa kwani ni lazima thamani ya fedha ionekane na miradi iishe kwa wakati ili walengwa waweze kutumia madarasa hayo.
No comments:
Post a Comment