Tuesday, May 02, 2023

Wazazi wetu waliinda misitu haiwezekani sisi tuache kuilinda - RC Serukamba

MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba amepiga marufuku shughuli za kibinadamu ikiwemo kulima, kuchungia mifugo na kuanzisha ujenzi wa makazi katika hifadhi ya Msitu wa Sekenke uliopo Wilaya ya Iramba ili kulinda msitu huo utakaosaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

RC Serukamba amesema hayo leo Mei 2, 2023 wakati akisikiliza kero za wananchi wa Kijiji cha Masagi kata ya Mtoa Wilayani Iramba ambapo wananchi waliiomba Serikali ya Wilaya kuwaruhusu kuchungia mifugo yao kwenye Hifadhi ya Msitu huu.

Mkuu huyo amesema kuwa shughuli za kibinadamu kwenye hifadhi za misitu ndio sababu ya kupelekea ukame ambao umekuwa ukiathiri shughuli za uzalishaji kama vile kilimo hivyo amewataka wananchi hao kuanza kutenga maeneo ya malisho pamoja na kuanzisha kilimo cha nyasi kwaajili ya kulisha mifugo yao.

“Wazee nyie mmekuwa hapa kote huko kulikuwa na misitu kwasababu wazazi wetu waliinda misitu haiwezekani sisi tuache kulinda misitu mlima Sekenke lazima tuulinde, habari ya kuchunga, kukata kuni huko haipo, umefika wakati mtu awe anatenga eneo la kufugia na ardhi ambayo utalima, tubadilike muanze kuwa na maeneo ambayo mtakuwa mnalima nyasi za kulisha mifungu sasa hivi Dunia imefikia huko” Alisema RC Serukamba

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleiman Yusuph Mwenda amesema kuwa kuharibiwa kwa misitu katika kata ya Mtoa na maeneo mengine kumepelekea kuharibu vyanzo vya maji na mvua hali ambayo imeathiri uzalishaji ukilinganisha na hapo awali ambapo kulikuwa na misitu mingi ambayo ilikuwa inavutia mvua.

DC Mwenda aliongeza kuwa awali Wilaya ya Iramba ndio ilikuwa eneo pekee lenye vyanzo vingi vya maji kwa kuwa na Maziwa na mabwawa ikiwemo ziwa Kitangiri, Doromoni, Mabwawa ya Urughu na Mayanzani lakini kwa sasa kutokana na uharibifu wa misitu vyanzo hivyo vimeathirika na vingine kukauka.

Kero nyingine iliyowasilishwa na wananchi wa Masagi ni katika idara ya afya ambapo wananchi wa Kijiji hicho walimueleza Mkuu wa Mkoa kuwa wahudumu wa afya wamekuwa hawatoi huduma nzuri kwa wananchi hasa akina mama wakati wa kujifungua na kupelekea kujifungulia nyumbani.

Kufuatia kero hiyo RC Serukamba amemwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida kuanza kuwafuatia wataalam na wahudumu wa afya ngazi za chini ili kuhakikisha huduma nzuri zinatolewa kwa wananchi.

Pamoja na mambo mengine Rc Serukamba amemwagiza Mganga Mkuu wa Wilaya ya Iramba kumalizia hatua zilizo bakia kwenye Zahanati ya Kijiji cha Masagi ambapo ametoa siku tano Zahanati hiyo ianze kutoa huduma kwa wananchi.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Fatma Mganga akizungumza wakati wa mkutano huo.









No comments:

Post a Comment