Siku tatu baada ya Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatma
Mganga kutoa maagizo kwa Mkandarasi anayejenga wodi mbili na nyumba ya
kuhifadhia Maiti Wilayani Manyoni ya kuwalipa staahiki zao mafundi na vibarua
leo Mkuu wa Mkoa huo, Peter Serukamba naye ametembelea eneo hilo na kumuagiza
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manyoni kulipa fedha za Mkandarasi huyo na
kuwalipa mafundi pamoja na vibarua ili kazi iweze kukamilika kwa wakati.
RC Serukamba ametoa maagizo hayo baada ya kupewa taarifa na
Mhandisi wa Wilaya hiyo, Gabriel Mayaya kwamba, kazi ya ujenzi inachelewa kwa
sababu Mkandarasi haonekani eneo la kazi na vibarua hawajalipwa fedha zao jambo ambalo huchangia
kusuasua kwa kazi hiyo ndipo alipotoa maelekezo fedha hizo kukatwa na kuwalipa
vibarua na mafundi huku akimtaka Mhandisi huyo kuongeza usimamizi ili kazi
ikamilike kwa wakati.
"Huwezi kuacha kuwalipa vibarua halafu utegemee kazi
itamalizika, Mhandisi kaa na Mkurungezi chukueni fedha za Mkandarasi lipeni
vibarua wake kwa kuwa inafahamika kiasi wanacholipwa kwa kazi walizofanya"
Serukamba
Aidha amemuagiza Mhandisi Mayaya kuongeza mafundi wengine
kwa kuwa sehemu ya ujenzi iliyobaki ni kubwa na mafundi ni wachache huku muda
ukiwa ni mdogo uliobaki.
"Hatuwezi kumsubiri mtu ambaye hata ‘site’ haonekani,
fedha zake walipeni hao vibarua na tafuteni mafundi wengine ili kazi ikamilike
kwa wakati".
Hata hivyo RC Serukamba amebainisha kwamba mtumishi yeyote
atakayeshindwa kusimamia miradi ya maendeleo Mkoani Singida na akasababisha
fedha kurudi hazina watakuwa wamehatarisha vibarua vyao.
Hata hivyo akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Manyoni, Elias Moleli (Afisa Maendeleo ya Jamii) Wilayani hapo amemuahidi Mkuu
wa Mkoa kwamba wataongeza mafundi na watahakikisha kazi inafanyika usiku na
mchana na kwa viwango vinavyotakiwa.
Aidha Moleli amesema tayari wamenunua vifaa vyote muhimu
vikiwemo mabati nondo na madirisha na mbao kwa ajili kukamilisha kazi hiyo.
MATUKIO KATIKA PICHA WAKATI WA ZIARA
No comments:
Post a Comment