Monday, August 01, 2022

Wakumbushwa kuongeza umakini katika kupokea mafunzo ya Sensa mkoani Singida

 
Makarani na Wasimamizi wa maudhui wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022  Mkoa wa Singida wametakiwa kuongeza umakini ikiwa ni pamoja na kupokea mafunzo yanayoendelea kutolewa katika ngazi za wilaya kwa kuwa ndio wahusika watakao kutana na wananchi wakati wa kuwahesabu.

Wito huo umetolewa leo na Mratibu wa Sensa Mkoa wa Singida Naing’oya Kipuyo  alipotembelea maeneo ya Wilaya ya Singida vijijini na Manisapa ambapo mafunzo hayo yanaendelea huku akiwasisitizia kwamba watakaoshindwa katika mitihani yao hawataendelea na mafunzo kwa kuwa Serikali inataka Watumishi watakaoweza kuleta matokeo yaliyotarajiwa.

Kipuyo amesema mafunzo hayo yatahusisha watendaji wa Kata Makarani, Maafisa Tehema, Wasimamizi wa maudhui  ambayo yatadumu kwa muda wa siku 19 huku Watendaji wa  Kata wapatao 139 Mkoa mzima watapata mafunzo hayo kwa muda wa siku mbili tu kuanzia tarehe 31 Julai 2022 mpaka tarehe 1 Agosti 2022 ili waweze kuendelea na zoezi  la uhamasishaji  katika maeneo yao.

Mratibu wa Sensa Mkoa wa Singida Naing’oya Kipuyo akizungumza na waandishi wa habari 

Aidha Kipuyo alifafanua kwamba kutakuwa na kikao cha Kamati ya Sensa ngazi  ya Kata tarehe 21, Agosti 2022  ambacho kitawahusisha Madiwani na watendaji wa Kata lengo likiwa ni kuhakikisha  zoezi linaratibiwa vizuri.

Hata hivyo amepongeza utekelezaji wa majukumu ya utoaji wa mafunzo ya namna ya kukamilisha zoezi hilo ambapo amebainisha kwamba katika mkoa wa Singida kuna vituo 22 vya kutolea mafunzo   ambapo vyote hakuna changamoto iliyojitokeza.

“Sisi kama wasimamizi wa ngazi ya mkoa tunaamini zoezi hili litafanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa sababu tunao Makarani wenye uwezo mkubwa kutokana na namna walivyopatikana kupitia sifa na vigezo mbalimbali vilivyotumika kuwapata” alisema Kipuyo.

Bwana Kipuyo ameeleza kwamba mkoa wa Singida una jumla ya Madarasa 28 ambako mafunzo yanaendele na jumla ya makarani 5449  ambao watapatikana kupitia wakufuzi walipata mafunzo ngazi ya pili ya mkoa.

Akimaliza maelezo yake Kipuyo amewashauri  wananchi kujitokeza kuhesabiwa siku ya tarehe 23 mwezi  wa Nane (8) 2022 na kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi kwa Makarani na taarifa za watoto na walemavu bila ya kuwaficha ili waweze kuhesabiwa.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu shule ya msingi Mramba Rukia Swido ambaye pia ni Mwenyekiti wa Makarani katika kituo cha Ilongero amesema ili waweze kufanikiwa Makarani wanaaswa kuwa na haiba ya uvaaji ili waweze kukubalika katika jamii watakayokuwa wakiihesabu kwa kuwa uvaaji huweza kusababisha mtu kupokelewa vibaya katika jamii.

Mwalimu Rukia akaendelea kufafanua kwamba wakimaliza mafunzo hayo watashuka ngazi za chini mpaka kufikia kwenye vitongoji ambapo watatumia lugha nzuri na yenye ushawisha pamoja na kuwahakikishia wateja wao kwamba taarifa hizo zitabaki kuwa siri baina ya Karani na mhojiwa.

Hata hivyo Mwalimu Rukia amesema kwamba watazingatia mila na desturi za kila mahala ili wasionekane kama wavamizi jambo ambalo litawasaidia kuapata taarifa muhimu kwa kuwa Serikali imeweza kuwaamni. 

Elizabeth Ramadhani ni Mtendaji ni wa Kata ya Ntonge ameishukuru Serikali kwa uamuzi wake wa kutoa semina ya siku mbili ambayo ameeleza kwamba itawasaidia katika kuendesha majukumu yao ya uhamasishaji kwa jamii kuhusu zoezi hilo.

Ameeleza kwamba watafanya jukumu hilo kwa ufasaha na kwamba habari watazifikisha katika kamati zote za sensa pamoja na vikao mbalimbali kama sehemu ya kuhamasisha ushiriki wa kila mwananchi katika zoezi hilo.

Kwa upande wa wasimamizi wa maudhui mwalimu Filibert Salvatory Limo kutoka shule ya Ikanoda amesema wakufunzi wamewafundisha miongozo mbalimbali ambayo imewapatia mwanga mkubwa na wameweza kutambua namna ya kuendesha na kusimamia zoezi kwa weledi ili kuandika historia mpya ya nchi yetu.

Naye Mtendaji wa Kata ya Mungumaji Bakari Ntandu amesema mafunzo ya siku mbili waliyoyapata yamekuwa chahu kwao katika kuimarisha uhamasishaji kwenye vijiji na vitogoji wanakofanya kazi huku akiendelea kuiomba Serikali kuendela kukutana na makundi maalum kama boda boda jambo ambalo litasaidia kuongeza uelewa wa wananchi.

Aidha amewataka Makarani na wasimamizi wao kuwasikiliza wakufunzi kwakuwa wao ndio watakaoleta mafanikio ya zoezi hilo.




Mafunzo yakiendelea

mwisho

No comments:

Post a Comment