Wakurugenzi wa Halmashauri Mkoani
Singida wametakiwa kuunda Kamati ndogo ambazo zitakuwa zikikutana kwa wiki mara
mbili katika kila Halmashauri ili kutathimini mapato ya kila chanzo cha fedha
huku Madiwani waliotumia fedha za Halmashauri kinyume na utaratibu wakipewa siku
tano kurejesha fedha hizo.
Akiongea katika ukumbi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba amesema
ni lazima kuundwa kwa kamati hizo ambazo zitashughulikia upotevu wa mapato
katika kila Halmashauri kwa kuwa swala hilo ni la kufa na kupona.
Aidha ameonya tabia ya baadhi ya Watendaji
ambao wengi wao wanakusanya hela katika vyanzo mbalimbali vya fedha pasipo
kuipeleka Benki jambo ambalo limekuwa likisababisha upotevu wa fedha za
Halmashauri.
Hata hivyo ametumia Mkutano huo wa
Baraza la Madiwani kuwaonya Madiwani wote ambao wanahusika na ukusanyaji wa
mapato kazi ambayo ingefanywa na watendaji wa Halmashauri, huku akiwaasa Madiwani
kutenganisha majukumu yao ili waweze kuwasimamia.
"Madiwani tuepuke kufanya
vitendo ambavyo vitasabisha kushindwa kuwasimamia Watendaji, ukianza kukusanya
Kodi ikatokea upotevu hakuna atakayeweza kukuuliza na Mtendaji akifanya kosa
hilo hutaweza kumuwajibisha". Alisema Serukamba
Amesema kiwango cha makusanyo katika
kipindi cha robo mwaka kwa baadhi ya Halmashauri Mkoani hakiridhishi hivyo ni
jukumu la kila Mkurungezi wa Halmashauri kupitika upya vyanzo vyake vya mapato
na kuhakikisha fedha hazipotei.
Hata hivyo RC Serukamba
amewakumbusha Madiwani na Watendaji wa Kata na Vijiji kuhakikisha kwamba
wakulima wanaanza kuandaa mashamba yao kwa wakati kwa kuwa Mkakati wa Mkoa kwa
mwaka huu ni kuongeza uzalishaji wa mazao ya alizeti mahindi mpunga mbaazi na
viazi.
Amesema Mkoa umejipanga kuongeza
uzalishaji wa alizeti kwa kuongeza maeneo ya kulima ili kulifanya Taifa lijitosheleze
kwa mafuta ya kula huku akifafanua kwamba Serikali imeboresha mazingira ya
kilimo kwa kupunguza bei ya mbolea na ruzuku katika mbegu Bora za kilimo.
RC Serukamba amewataka Madiwani na Watendaji kuendelea kuwahamasisha wananchi kukata Bima ya afya ya CHF iliyoboreshwa ili kuimarisha Afya za watu na kuimarisha uchumi wao.
No comments:
Post a Comment