Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatma Mganga ameiagiza
Taasisi ya Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kujitangaza kwa kufanya
kazi zenye ubora na kutafuta wateja wapya badala ya kutegemea Serikali na Taasisi
zake.
Kauli hiyo ameitoa leo tarehe 29.03.2023 wakati wa ufunguzi wa kikao cha wadau wa
TEMESA kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi hizo zilizopo Singida
mjini ambapo amesema Serikali imetoa mashine na mitambo mbalimbali kwa taasisi
hiyo ambazo zinaweza kuwa sababu ya kimbilio
kwa wateja wa nje endapo huduma itaboreshwa kwa kiwango kikubwa.
Dkt. Mganga ameagiza taasisi hiyo kufanya utafiti na kubaini
sababu zinazosababisha upatikanaji hafifu wa wateja huku akibainisha kwamba
uboreshaji wa huduma kwa mteja utasaidia kwa kiasi kikubwa Taasisi hiyo kufanya
kazi ki biashara.
"Kwa vifaa ambazo Serikali imevileta tunategemea TEMESA
iwe kimbilio kwa watu wengi, tangazeni kazi zenu muongeze wateja wa nje ya
Serikali na hakikisheni mnaboresha huduma kwa wateja wavutiwe" Dkt. Mganga
Aidha amewataka kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kuondoa
malalamiko ambayo yalikuwepo awali yaliyohusu upatikanaji wa vipuri,
matengenezo kuchukua muda mrefu na gharama kubwa ya matengenezo ambapo
amewataka kuhakikisha wanakabiliana na hali hiyo na kununua vitu kwa pamoja
(balk procurement) ili kupunguza gharama kwa wateja.
"TEMESA imeanzishwa ili kutoa unafuu wa utenegenezaji wa
magari na umeme pamoja na mitambo kwa bei nafuu kuliko wengine hivyo
niwapongeze kama mmeanza hatua za mabadiliko"
Hata hivyo RAS ameishauri Taasisi hiyo kupitia kitengo chake
cha usimikaji wa umeme kuandaa mkakati wa kupima umeme katika majengo ya
Serikali na Taasisi mbalimbali na kutoa
ushauri kwa wamiliki ili kuondoa changamoto za ajali za moto ambazo mara nyingi
zimekuwa zikielezwa kuwa zinasababishwa
na hitilafu za umeme.
Hata hivyo Dkt. Mganga
amesisitiza watumishi hao kuhakikisha wanakuwa waaminifu katika kutunza na
kutumia mali za Umma na kuwekeza katika matumizi ya TEHAMA katika uhifadhi na
ugawaji wa vipuri ili kuepusha upotevu.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TEMESA Mhandisi Hassani
Karonda amesema katika kuboresha huduma zao Serikali katika mwaka wa fedha kwa
mwaka uliopita ilitoa milioni 700 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu lakini
ambapo kwa mwaka wa fedha ujao wametenga Bilioni moja kwa ajili ya kuendeleza
uboreshaji huo.
Awali akitoa taarifa ya kikao kazi hicho Erasto Cheza fundi mkuu wa Karakana Mkoa wa Singida
amesema majukumu ya karakana yao ni kufanya matengenezo ya magari pikipiki na
mitambo ya Serikali, utenegenezaji na usimikaji wa mifumo ya Umeme na viyoyozi
na ameendelea kueleza kwamba wanatoa ushauri wa kitaalamu nyanja za Mhandisi wa
ufundi na umeme.
No comments:
Post a Comment