Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Mkoani Singida leo tarehe 21.06.2023 wametakiwa kutumia Kituo cha mabasi makubwa na madogo cha mjini hapo kuegesha malori muda wa usiku wakati mchana wakiendelea na huduma za mabasi hayo.
Maagizo hayo yametolewa na Mkuu wa Mkoa huo Peter Serukamba,
wakati wa Baraza la Madiwani lililokutana kupitia hoja za ukaguzi ambapo alibainisha
kwamba ili kuongeza mapato ya Halmashauri hiyo lazima chanzo hicho kitumike kupata
fedha.
Amesema mwezi kuanzia tarehe 1 hadi tarehe 31 mwezi wa tano
wakati malori yakipaki nje ya kituo cha mabasi walikusanya jumla ya Tsh.Milioni
2 na laki moja (2,100,00) lakini baada ya malori kuamriwa kupaki ndani ya Kituo
cha mabasi kwa siku nane (8) walikusanya zaidi ya Tsh.Milioni 1 na laki Tano (1,500,000).
RC amewataka Madiwani wa Halmashauri hiyo kuunga mkono kwa sababu
fedha zitakazopatikana ni kwa ajili ya maendeleo ya Halmashauri ya maendeleo
kwa wananchi wa Manyoni.
Hata hivyo amesisitiza kwamba zoezi la makusanyo ya mapato
ni suala la kufa na kupona hivyo hategemei kuona watu wakienda kinyume na
makubaliano hayo.
Kwa upande wake Dkt. Pius Chaya Mbunge wa Manyoni amesema wao walijaribu kuweka askari kwenye
geti la Kintinku ambapo mapato yaliongezeka kutoka Milioni 2.5 kwa mwezi hadi
kufikia zaidi ya Milioni 20 kwa mwezi hivyo akimhakikishia RC kwamba watamuunga
mkono kufanikisha hilo.
Akikomelea hoja ya kuinua mapato Wilayani Manyoni Katibu Tawala
Mkoa wa Singida Dkt. Fatma Mganga ameshauri kuboreshwa vibanda vilivyopo ndani ya stendi hiyo ili iwe ni
chanzo cha uhakika ili kubadilisha hali ya makusanyo eneo hilo.
No comments:
Post a Comment