Mkuu wa Mkoa wa SIngida Dk. Binilithy Mahenge akiongea na wanafunzi wa shule ya msingi Mandimu alipofanya ziara hivi karibuni katika shule hiyo.
Wazazi na walezi Mkoani Singida wametakiwa kuchukua tahadhari
katika kipindi hiki cha mvua dhidi ya uwepo wa madimbwi, mifereji kujaa maji
pamoja na vyoo vya mashimo kwa kuwa imeonekana kuwa hatari kwa watoto.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Binilithy Mahenge
leo Februari 15, 2022 alipofanya ziara katika shule ya msingi Mndimu iliyoko
wilayani Ikungi Mkoani hapa.
Amesema katika kipindi hiki cha mvua kila mzazi au mlezi
anapaswa kuangalia miundombinu yote ya barabara na majumbani mwao kama sehemu
ya kuchukua tahadhari na kuepuka maafa yanayoweza kutokea kutokana na uwepo wa
mvua nyingi.
Hata hivyo amebainisha kwamba katika kipindi hiki cha mvua
kuna uwezekano mkubwa wa majengo na miundombinu mbalimbali kupata nyufa ambazo
zinaweza kusababisha majanga hivyo ni jukumu la kila mmoja kuchukua tahadhari.
RC Mahenge akawaagiza Wahandisi mkoani hapo kutembelea na
kukagua maeneo yote na kufanya tathmini itakayoonesha uharibifu wa miundombinu
ya shule madaraja na barabara kama sehemu ya kuepusha majanga katika jamii
inayowazunguka.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji Halmashauri ya wilaya Ikungi
Justice Kijazi akatumia muda huo kumueleza Mkuu wa mkoa kwamba kutokana na
uwepo wa mvua nyingi ipo miundo mbinu ya baadhi ya shule ikiwemo shule ya
msingi Mandimu ambayo imeathiriwa na mvua zinazoenedelea kunyesha.
Kijazi akaendelea kufafanua kwamba tayari Serikiali imetoa
jumla ya Tsh. Milioni 40 na wakati huo Mbunge wa jimbo la Ikungi Mashariki akatoa
ahadi ya Tsh. milioni moja kwa ajili ya
ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule hiyo ambapo RC Mahenge naye
akaahidi kutoa kiasi cha Tsh. Milioni moja kwa ajili ya ujenzi huo.
Wakati huo huo RC. Mahenge ametoa pole kwa familia ya watu
sita (6) wa Kata ya Ihanja wilayani humo ambao wamelazwa katika kituo cha afya
cha Ihanja baada ya kula uyoga ambao umeonekana kuwa na sumu na kuathiri afya
zao.
Amesema familia hiyo inahusisha watoto wane (4) na wazazi
wawili (2) ambao hivi karibuni walikula uyoga huo kwa kuchanganya na mboga za
majani kama sehemu ya kitoweo pasipo kujua kama ungekuwa na sumu.
Aidha RC Mahenge amewataka wataalum wa afya na maafisa kilimo
kutoa elimu kuhusu aina za uyoga na matumizi yake ili kuondoa changamoto za
kiafya.
Kaimu Mkuu wa wilaya ya Ikungi Mhandisi Pasikas Muragili wakati akiwatambulisha viongozi mbalimbali wa mkoani hapo walipotembelea shule ya Mandimu hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment