Wednesday, October 26, 2022

Balozi wa Sweden Nchini Tanzania afanya ziara ya kikazi Mkoani Singida kutembelea miradi minne (4) inayofadhiliwa na Shirika la Kimatafa la Maendeleo la Korea (KOICA).

 

Balozi wa Sweden Nchini Tanzania  Charilotta Ozaki  Makiasi (wa tatu kutoka kushoto).

Balozi wa Sweden Nchini Tanzania  Charilotta Ozaki  Makiasi 26.10.2022 amefanya ziara ya kikazi  Mkoani Singida ya kutembelea miradi minne (4) inayofadhiliwa na Shirika la Kimatafa la Maendeleo la Korea (KOICA) chini ya uratibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia maswala ya kijinsia (UN Women)

Akiwa Mkoani hapa Balozi ametembelea miradi ya jengo la soko la mazao ya mboga mboga lililojengwa Wilayani Ikungi, Kilimo cha Alizeti na Ujenzi wa ghala la Mazao kwa ajili ya uhifadhi wa alizeti lililojengwa katika Kijiji cha Mnang'ana Kata ya Sepuka Wilayani hapo.

Hata hivyo Bolozi alitembelea Kituo cha kupinga ukatili wa kijinsia ambacho kimejengwa Wilayani hapo na kinapokea taarifa mbalimbali kuhusu wahanga wa matukio ya kijinsia.

Akiongea na Wakulima wa Mnang'ana Balozi mara baada ya kutembelea mradi wa jengo la ghala la kuhifadhia mazao linalotekelezwa na Shirika la Farm Afrika amewapongeza Wanawake wa eneo hilo kwa ushiriki wao katika utekelezaji wa kilimo cha alizeti ambapo amesema ameweza kuiona nguvu ya wanawake wa Tanzania katika kuinua uchumi.

Amesema nguvu ya wanawake ni kubwa na anategemea kuona mapinduzi makubwa katika kuongezeka kwa uzalishaji wa zao la alizeti kupitia elimu ambayo wanapatiwa kupitia Shirika la Farm Afrika ikiwemo matumizi ya mbegu bora uhifadhi salama wa mazao pamoja na undelezaji wa mnyororo wa thamani.

Aidha, Balozi ameendelea kueleza kwamba katika ziara yake hiyo amejifunza kwamba ushirikishwaji wa wanawake katika shughuli za kiuchumi na ugawanaji wa rasilimali kwa usawa ni chanzo kikubwa cha kuleta mabadiliko ya uchumi fikra na maendeleo kwa ujumla.

Hata hivyo Balozi amewapongeza Wanawake na wa Kata  ya Sepuka  na wale waliojiunga na AMCOS kwa jitihada zao za kujifunza kilimo na kukitekeleza ambapo amesema atafikisha maombi yao nchini Swedeni kuhusu upatikanaji wa zana za kilimo ikiwemo trekta.

Kwa upande wake Tumaini Elibariki Mratibu wa Mradi wa Alizeti na Ujenzi wa Ghala la Mnang'ana kutoka Shirika la Farm Afrika amesema wakulima wamekuwa na mwitikio mkubwa katika kuzalisha alizeti na watafaidika na uwepo wa ghala hilo.

Amesema wakulima hao wamepata faida ya elimu ya masoko na mradi huo umewafikia wanawake na wakulima wapatao 500 ambapo eneo hilo limekuwa kama Kituo cha kutolea mafunzo kwa wakulima wengine.

"Mradi huu unawezesha wanawake ki uchumi na kupitia  Shirika la Farm Afrika wanawake wamepata mafunzo ya kuongeza thamani na uendelezaji wa biashara na kilimo cha alizeti" alisema Tumaini

Hata hivyo Tumaini alieleza kwamba kupitia Shirika hilo wameweza kuboresha chama cha ushirika cha Mnang'ana na vyama vilivyopo vijiji vya jirani ikiwemo Amunyu ambapo wamejifunza matumizi ya mbegu bora namna ya upandaji na matumizi sahihi ya pembejeo.

Kupitia Shirika la Farm Afrika wameitaka jamii hiyo kuongeza maeneo ya Kilimo na kuhakikisha wanalima alizeti kwa wingi kwa kuwa wamepata fursa ya mafunzo ya mazao hayo huku akiwasihi kuzalisha mbegu zao wenyewe za kuazimiwa (QDS) kupitia baadhi ya wakulima ili kupata mbegu kwa wakati.

kwa upande wao wanawake na Wakulima wa Amcos ya  Mnang'ana  wamewashukuru wadau wa Maendeleo wakiwemo Farm Afrika  kuwajengea  ghala la kuhifadhia alizeti ambapo mfumo wa stakabadhi ghalani unatumika.

Wamesema ghala hilo litawasaidia kuhifadhi mazao yao wakati wa kusubiria upatikanaji wa soko la uhakika na kuepuka upotevu au kuharibika kwa mazao yao.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Kilimo Wilaya ya Ikungi Gurisha Msemo amesema Mradi huo unatekelezwa katika vijiji vinne vya Kipumbuiko, Irisi, Munyo na Mnang'ana ambapo umeweza kuwafikia wananchi kuanzia elfu sita (6000) mpaka elfu 14 (14,000).

Msemo alisema katika mpango wa matumizi bora ya ardhi Mradi kwa kushirikiana na Serikali ya vijiji ulitarajia kutoa hati miliki za ardhi 6000 katika vijiji hivyo lakini mpaka kufikia sasa jumla ya hati 5550 zimekwisha tolewa.

Mradi huo ulianza kutekelezwa Octoba 2020 na unatarajia kukamilika mwezi Machi 2023 alimalizia kueleza Msemo.

No comments:

Post a Comment