Friday, March 28, 2014

WARSHA YA MAFUNZO KWA WAFUGAJI NYUKI NA WAJASIRIAMALI WA MAZAO YA NYUKIN MACHI 25 - 26, 2014


“Asali ni chakula na pia Asali ni dawa, Asali inatakiwa ibaki na ubora uleule toka kwenye mzinga mpaka kwa mtumiaji, unapochemsha asali au unapoiweka katika chupa zilizotumika mfano chupa za Konyagi unaharibu ubora wa asali hiyo”, Hassan.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Liana Hassan ametoa angalizo hilo wakati akifungua warsha ya mafunzo kwa wafugaji nyuki na wajasiriamali wa mazao ya nyuki mkoani Singida iliyoandaliwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Hassan amesema wajasiriamali na wafugaji hao wanapaswa kufuata taratibu na kanuni ambapo wataelekezwa katika mafunzo hayo kwani asali ni rahisi kuharibika isipotunzwa vizuri.

Ameongeza kuwa ufugaji nyuki una hatua muhimu nne ambazo ni kupata mzinga, kuuweka mzinga sehemu ambayo nyuki wataufikia na kuishi, kuvuna mazao ya nyuki na hatua ya nne ni kuchakata na kufungasha mazao ya nyuki (asali na nta) hatua mbayo bado ina changamoto hasa kwa wafugaji na wajasiriamali wadogo.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Liana Hassan akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake (hawapo pichani).

Kwa upande wake Meneja Msaidizi Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kanda ya kati Joyce Chonge amesema mafunzo hayo yametolewa kwa wajasiriamali na wafugaji 30 wa Mkoa wa Singida ambao wameelimishwa juu ya usalama na ubora wa mazao ya nyuki, pamoja na nama ya kupata masoko ya mazao hayo.

Chonge amesema uhamasishaji juu ya ufugaji nyuki umefanyika vizuri hivyo hatua inayofuata ni kutoa elimu juu ya sheria na kanuni za ufugaji nyuki na uuzaji wa mazao ya nyuki kabla ya utekelezaji wa sheria hiyo miaka mitatu ijayo.

Amesema baada ya miaka mitatu asali itakayokuwa na sumu, maji au imefungashwa katika chupa zilizotumika kama za konyagi, itamwaga na mhusika atatozwa faini kati ya shilingi elfu hamsini hadi milioni moja au kifungo cha mwaka mmoja au adhabu zote mbili yaani kifungo na faini.
Meneja Msaidizi Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kanda ya kati Joyce Chonge akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani). 
Aidha, Afisa Nyuki Kanda ya kati Mathew Robert Kiondo amesema mtu yeyote akitaka kufanya biashara ya mazao ya nyuki anatakiwa kujisajili kwanza ambapo anatakiwa kuwa na leseni ya biashara, awe mlipa kodi ndipo afisa nyuki wa eneo alipo amkague kabla ya kumruhusu kufanya biashara hiyo.

Kiondo ametoa rai kwa watumiaji wote wa mazao ya nyuki kutokukubali kuuziwa asali katika chupa iliyotumika akitoa mfano kuwa huwezi kukubali kununua maji ya kunywa katika chupa ya soda iliyotumika hivyo hivyo katika asali.
Afisa Nyuki Kanda ya kati Mathew Robert Kiondo akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani).
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru Wakala wa Huduma za Misitu kanda ya kati kwa kutoa mafunzo hayo.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Rey Products cha Manispaa ya Singida Rehema Hamis amesema mafunzo hayo yamewasaidia kufahamu juu ya sheria za ufugaji nyuki na uuzaji wa mazao ya nyuki hivyo itawasaidia kufanya biashara hiyo kwa ufanisi na kwa kufuata taratibu na sheria.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Rey Products cha Manispaa ya Singida Rehema Hamis akiwaeleza waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya mafunzo hayo.
Naye Mwenyekiti wa kikundi cha Sombi na Maendeleo cha Msikii Singida Vijijini Sombi Jaksoni Sombi amesema amejifunza jinsi ya uvunaji wa asali iliyokomaa na pia mafunzo hayo atayafikisha kwa wanakikundi wenzake.

Sombi amesema wafugaji nyuki na wajasiriamali wa mazao ya nyuki hawanabudi kufuata taratibu na sheria walizofundishwa katika semina hiyo kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.

Mwenyekiti wa kikundi cha Sombi na Maendeleo cha Msikii Singida Vijijini Sombi Jaksoni Sombi akimueleza mwandishi wa habari  juu ya mafunzo hayo.
Mafunzo ya kuhusu usalama, ubora na masoko ya mazao ya nyuki yamefanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa mikutano ofisi ya Mkuu wa Mkoa, mafunzo hayo yamejumuisha sheria na kanuni za ufugaji nyuki na mfumo wa ufuatiliaji na udhibiti wa mabaki ya kemikali katika asali.

Washiriki wamejifunza pia sera ya TFS ya ugawaji wa vifaa vya ufugaji nyuki kwa wadau, vifaa vya ufugaji nyuki na umuhimu wake katika kuboresha mazao ya nyuki, biashara na masoko ya mazao ya nyuki na uzalishaji na utengenezaji wa nta.

Baadhi ya washiriki wakifuatilia mafunzo ya usalama, ubora na masoko ya mazao ya nyuki yaliyoandaliwa na TFS katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

No comments:

Post a Comment