Friday, August 26, 2022

Watoto 363,315 chini ya umri wa miaka mitano kupatiwa chanjo ya Polio Mkoani Singida.

Mkoa wa Singida unatarajia kutoa chanjo ya matone dhidi ya Ugonjwa wa Polio kwa watoto 363,315 wenye umri chini ya miaka mitano ili kujikinga na maradhi hayo.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba katika kikao cha uhamasishaji wa Kampeni ya utoaji wa chanjo ya matone dhidi ya Ugonjwa wa Polio kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akizungumza na viongozi wa Dini mbalimbali na Wadau wa Afya katika kikao cha uhamasishaji wa Kampeni ya utoaji wa chanjo ya matone dhidi ya Ugonjwa wa Polio kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi hiyo.

RC Serukamba amesema Halmashauri zote za Mkoa huo zitashiriki katika utoaji wa chanjo hizo ambapo Wilaya ya Iramba inatarajiwa kuwafikia watoto wasiopungua 56,360 Wilaya ya Singida inatarajia kuwafikia watoto 58,197 Manyoni 45,416 Manispaa 39,841 na Wilaya ya Ikungi watoto 77,638

Wilaya nyingine ni Mkalama ambapo inatakiwa kuwafikia watoto 51,658 na Itigi ambayo jumla ya watoto 34,205 watakaopata chanjo ya matone ya Polio alieleza RC Serukamba.

Aidha Serukamba amesema kauli mbiu ya Kampeni hiyo ni "Kila tone la chanjo ya Polio litawekwa, Tanzania salama dhidi ya Ugonjwa wa kupooza" ambapo kupitia kampeni hiyo inategemewa watoto wote wenye umri wa chini ya miaka mitano watapatiwa.

Hata hivyo RC Serukamba amesisitiza kwamba katika maandalizi hayo wataalamu wa afya wataendesha zoezi hilo katika vituo vya kutolea huduma ya  afya na kwa kutumia njia ya mkoba na kwamba kampeni hiyo itaendeshwa nyumba kwa nyumba, mtoto kwa mtoto ili kuwafikia wote.

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa wakuu wa Wilaya kupitia kamati za Afya ya msingi za Halmashauri kusimamia utoaji wa huduma ya chanjo kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya na zitakazotolewa kwa njia ya mkoba ili kuwafikia watoto kwa asilimia 100.

RC Serukamba amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha watoto wote waliokosa chanjo ya awamu ya kwanza na pili wahakakishe wanapata awamu hii.

Akimalizia hotuba yake Mkuu wa Mkoa huyo akawataka wananchi kuhakikisha wanajitokeza kushiriki katika kampeni hiyo na kuwapeleka watoto wao kupata chanjo kwa ajili ya maisha yao.

Kwa upande wake Mratibu wa chanjo hiyo ki mkoa Habibu Mwinorya amesema kampeni hiyo inaanza tarehe 28 Agosti, 2022 wakati uchanjaji utanza tarehe 1 Septemba, 2022.

Habibu amebainisha kwamba chanjo kiasi cha dozi 350,000 zimekwisha sambazwa katika Halmashauri zote Saba za Mkoa wa Singida na mpaka sasa zimekwisha pelekwa katika vituo vyote vya kutolea huduma.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Victorin Ludovick akizungumzakabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Singida.

Mratibu wa chanjo hiyo ki mkoa Habibu Mwinorya akiwasilisha mada wakati wa kikao hicho.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama akichangia hoja wakati wa kikao hicho.



Kikao cha kampeni ya chanjo kikiendelea


No comments:

Post a Comment