Saturday, September 16, 2023

RC SERUKAMBA ATOA MIEZI MIWILI (2) KWA MANISPAA KUTUNGA SHERIA NDOGO YA UDHIBITI TAKA

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, akishiriki shughuli ya usafi wa mazingira wakati wa maadhimisho ya siku ya usafishaji Duniani iliyofanyika Ki Mkoa katika Soko la Msufini kata ya Mghanga katika Manispaa ya Singida.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba ametoa maelekezo kwa Halmashauri ya Manispaa ya Singida, kuhakikisha ndani ya miezi miwili, Baraza la Madiwani likutane kwa ajili ya kutunga sheria ndogo ndogo ambazo zitadhibiti tatizo la uchafu unaofanywa kwa asilimia kubwa na wakazi wa Manispaa ya Singida.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, akizungumza na wafanyabiashara wa Soko la Msufini pamoja na wananchi waliojitokeza kufanya usafi wakati wa maadhimisho ya siku ya usafishaji Duniani iliyofanyika Ki Mkoa katika Manispaa ya Singida.

Serukamba amesema hayo leo Jumamosi Septemba 16, ambayo ni siku ya usafishaji mazingira Duniani inayofanyika kila mwaka Septemba 16, ambapo Ki Mkoa yamefanyika katika Soko la Msufini lililopo katika Manispaa ya Singida kwa lengo la kuikumbusha jamii kuhusiana na suala zima la usafi wa mazingira ili kumwepusha mwananchi juu ya maradhi mbalimbali.

Aidha akizungumza kwa msisitizo, RC Serukamba amesema kuwa uongozi wa Manispaa unatakiwa kuwasimamia kikamilifu wananchi kuhusiana na sula la usafi kwasababu zana za kufanyia usafi yakiwemo magari yapo.

“Ndugu zangu mlioko hapa, wote mtakubaliana nami Singida Manispaa ni chafu sana, na wanaoichafua ni ninyi miliopo mbele yangu, na wanaoshindwa kuwasimamia ni sisi viongozi tuliokaa hapa nyuma leo nimekuja kutoa maelekezo…ndani ya miezi miwili Baraza la Madiwani likutane kutunga sheria ndogo ndogo kudhibiti tatizo la uchafu…,”ameagiza Serukamba.

Amesema wajibu wa usafi na kuyaweka mazingira kwenye hali ya usafi ni wajibu wa kila mmoja hivyo wanaotupa taka ovyo ikiwemo chupa za maji, karatasi na kila aina ya uchafu wanapaswa kuadhibiwa ikiwemo kutozwa faini kwa kiwango kinachofikia hadi shilingi 50,000 ili kuufanya mji katika hali ya usafi.

“Na mimi niwashauri kama nyumbani kwako kuna uchafu na unaona vibaya kulipa ada tafuta chumba chako kimoja weka uchafu wako humo hatutakuuliza una vyumba vyako vinne chagua kimoja weka uchafu wako wote lakini ukitoa uchafu ukauweka nje lazima tutakudai ulipie ada ya taka…,”amesema Serukamba

Hata hivyo, RC Serukamba amepiga marufuku ufanyaji wa biashara kwenye eneo la barabara na kuagiza Jeshi la Polisi kusimamia suala hilo kwa dhati kuanzia siku ya Jumatatu ya wiki ijayo Septemba 18, pamoja na mbele ya nyumba, pembeni mwa kibanda ni marufuku vinginevyo mwenye nyumba atakayeruhusu atapaswa kulipia ada ya leseni ya biashara.

Katika Hatua nyingine Mkuu wa Mkoa huyo amewasisitiza Watendaji wa Mkoa huo kuhakikisha maeneo yote yatakayopitiwa na Mwenge wa Uhuru kuwa safi, kuwaandikisha wakulima ili kupata mbegu, Maafisa Kilimo wa Kata kuongeza maeneo ya kilimo ili kuwa na mavuno mengi.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga, akisisitiza jambo kwa Watendaji na Wananchi waliojitokeza kufanya usafi wakati wa maadhimisho ya siku ya usafishaji Duniani iliyofanyika Ki Mkoa katika Manispaa ya Singida.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, ameuagiza uongozi wa Serikali ya Mtaa inayosimamia Soko la Msufini kuweka utaratibu mzuri utakaowezesha soko hilo kuliweka kwenye hali salama na safi ili kulinda afya za wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.

“Nawaasa wananchi, tuwe tunafanya usafi, hivi leo tumeamua kufanya kwenye eneo hili, lakini yawezekana tungepita nyumba hadi nyumba si ajabu wengine hapa tungekuta hata hamjafagia nyumba zenu, eneo la Soko la Msufini lingekuwa linafanyiwa usafi hata kazi ya kulisafisha ingekamilika kwa muda mfupi, hivyo nawaomba sana tuzingatie usafi ” amesema Dkt. Mganga.

Aidha Dkt. Mganga katika kusheherekea maadhimisho hayo amewasihi wanawake mkoani humo kuwa mfano bora katika utekelezaji wa zoezi la usafi wa mazingira kwa kutambua kuwa mwanamke sifa yake ya kwanza ni usafi wa mazingira pale anapoishi ikiwemo nyumbani kazini  ili kuvutia na kuzuia milipuko ya magonjwa yanayosababishwa na uchafu na si kujikita katika muonekano wa mwili.

Kwa upande wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida imejipanga kuongeza vitendea kazi vya kuzolea taka pamoja na kuendelea kutoa elimu ya usafi wa mazingira kwa wananchi ili kuwawezesha kuwa na uelewa mpana wa udhibiti wa taka, kufanya usafi binafsi kwenye maeneo yao ili kuzuia magonjwa na kupendezesha mji.

Aidha, Katika kuhakikisha mji unakuwa safi, Manispaa imewahimiza wananchi kutoa taka siku iliyopangwa ya uchukuaji katika mitaa husika, kulipa tozo ya taka kwa wakati, kutotupa taka ovyo ili kuepuka uharibifu wa miundombinu ya barabara hususan mitaro ya maji ya mvua.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida Jeshi Lupembe (kulia) pamoja na Diwani wa Kata ya Mghanga, Vellerian Kimambo, wakishiriki zoezi la usafi wa mazingira katika eneo la barabara iliyopo jirani na soko la Msufini kata ya Mghanga ambapo maadhimisho ya siku ya usafishaji Duniani iliyofanyika Ki Mkoa katika Manispaa ya Singida.

Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya Ustawi wa Jamii na Lishe Dkt. Victorina Ludovick (kulia) akiwa na Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Singida Habibu Mwinory wakishiriki zoezi la usafi wa mazingira katika Soko la Msufini kata ya Mghanga ambapo maadhimisho ya siku ya usafishaji Duniani iliyofanyika Ki Mkoa katika Manispaa ya Singida.













Kauli mbiu: “Tuungane Pamoja, Kujifunza, Kupanga na Kuhimiza Uimarishaji Huduma za Udhibiti wa Taka”.

No comments:

Post a Comment