Wednesday, July 27, 2022

Rc Mahenge Aagiza Taasisi Zinazohusika na Barabara Kutumia Bajeti zao Kuleta Maendeleo kwa Wananchi

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge akizungumza wakati akifungua kikao cha Bodi ya barabara  kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge ameagiza fedha za barabara zilizotengwa kupitia Taasisi zinazohusika na uendelezaji wa barabara wakiwemo wakala wa barabara za mijini na vijijini TARURA na Wakala wa barabara TANROADSS Mkoa wa Singida zitumike kuleta mabadiliko makubwa kwenye miundombinu ya barabara na kuleta maendeleo kwa wananchi.

Agizo hilo amelitoa leo tarehe 27.7.2022 katika kikao cha Bodi ya barabara kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo ambapo alisema Serikali imetenga fedha nyingi kwa ajili ya matengenezo na ufunguzi wa barabara mpya ili ziweze kusaidia maendeleo ya wananchi.

RC Mahenge amewataka viongozi wa TARURA na TANROADS kuhakikisha fedha hizo zinatumika vizuri kukarabati na kuanzisha barabara mpya katika maeneo yenye changamoto za upitaji ili kukamilisha kauli ya tunawafikisha pasipo fikika.

“Bado yapo maeneo ya mkoa wa Singida ambayo yana changamoto kubwa ya miundombinu ya barabara hivyo ajenda hiyo ni muhimu kujadiliwa kwa kina kwa kuwa ni chombo cha kuleta maendeleo ya wananchi” Alisema.

Aidha RC Mahenge ametumia muda huo kuwapongeza Wabunge wa Mkoa wa Singida kwa ushirikiano wao katika kuwaletea maendeleo Watanzania wa mkoa wa Singida kwa kupambania upatikanaji wa fedha za barabara kwa kiasi kikubwa.

Aidha amewataka Meneja  wa barabara zote mkoa wa Singida  kuongeza usimamizi wa Makandarasi  ambao wanachukua kazi wakati hawana uwezo wa kutosha jambo ambalo limekuwa ni kero kwa wananchi hasa wa wilaya ya Manyoni ambapo Mkandarasi alipewa fedha za barabara ya majengo mpaka hospitali ya wilaya  lakini mpaka sasa haijakamilika.

Mbunge wa Singida Mashariki Jumanne Miraji Mtaturu akizungumza wakati wa kikao hicho.


Naye Mbunge wa Singida Mashariki Jumanne Miraji Mtaturu amesema pamoja na jitihada za kutengeneza na kufungua barabara mpya lakini kasi ya uharibifu wa barabara hizo imekuwa ikiongezeka jambo ambalo amewataka wataalamu kuangalia chanzo cha tatizo ikiwemo upitishaji wa mifugo kwenye barabara na matumizi ya mabasi madogo “NOHA” kwa kuwa imeonekana sehemu mbalimbali wanakotumia usafiri wa aina hiyo  barabara zinaharibika zaidi.

Hata hivyo ameomba kuwepo kwa taa za barabarani katika miji midogo ikiwemo Ikungi na maeneo mengine ili kuweza kuchangamsha mji jambo ambalo Meneja wa TANROADS na TARURA wamelipokea na kuahidi kulifanyia kazi.

Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida Mhandisi Tembo Devid akizungumza wakati wa kikao hicho.


Awali akitoa taarifa ya Mkoa Meneja wa TARURA Mhandisi Tembo Devid amesema mkoa una mtandao wa barabara upatao KM 5,666.412 ikijumuisha barabara za mkusanyo (collector roads) yenye KM 1946.08, Barabara za mrisho (feeder roads) KM 2840.62 na barabara za kijamii KM 863.20

Mhandisi Tembo ameendelea kusema kwamba jumla ya KM 1360.6 sawa na asilimia 24 zina hali nzuri na zinapitika majira yote ya mwaka wakati KM 1700.8 sawa na asilimia 30 zina hali ya wastani  na  KM 2607.9 sawa na asilimia 46 zina hali mbaya  na hupitika majira ya kiangazi alibainisha Mhandisi Tembo.

Meneja  wa  TANROADS Mkoa wa Singida Mhandisi Msama Kosani Msama akizungumza wakati wa kikao hicho.


Kwa  upande wake  Meneja  wa  TANROADS Mhandisi Msama Kosani Msama amesema katika mpango wa bajeti wa mwaka 2022/23 Mkoa wa Singida wameweka mpango wa Uwekaji wa taa za Barabarani (Street Lights) kuanzia TRA mpaka maeneo ya Mwenge katika barabara ya Singida – Gehandu (Manyara) (T014) na kuanzia Skyway hadi Kona ya Mohamedi, na Njuki hadi Mizani katika barabara ya Dodoma – Singida – Mwanza (T003)

Aidha Mhandisi alibainisha kwamba TANROADS wanaendelea kuimarisha  barabara kuu ya lami Dodoma – Singida – Mwanza (T003) kwa kufanya matengenezo mbalimbali na Ujenzi wa daraja eneo la Kyengege na kuimarisha barabara kuu ya Rungwa (Mbeya/Singida Mpakani) – Itigi – Mkiwa (T022); hasa sehemu ya Rungwa – Mwamagembe (km 65) kwa kuinua tuta la barabara na kuweka changarawe ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madaraja makubwa maeneo ya Itagata na Mwamagembe.

Mhandisi Msama wametoa wito kwa watumiaji wengine kuomba kibali endapo wanataka kutumia barabara kwaweka mageti barabarani na upitishaji wa mifugo  ambayo imekuwa chanzo cha uharibifu wa barabara.

Mbunge wa Iramba Magharibi Dk. Mwigulu Nchemba (Waziri wa Fedha) akizungumza wakati wa kikao hicho. 

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Alhaji Juma Kilimba, akizungumza kwenye kikao hicho.

Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, Mheshimiwa Ramadhan Ighondo akizungumza wakati wa kikao hicho.

Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskasi Muragili akizungumza wakati wa kikao hicho.

Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki, Dkt. Pius Chayaakizungumza wakati wa kikao hicho.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida Yagi Kiaratu akizungumza wakati wa kikao hicho.


Kikao kikiendelea

MWISHO

No comments:

Post a Comment