Saturday, June 04, 2022

Lamba lamba wapigwa marufuku Mkalama Mkoani Singida.

 

Kikundi cha watu wanaojiita waganga wa Kienyeji ambacho kimekuwa kikizunguka Kata mbalimbali za Wilaya ya Mkalama ikiwemo Kata ya Ilunda huku wakiwachangisha wananchi fedha kiasi cha Shilingi 15,000 kwa kila nyumba na kuwaaminisha kwamba wanatoa uchawi kimepigwa marufuku kuendelea na Biashara hiyo na yeyote atakayeshiriki atachukuliwa hatua za kisheria.

Marufuku hiyo imetolewa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge alipokuwa katika Mkutano wa hadhara katika Kata na Kijiji cha Ilunda Wilayani hapo baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu uwepo wa kikundi cha Lamba lamba ambacho kimekuwa kikiratibiwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wenyeviti wa  vitongoji.

Dkt. Mahenge pia amepiga marufuku kwa Jeshi la zamani NKR ambalo limetajwa kuhusika na uratibu wa kikundi hicho kwa kuwalazimisha wananchi kutoa fedha kama gharama ya kuwatafuta wachawi na kusimamia utoaji wa faini kwa wale waliohisiwa kuwa ni wachawi.

Akiongea katika Mkutano huo na wananchi Mkuu wa Mkoa akasema ni aibu kubwa wananchi kuacha kufanya kazi za maendeleo na kujihusisha na Ramli chonganishi ambazo zimelenga kuwaibia wananchi.

"Serikali imetoa fedha nyingi za Ujenzi wa Zahanati na vituo vya Afya ili kuwasaidia wananchi wake lakini inashangaza wananchi kuchangishwa fedha za kulanguliwa mnaibiwa mkiwa mnaona hili halikubaliki." Alisema Mahenge

RC Mahenge akabainisha kwamba hakuna ruhusa  kufanya Mkutano wowote na popote Mkoani hapa wenye malengo ya kuwaleta Lamba lamba  na endapo litatokea Rc ameagiza Polisi kumkamata  Mwenyekiti wa Kitongoji mkutano ulipofanyikia, Mtendaji wa Kata hiyo na Diwani wa eneo husika ili wakatoe maelezo.

Awali akitoa maelezo  Mkuu wa Wilaya Mkalama Sophia Kizigo amesema tayari wamewakamata baadhi ya wahusika na wamewafikisha kwenye vyombo vya Sheria ambapo walikiri kukusanya fedha katika Kata mbalimbali.

DC Kizigo amesema watu hao waliojinasibu kuwa ni waganga, walikusanya zaidi ya Milioni 100 kutoka kwa wananchi kwa kuwa nyumba zilizoguswa na mkasa huo zipo zaidi ya Mia moja.

Kizigo amesema kwamba Lamba lamba haikubaliki Mkalama hivyo akawataka viongozi wa Dini kushirikiana na Serikali kukomesha mambo hayo ya kishirikiana kwa kuwa ni chanzo cha umaskini.

DC amebainisha kwamba utapeli huo kwa wananchi unafanyika kipindi cha mavuno ambapo Inaaminika kwamba katika kipindi hicho wananchi wana fedha na mifugo hivyo kuwa rahisi kuchangia.

Hata hivyo Kizigo akawataka wananchi wa Mkalama kuacha kufichiana siri na kutoa taarifa kwa viongozi ili Serikali iweze kuchukua hatua za haraka na kuepusha madhara ambayo yangeweza kutokea.

"Hata hivyo kwa kuliongezea nguvu katazo hilo la Mkuu wa Mkoa sisi kama Serikali ya Wilaya tutaendelea kuwasaka wahusika mpaka tuwapate na tutafanya doria kuwabaini wote watakaofanya kwa Siri". Alisisitiza Kizigo.

Kamada wa Polisi Mkoa wa Singida ASP Stella Mutahibirwa akiwa katika Mkutano huo wa Mkuu wa Mkoa akawataka wanachi kuachana na ramli chonganishi ambazo zimesababisha mgawanyiko mkubwa wa kijamii kwa kuwahisi watu wengine kuwa ni wachawi kutokana na mueonekano wa macho yao.

Amesema kwa sasa Jeshi la Polisi limeshuka mpaka ngazi za Kata ambako kuna Maafisa wa Polisi hivyo wananchi wanaweza kuwatumia kwa kuwapa taarifa au kuzuia changamoto za kiusalama zinazoweza kutokea.

Amewataka wananchi kuacha tabia ya kuleta visababishi vya uvunjaji wa amani kufuata uwepo ya Lamba lamba katika Kata hiyo.

Aidha Afisa maendeleo ya Jamii Ngazi ya Mkoa  Shukuru Mbago akafafanua kwamba mtu yeyote anayejihusisha na  uchimbaji au uuzaji wa dawa za asili kwamba anatakiwa kuwa na kibali kinachotolewa na Halmashauri husika kwa kupitia hatua mbalimbali za Viongozi.

Shukrani akaendelea kusema kwamba hata kama Mganga anatoka eneo tofauti analazimika kutoa taarifa Serikali za mitaa ili kuendelea na matibabu tofauti na hivyo atakuwa anatenda kosa la kisheria.

Hata hivyo akawataka wananchi wanaojihusisha na tiba za kienyeji bila kuwa na kibali itambulike kuwa ni kosa kisheria na atalazimika kulipa faini ya fedha na kifungo kwa pamoja.

 Belinda Soyo ni mkazi wa Kata hiyo ambapo ameishukuru Serikali kwa kuchukua hatua hiyo kwa kuwa uwepo wa Lamba lamba umechangia kurudi nyuma kiuchumi kwa kuwa wengi walijihusisha na maandamano ya waganga badala ya kufanya kazi zao za kila siku.

Mwisho


No comments:

Post a Comment