Monday, February 14, 2022

Singida yaanza zoezi la uwekaji wa mifumo ya anuani za makazi

Mkoa wa Singida umedhamiria kukamilisha zoezi la uwekaji wa  mfumo wa anuani za makazi  ndani ya kipindi cha miezi miwili (2) ambapo kazi hiyo imeanza kwa kuwajengea uwezo wataalamu na viongozi mbalimbali,  utambuzi wa barabara na mitaa, kukusanya na kupitia taarifa  pamoja na uwekaji wa miundombinu katika Halmashauri zote mkoani hapo.

Kauli hiyo imetolewa leo Februari 14, 2022 na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa mkoa na kuhusisha Wakuu wa wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wenyeviti wa Halmashauri na wataalamu mbalimbali wa mipango miji ambapo aliwataka kuhakikisha zoezi linakamilika katika kipindi cha miezi miwili kuanzia tarehe ya leo.

Akizungumza namna ya ukamilishaji wa zoezi hili RC Mahenge akaelekeza kuundwa kwa kamati maalumu ya kusimamia utekelezaji wa uwekaji wa mfumo huo ambapo ametaka wananchi kushirikishwa kikamilifu hasa katika uwekaji wa vibao vitakavyotambulisha mitaa yao na majina ya mitaa husika.

Aidha amewaagiza wakurugenzi na wataalamu kushirikiana kikamilifu na Wakuu wa Wilaya na Wenyeviti wa Halmashauri katika utekelezaji wa zoezi hilo huku akitolea mfano wa ufanikishwaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa kupitia mradi wa fedha za uviko ambao ulikamilika vizuri kutokana na ushirikishwaji mzuri wa viongozi na wananchi.

Hata hivyo RC. Mahenge akawaagiza viongozi hao kuandaa orodha ya kazi zinazotakiwa kutekelezwa pamoja na kuwekwa ukomo wa muda ili kamati pamoja na viongozi wengine waweze kufuatilia huku akiwakumbusha kuwa na nakala ya muongozo uliotolewa na serikali juu ya utekelezaji wa uwekaji wa anuani hizo.

Akimalizia hutoba yake kwa viongozi hao RC. huyo akabainisha kwamba  kamati hiyo ambayo itaundwa na Katibu Tawala wa Mkoa itakuwa na jukumu la kuleta taarifa ya utekelezaji kwake kila baada ya wiki mbili.

Naye Katibu Tawala Mkoa Dorothy Mwaluko akawakumbusha wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha kwamba wanawashirikisha wakuu wa Idara zote katika kupata uelewa na katika kuanza utekelezaji.

Mwaluko amewataka wadau kuhakikisha wanapitia muongozo ambao ulikwishatolewa na serikali juu ya namna ya kuweka anuani mijini na vijijini huku akisisitiza utekelezwaji huo uwashirikishe viongozi mbalimbali wa serikali waliopo ngazi za kata Tarafa na Vijiji.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida Vijijini Elia Digha, akitolea ufafanuzi hoja iliyotolewa na DC Iramba Suleimani Mwenda iliyohusu changamoto ya kuhamahama kwa wakulima na wafugaji katika baadhi ya maeneo mkoani hapo hasa katika kipindi hiki cha uwekaji wa anuani za makazi amesema miongozo inaonenesha anuani zinatolewa kwenye nyumba na viwanja lakini pia ushirikishwaji wa Wenyeviti wa Vitongoji kutasaidia kuondoa changamoto hizo alisema Digha.

Kwa upande wake DC Mkalama Sophia Kizigo akasisitiza kwamba ana imani kubwa kwamba kazi hiyo ya uwekaji wa anuani za makazi itamalizika kwa wakati na hasa kwakuwa kutakuwa na mfumo unaofanana na ule wa utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ya uviko na utakuwa unaratibiwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Singida vijijini Ester Chaula amesema katika kuanza utekelezaji wa kazi hiyo Halmashauri yake imeteua washiriki 13 kwa ajili ya zoezi la  anuani za makazi kutoka Ilongero ambapo tayari wamejengewa uwezo  juu ya uelewa wa mfumo wa anuani za makzi na wajibu wao wakati wa utekelezaji.

Aidha Mkurugenzi wa Halmashauri amesema tayari wameshatambua jumla ya barabara na mitaa 41 ambazo nyingi ni zile zenye historia na matamshi yanayoweza kutamkwa ambayo hayana ukabila wa udini.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi  Justice Kijazi amesema tayari Halmashauri hiyo imeshapeleka wataalamu wawili (2) kupata mafunzo kwa ajili ya utekelezaji wa kazi hiyo mafunzo yaliofanika mkoani Tanga.

Hata hivyo amemaliza katika wasilisho lake kwamba Halmashauri hiyo inaendelea na ugawaji wa fomu maaalum za utoaji wa majina ya barabara kwa kuzingatia sifa zilizowekwa kwenye  mwongozo wa mfumo wa anuani za makazi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi  Justice Kijazi akizungumza wakati wa kikao

No comments:

Post a Comment