MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, leo (Juni 14, 2023) amezindua Mradi wa Skimu ya Umwagiliaji utakaogharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 34. 176 utakaotekelezwa katika Kijiji cha Msingi, Kata ya Msingi Wilayani Mkalama mkoani Singida.
Akizungumza
wakati wa makabidhiano ya mradi huo ambao utatekelezwa kwa kipindi cha miezi
18, alisema Mradi wa Skimu ya Msingi utakuwa na jumla ya eneo la hekta 2,000.
Serukamba
alisema mradi huu utakapokamilika utawanufaisha wakazi 12,000 kutoka Vijiji
vinne vya Ishinsi, Ndurumo, Msingi na Kidi vilivyopo Kata ya Msingi Tarafa ya
Kinyangiri ambao watalima mazao ya mpunga, mahindi na mbogamboga kwa misimu
miwili hadi mitatu kwa mwaka.
Alisema
shughuli kuu zitakazofanyika katika shughuli ya ujenzi wa mradi ni ujenzi wa
bwawa lenye ujazo wa Lita 1,875,000, ujenzi wa mifereji ya umwagiliaji yenye
kilometa 19.12, uchimbaji wa mifereji ya matupio yenye urefu wa kilo mita
42.539, uchimbaji wa mifereji ya kuingiza maji mashambani yenye urefu wa jumla
ya kilometa 34.778.
Shughuli
nyingine zitakazofanyika ni ujenzi wa barabara za mashamba zenye urefu wa
kilomita 36.1, kusawazisha ekari 2,000 za mashamba, ujenzi wa kilomita nane za
barabara na makaravati sita kuelekea ndani ya mradi na ujenzi wa vigawa maji
14, vipunguza mwendo, viumbo angalizi 90, vipitisha maji 90, makaravati 14
pamoja na vivuko nane.
Mkuu wa Mkoa
alisema ili Mkandarasi aweze kuendelea na kazi za ujenzi bila kukwama Tume ya Umwagiliaji
ihakikishe inamlipa Mkandarasi kila anapokamilisha hatua mojawapo ya ujenzi.
Akizungumza
na wananchi wa vijiji vitakavyonufaika na mradi huo katika mkutano wa hadhara
uliofanyika eneo la mradi, Mkuu wa Mkoa huyo aliwataka wananchi kutouza ardhi
kwani lengo la Serikali ni kutaka wenyeji wafaidike na mradi huo.
Serukamba
aliwaondoa hofu wananchi kwamba watanyang'anywa ardhi kwamba hizo ni propaganda
hakuna atakayenyang'anywa na kuagiza wenyeviti wa vijiji kusimamia kuhakikisha
kila mwananchi anapata eneo la kulima.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymondi Mndolwa, alisema
pamoja na kwamba sio jukumu la Tume hiyo kujenga barabara lakini katika mradi
huo zimetengwa fedha kwa ajili ya kujenga kilometa nane ili kuwawezesha
wananchi kupata urahisi wa kusafirisha mazao yao kutoka mashambani.
Alisema katika
mwaka wa fedha ujao Tume hiyo itajenga ghala la kuhifadhia mazao katika kata
hiyo ya Msingi ili wakulima wakishavuna wanayahifadhi kwa ajili ya kusubiri
kuyauza na kwamba ni jukumu la viongozi wa kijiji kutenga eneo litakapojengwa
ghala hilo.
Mndolwa alisema
wakati Serikali inajenga miundombinu hiyo ya umwagiliaji wakulima wana wajibu
wa kulipa ada ya umwagiliaji fedha ambazo zitakuwa zinawekwa kwenye akaunti
maalum ambazo zitatumika kwa ajili ya ukarabati na uendelezaji wa sehemu
nyingine zenye miradi hapa nchini.
“Wakati
mnaushangilia mradi huu mjue kwamba mtakuwa na miundombinu mizuri mkilima
vizuri lakini mtapaswa kulipa ada ya umwagiliaji, msipolipa nitafunga bomba na
nitalifunga bomba sio kwa macho hautaniona nitafunga kwa mtandao kwa hiyo huna
pa kunikamatia,” alisema.
Aidha,
Mkurugenzi huyo aliwataka wananchi wa kata hiyo kumsimamia Mkandarasi aliyepewa
zabuni ya kujenga miundombinu ya umwagiliaji ili akamilishe mradi huo kwa
wakati lakini pia kuhakikisha hawamwibii vifaa.
Naye Mkuu wa
Wilaya ya Mkalama, Moses Machali, alimshukru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa
kutoa fedha za ujenzi wa mradi huu na kwani
utasaidia kuinua uchumi wa Wilaya hiyo.
Kwaupande
wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya
ya Mkalama, James Mkwega, alisema fedha zilizotolewa na Rais Samia Suluhu
Hassan katika mradi huu ni nyingi hivyo watahakikisha wanautunza ilu wanufaike
na kubadili maisha ya Wananchi.
No comments:
Post a Comment