Waandishi wa Habari Mkoani Singida wameshauriwa kutangaza
fursa zinazopatikana katika Mkoa huo ikiwemo kilimo ufugaji na utalii ambazo
zitasaidia kuongeza uwekezaji na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa
ujumla.
Ushauri huo umetolewa leo na Katibu Tawala Mkoa huo Dkt. Fatma Mganga alipokutana na
viongozi mbambali wa chama cha waandishi
wa habari mkoani Singida (Singida Press Club) kwa lengo la kujitambulisha na kujadili namna ya kuboresha
ufikishwaji wa taarifa kwa jamii.
Amesema Mkoa wa Singida una vivutio vingi vya kitalii
ambavyo vikitangazwa vinaweza kuongeza idadi ya watalii na wananchi kuongeza
maslahi kwa wananchi.
Aidha RAS Fatma ameeleza nafasi ya waandishi wa habari
Mkoani hapo katika kukuza viwango vya ufaulu kwa kufanya mahojiano baina ya
shule zinazofanya vizuri na zinazofanya vibaya hasa katika kipindi hiki ambacho
wanafunzi walioripoti shule ni asilimia 87
mkoa mzima.
Hata hivyo amewapongeza kwa namna waandishi hao
wanavyoshirikiana na Serikali kupeleka taarifa kwa wananchi huku akiwakumbusha
kufuata maadili ya kazi yao ili kuleta tija kwa jamii.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama hicho Elisante John
amesema chama kinahitaji kufanya kazi kwa karibu na Serikali ili kuweza
kuwafikishia habari wananchi huku akieleza kwamba wanajipanga kuadhimisha miaka
20 tangu kuazishwa ifikapo Oktoba, 2023.
Aidha mwenyekiti huyo alimumba Katibu Tawala kuona uwezekano wa kuongeza ushirikiano na chama hicho ambacho kina mpango wa kuanzisha miradi yake hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment