Jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi Mkoa Singida limeundwa rasmi likienda sambamba na uchaguzi wa viongozi mbalimbali ambao watawakilisha Mkoa huo katika ngazi ya Taifa.
Akiongea baada ya Mkutano huo Mratibu wa Jukwaa hilo ngazi ya
Mkoa Jonathan Semiti amesema kwamba kazi
kubwa iliyofanyika ni kuunda jukwaa na kuchagua viongozi watano huku
wakiwapitisha katika muongozo wa namna ya kuendesha majukwaa hayo.
Semiti amesema lengo la Serikali kuanzisha jukwaa la
uwezeshaji wanawake kiuchumi ni kuhakikisha wanajikomboa kiuchumi kwa
kuwajengea uwezo na kuwakutanisha wanawake ili waweze kujadili fursa za
kiuchumi na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wakati wa utekelezaji wa
shughuli za kiuchumi nchini.
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Shukrani Mbago amesema
jukwaa hilo ni muhimu katika kuwezesha wanawake kwenye masuala ya biashara na
uchumi kwa kutumia fursa zilizopo katika maeneo wanayoishi.
Naye Katibu wa jukwaa
Priscadiana Maleta amefafanua kwamba wao kama viongozi watahakikisha wanafikia
wanawake wote Mkoani hapo kupitia majukwaa ya kata na vijiji ili kuwasaidia
kuziona na kuzifikia fursa zilizopo Serikalini na sehemu nyingine.
Naye Mwenyekiti wa jukwaa hilo Zamda Ahamedi John amebainisha
kwamba jukwaa litawasaidia kuwafikia wanawake wote Mkoani hapo na kujua
changamoto zinazowakabili na kujua mahitaji yao katika kujikwamua.
No comments:
Post a Comment