Friday, September 22, 2023

KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE KITAIFA AKEMEA VITENDO VYA RUSHWA.

 

MKIMBIZA Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Abdalla Shaibu Kaim amewataka Watanzania kuhakikisha wanakemea vitendo vya rushwa kwa maelezo kuwa rushwa inakwamisha maendeleo ya Mkoa pamoja na Taifa kwa ujumla.

Ametoa kauli hiyo tarehe 22 Septemba, mwaka 2023 muda mfupi baada ya kumaliza kutembelea, kukagua, kuzindua na kuweka jiwe la msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Wilaya ya Iramba Mkoani Singida na kuzinduliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru ambao umepokelewa kutokea Mkoani Tabora.

Akiwahutubia wananchi wa kata ya Kiomboi, Tarafa ya Kisiriri Wilaya ya Iramba Mkoani Singida muda mfupi baada ya kumaliza kukagua miradi ya maendeleo, amesema kuwa miradi mingi inakwama kutokana na watekelezaji au wasimamizi wa miradi hiyo kutoa au kupokea rushwa kwa nia ya kukinufaisha wenyewe.

Amesema kuwa ili kuwa na miradi bora na yenye kukubalika ni lazima kila Mtanzania kuhakikisha anapinga na kupiga kelele juu ya kuzuia vitendo viovu ambavyo vinatokana na vitendo viovu vya utoaji au upokeaji wa rushwa na kusababisha miradi au huduma kuwa chini ya ubora.

"Tunasema kuwa tupambane na rushwa kwa maana kwamba unaweza kuona kuwa mtu akitoa rushwa au kupokea rushwa anaweza kufanya kazi chini ya kiwango na kusababisha huduma kuwa mbovu.

"Tatizo la rushwa bado lipo nchini na imefika wakati watanzania wanaweza kuichukia Serikali yao kwa kukosa huduma nzuri pale mmoja anapokuwa amepokea rushwa au kutoa rushwa kwani ni wazi kuwa rushwa upotosha haki" amesema mkimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa.

Akizungumzia suala la amani Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge kitaifa amewataka watanzania kuwa mabalozi waaminifu katika kutunza amani ya nchi kwa kusimamia amani, upendo mshikamano pamoja na kuendeleza na kulinda umoja wa kitaifa.

Kuhusu utunzaji wa mazingira Abdalla amewataka watanzania kuhakikisha wanatunza mazingira ili kuepuka kupata magonjwa yanayosababishwa na uchafu na kuepukana na kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo yenye vyanzo vya maji.

Amesema kwa sasa kuna hali ya mabadiliko ya tabia nchi hivyo ni vyema kuhakikisha watanzania wote kwa ushirikiano wa wanatunza vyanzo vya maji na kukaa zaidi ya mita 60 zaidi ya chanzo cha maji.

Sambamba na hilo Abdalla amesema ili kulinda nguvu kazi ya taifa ambapo asilimia kubwa ni vijana kila mmoja awe askari kwa lengo la kupambana na matumizi ya dawa za kulevya nchini.

Amesema kuwa vijana wengi ndo nguvukazi ya taifa hivyo wanatakiwa kutokutumia dawa za kulevya huku akiwashauri watanzaia kujiepusha na uagizaji, usambazaji pamoja na kilimo ambacho ni halamu.

Mwisho.


No comments:

Post a Comment