Akifungua mkutano wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Singida jana, alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzingatia sheria inapotekeleza majukumu ya ukusanyaji kodi kwa wafanyabiashara.
Serukamba alisema Serikali imekuwa ikiboresha mazingira ya biashara kwa kuondoa tozo ambazo hazina tija ili kuongeza ukuaji wa biashara na uwekezaji hivyo wafanyabiashara waunge jitihada hizi za Serikali kwa kulipa kodi.
Alisema Serikali pia imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa sekta za biashara na uwekezaji zinakuwa na kutoa mchango stahiki katika kukuza uchumi na pato la taifa kwa manufaa ya Watanzania.
Serukamba aliongeza kuwa ili kuhakikisha uboreshaji huu unakuwa na tija zaidi Serikali imeanzisha idara ya uwekezaji, viwanda na biashara katika Sekretarieti za mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kusimamia kwa karibu tasnia ya biashara nchini.
Alisema Mkoa wa Singida umebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi hivyo sekta za umma na binafsi zinapaswa kufanya kazi kwa pamoja ili kuwaletea wananchi maendeleo na hivyo kukuza uchumi.
"Ndoto yangu ni kuifanya Singida kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji nchini na chombo muhimu kitakachonisaidia kutimiza ndoto hii ni Baraza la Biashara la Mkoa hivyo tuweke mpango mkakati wa kufanya kazi ndani ya miaka mitatu kwa kutangaza shughuli za biashara na uwekezaji," alisema Serukamba.
Aliongeza kuwa Dunia kwa sasa inakabiliwa na mabadiliko makubwa ya teknolojia ambayo yanasababisha kukua kwa haraka kwa uchumi hivyo jitihada zinahitajika kujipanga kukabiliana nazo kwa kuimarisha mazingira wezeshi ya wafanyabiashara.
"Kasi hii ya ukuaji wa teknolojia imeendelea kuibua changamoto mbalimbali katika mazingira ya biashara ambazo zinahitaji utatuzi kwa njia ya majadiliano kuzipitia ufumbuzi changamoto zote zinazokabili ufanyaji wa biashara kwa kuzingatia miongozo iliyopo," alisema Serukamba.
Naye Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Singida, Kitila Katala, alisema sekta binafsi imekuwa ikikabiliwa na mamlaka nyingi za Udhibiti ambazo hudai tozo zaidi ya 18 na hivyo kuongeza mzigo mkubwa kwa wafanyabiashara.
Alisema Serikali iweke utaratibu kwamba tozo zote hizo zilipwe kwa mamlaka moja ili kupunguza mtafaruku na kuwepo majadiliano badala ya kutumia nguvu katika kutekeleza majukumu.
"Mfano hivi karibuni hapa Manispaa ya Singida wafanyabiashara waliofungiwa biashara zao kwa kudaiwa tozo ya huduma (service levy) bila hata kupatiwa muda wa kunieleza ili wakubaliane cha kulipa," alisema Katala.
Kuhusu mashine za kielekroniki za EFD alisema zina ukomo wa kutumia ambapo wafanyabiashara wamekuwa wakitumia fedha nyingi kuzifanyia ukarabati na kuiomba Serikali kama itawezekana mzigo wa kuzikarabati uwe unafanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Kwa upande wake Afisa Biashara kutoka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Herbert Hatibu, alisema wafanyabiashara wawe wanashirikiana na mamlaka hiyo katika kutangaza biashara zao kupitia maonyesho biashara ambayo yamekuwa yakiandakiwa na TanTrade.
MATUKIO KATIKA PICHA
No comments:
Post a Comment