Jumla ya kilo Mia tano (500) za mbegu bora za alizeti aina ya Certified 1 zenye thamani ya Tsh. Bilion 2.5 zimetengwa kwa ajili ya kugawiwa wakulima wa mkoa wa Singida ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo na kupunguza uagizaji wa mafuta toka nje ya nchi.
Akihutubia wananchi na wakulima wa Wilaya ya Iramba leo
tarehe 27.09.2022 katika viwanja vya Halmashauri ya wilaya Iramba Mkuu wa Mkoa
huo Peter Serukamba amesema Mbegu hizo
zenye ruzuku ya Serikali zitauzwa kwa bei ya Shilingi Elfu tano (5,000) kwa kilo
moja badala ya Tsh. 8,000.
Aidha amesema Serikali itatao ruzuku ya mbolea kwa wakulima
wote watakaojiandikisha kwenye mfumo maalum wa kupata ruzuku ambapo mfuko wa
kilo 50 wa UREA NPKs na DAP utauzwa kwa Tsh.
70,000 badala ya Tsh. 124,734 wakati CAN itauzwa kwa Tsh. 60,000 badala ya
131,676 na SA Tsh. 50,000 badala ya 82852.
Aidha Serukamba amesema kwamba katika bajeti ya mwaka 2022/23
Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu katika miradi ya
umwagiliaji Wilaya ya Iramba katika bonde la wembere linalounganisha Wilaya ya
Ikungi na Iramba na Wilaya ya Mkalama ambapo kutakuwa na ujenzi wa skimu ya
umwagiliaji na bwawa katika kata ya Msingi.
Hata hivyo RC Serukamba amesema kwamba njia pekee ya kuondoa
umaskini, kuondoa uhaba wa mafuta ya kula na kuongeza usalama wa chakula nchini
ni kukuza kilimo kwa kuiongeza eneo la uzalishaji wa kilimo cha umwagiliaji
ambapo kutasaidia kuongeza ajira na upatikanaji wa mali ghafi za viwandani.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleiman Mwenda
amesema lengo la kongamano hilo ni kuonesha wakulima njia ya kutatatua
changamoto walizokumbana nazo msimu uliopita kwa kuwa wana jukumu la kuongeza uzalishaji
wa zao la alizeti na Pamba na kuwaondolea wananchi umaskini.
Amesema wamewaalika Makampuni 16 ya uzalishaji na usambazaji
pembejeo za kilimo wauzaji na wakopeshaji wa matrekta pamoja na mabenki
mbalimbali ili waweze kutoa muongozo wa upatikanaji wa pembejeo na mikopo kwa
wakulima wa Iramba.
Naye Afisa kilimo na ufugaji wa Wilaya ya Iramba Marietha Kasongo amebainisha kwamba Wilaya imelenga kulima hekta 127,594 za mazao ya chakula na hekta 134,176.4 za mazao ya biashara.
Aidha Kasongo ameeleza kwamba Wilaya ya Iramba inakabiliwa na
changamoto za uzalishaji mdogo wa mazao kunakosababishwa na upatikanaji hafifu
wa mbegu bora za mazao, matumizi hafifu ya zana za kilimo na uwepo wa visumbufu
vya mazao.
Changamoto nyingine ni wakulima kutozingatia matumizi ya
kanuni bora za kilimo upungufu wa wataalamu, miuondombinu mibovu ya umwagiliaji
na mabadiliko ya tabia ya nchi alisistiza Marietha Kasongo.
MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA WAKATI WA SIKU YA UFUNGUZI WA KONGAMANO LA UZINDUZI WA MSIMU WA KILIMO 2022/2023 WILAYANI IRAMBA
Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akiendesha Trekta ikiwa ni ishara ya ufunguzi rasmi wa kongamano la uzinduzi wa msimu wa kilimo 2022/2023 katika uwanja wa ukumbi wa halmashauri ya Wilaya ya Iramba mkoani Singida.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akisisitiza jambo wakati akizungumza na wadau mbalimbali wa kilimo walioshiriki siku ya ufunguzi wa kongamano la uzinduzi wa msimu wa kilimo 2022/2023 wilayani Iramba.
No comments:
Post a Comment