Walimu wa shule za msingi na sekondari mkoani Singida wametakiwa kupeleka taarifa mkoani kila mwezi kuhusu hali ya utoro na mdondoko wa wanafunzi ili hatua madhubuti zichukuliwe kwa wazazi ikiwa ni hatua moja wapo ya kupambana na changamoto ya utoro.
Hayo yamesemwa leo tarehe 27.04.2023 na Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akiwa katika ukumbi wa mikutano wa Social Katoliki uliopo mjini hapo ambapo alikutana na wadau wa elimu kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu.
RC Serukamba amesema utoro na mdondoko wa wanafunzi kwa Mkoa wa Singida ni mkubwa ambapo jumla ya wanafunzi 9,134 sawa na asilimia 11 ya wanafunzi walioandikishwa mwaka 2019 wakishindwa kufikia darasa la nne jambo ambalo amesema linaathiri ufaulu wa wanafunzi katika ufaulu na upimaji hasa wanapokuja kufanya mitihani.
Aidha amesema kwa sasa Serikali itahakikisha inawachukulia hatua kali wazazi watakao bainika kuwaficha watoto wasiende shuleni lengo likiwa ni kuinua kiwango cha elimu mkoani hapa.
Aidha RC amebainisha kwamba mbali ya utoro wa wanafunzi changamoto nyingine inayosabisha kurudi nyuma kwa elimu ni ukosefu wa chakula shuleni ambapo ni shule 479 sawa na asilimia 78 ya shule za sekondari 53 sawa na asilimia 40.85 hazitoi chakula kwa wanafunzi jambo ambalo linachangia wanafunzi kutofanya vizuri.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatma Mganga amesema jumla ya wanafunzi 34,029 sawa na asilimia 10.18 hawamudu Stadi za KKK ambapo amewataka Wakuu wa shule kusimamia kikamifu kuhakikisha hali hiyo inakwisha.
RAS amesisitiza walimu kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo matumizi ya vijiti na visoda kama nyenzo itakayomsaidia mtoto kujua kuhesabu kwa mbinu hizo ndizo zikitumika awali na zilionesha mafanikio.
Hata hivyo amewaomba wazazi kusaidia upatikanaji wa chakula cha wanafunzi shuleni hasa kipindi hiki cha mavuno kwa sababu Serikali hazitaweza kutoa kwa kila mtoto ili kuboresha elimu.
Dkt. Mganga amefafanua kwamba Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya shule ikiwepo ujenzi wa madarasa vyoo na kuongeza walimu hivyo kutoa wito kila mdau kuhakikisha anatekeleza wajibu wake.
MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA
No comments:
Post a Comment