Jumla ya watu waliopata chanjo kwa mkoa wa Singida ni 26,739 kati ya 1,754,37 ambapo wamekwisha maliza dozi ya Janssen sawa na asilimia 1.5
Akiongea wakati akifungua mkutano wa viongozi wa Kanisa katoliki Jimbo la Singida uliohusu uhamasishaji wa chanjo ya corona kwa watanzania mganga mkuu wa mkoa wa Singida Victorina Ludovick, amesema kumekuwepo na jitihada mbalimbali za kuwafikia wananchi wa makundi yote ili kupata chanjo, ambapo mbinu mbalimbali zimetumika kuifikia jamii.
Aidha amesema uzoefu walioupata katika hatua za awali unaonesha kuwa elimu kwa umma imechangia mafanikio makubwa katika zoezi hili na kwamba bado ipo haja ya kuwashirikisha waumini wengi ili watambue umuhimu wa kupata chanjo.
Hata hivyo Dkt. Ludovick amefafanua kwamba Wizara ya Afya imepitisha mbinu na mikakati mbalimbali kuhamasisha mkakati harakishi na shirikishi wa kushirikisha taasisi mbalimbali, makundi ya kijamii na viongozi wa dini.
“Kupitia mkutano huu nina imani kubwa kwamba mtaendelea kuwa sehemu inayohubiri kuhusu afya bora kwa wananchi wetu ili kuepusha vifo zaidi vinavyotokana na corona” alisema Victorina Ludovick
“Natambua pia kuwa mbinu zingine za kukabiliana na ugonjwa huu zikiwemo kuvaa barakoa, kutumia vitakasa mikono, kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka pamoja kuzingatia afya ya ulaji vyakula vyenye kujenga kinga za mwili mmekuwa mkizihamasisha kila mkutanapo kwa waumini wenu”. Aliendelea kufafanua Mganga Mkuu
Hata hivyo Mganga Mkuu amebainisha kuwa kwa sasa chanjo mpya imeingia mkoani hapa aina ya Sinopharm ambayo hutolewa dozi mbili (2) ambapo amewataka wananchi wote waliopata dozi moja ya aina hiyo kuhakikisha wanamalizia dozi ya pili kulingana na maelekezo waliyopewa.
Dkt. Ludovick ameendelea kusema kwamba Chanjo hizo zinatolewa kwa mgawo duniani na wananchi wanazipata bure kupitia vituo maalum vya chanjo, ambapo zimeshapelekwa katika vituo vyote vya huduma za afya nchini. Aidha ameeleza kwamba huduma hii inapatikana katika maeneo mbalimbali kwa njia ya huduma mkoba (outreach), maeneo hayo ni pamoja na vituo vya usafirishaji, masokoni, vivukoni, mipakani na maeneo mengine mengi yenye mwingiliano mkubwa wa watu kwa wakati mmoja.
Bado idadi ya watu wanaohitaji chanjo ni kubwa kote duniani hivyo ni muhimu Tanzania nasi kuhakikisha mgawo wetu tunautumia vizuri na kwa kuzingatia muda wa chanjo hizi kutumika. Alieleza Mganga Mkuu.
Akimalizia hotuba yake amesema kwamba
Chanjo hizo ni salama, zimeonesha mafanikio makubwa na ni njia ya haraka
ya kupunguza makali ya ugonjwa wa Corona hivyo kutozipatia umuhimu ni sawa na
kujiumiza wenyewe na ni jukumu letu kuwafungua macho wengine ambao bado wana
wasiwasi ili wachanje na hivyo kujilinda wao wenyewe na kuwalinda wengine
wanaowazunguka. Alimazia Dkt. Victorina Ludovick
Kikao
hicho kilihudhurwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Singida, Muwakilishi wa baraza
la Maaskofu Tanzania (TEC), mwezeshaji kutoka Chuo Kishiriki cha Sayansi ya
Tiba Muhimbili, Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais – TAMISEMI,
AMREF Health, Wadau wa sekta ya Afya na Masista.
No comments:
Post a Comment