Friday, September 10, 2021

Bomba la mafuta kutoa fursa kibao Singida - Dkt. Mahenge

 

Wito umetolewa kwa wananchi mkoani Singida  kutumia fursa zitakazopatikana wakati wa Mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) utakao anza hivi karibuni mkoani hapo  ili waweze kujiongezea kipato na kuondoa umaskini.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge ametoa wito huo hivi karibuni  wakati akifungua mkutano uliofanyika katika ukumbi wa mikutano  ofisi za Mkaguzi wa Hesabu  na kuhusisha Wakuu wa Idara mbalimbali pamoja na wafanyabiashara wa Mkoa wa Singida na kuwataka kuzitumia fursa mbalimbali ambazo zitapatikana wakati wa ujenzi wa bomba hilo.

Amesema  ujenzi wa bomba hilo utakuwa na jumla ya  vituo 14 katika Wilaya na Mikoa mbalimbali ambapo kituo cha  11 kitakuwa mkoani Singida katika kijiji cha Ntondo kilichopo Manispaa ya Singida Mjini.

Dkt. Mahenge amesema kituo hicho kitakuwa na watumishi kuanzia 1,000 hadi 2,000 ambao watahitaji kula, kulala na kunywa  hivyo  wananchi wa Singida wanatakiwa kutumia fursa hiyo kwa kuanza kuwekeza  kwa kujenga vyumba za kupangisha, nyumba za kulala wageni pamoja na ufugaji wa kuku ili wapate kipato na watoe ajira kwa wengine.

Aidha Serikali tayari imeandaa mazingira wezeshi yanayovutia uwekezaji kwa kutengeneza barabara  na kuweka umeme ili wananchi waweze kuendelea na mapambano ya kuondoa umasikini alifafanua Mkuu wa Mkoa.

Akimalizia hotuba yake Mhe. RC ameeleza kwamba Serikali mkoani hapo imeendelea kuongea na mabenki mbalimbali wapunguze riba katika mikopo yao ili iweze kuwavutia wateja .

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Bi Dorothy Mwaluko moja ya wadau katika mkutano huo wakati akimkaribisha Mkuu wa Mkoa amesema bomba hilo litakuwa na urefu wa kilometa 140  kwa Singida ambapo litapita katika wilaya tatu  za Iramba, Mkalama na Singida Vijijini.

Katibu Tawa huyo amebainisha kwamba jumla ya vijiji 31 na kata 17 vitapitiwa na mradi huo  hivyo kuwataka wananchi wa maeneo husika kuhakikisha wanatumia fursa kwa ajili ya maendeleo ya Mkoa wa Singida na taifa kwa ujumla .

Kwa upande wake Bw. Safiel Msovu kutoka Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC) katika wasilisho lake mbele ya mgeni rasmi amebainisha kwamba bomba hilo litakuwa na urefu wa kilometa 1,448 ambapo litakuwa na uwezo wa kusafirisha mapipa 216 kwa siku.

Aidha Bw. Msovu amefafanua kwamba mradi huo ni mkubwa na unagharimu kiasi cha dola bilioni 3.5 sawa na shilingi triloni nane (8) na unatarajiwa kuanza hivi karibuni kwa kuwa mikataba muhimu  imekamilika.

Wanahisa katika mradi huo ni kampuni ya ufaransa inayojulikana kwa jina la Total, Uganda kupitia shirika la mafuta la  UNOC, kampuni ya kichina ya CNOOC na Shirika la Uendelezaji wa Petrol nchini (TPDC)” alisema Bwana Msovu.

Kwa mujibu wa  muundo wa sasa wa mgawanyo wa hisa, kampuni ya Ufaransa Total itamiliki asilimia 62, kampuni ya China CNOOC asilimia 8, UNOC ya Uganda  itamiliki asilimia 15 na asilimia 15 iliyobaki itamilikuwa na  Tanzania kupitia kwa kampuni yake ya maendeleo ya mafuta TPDC.

 Hata hivyo alimalizia kwamba  mradi huo unategemewa kujengwa kwa kipindi cha miaka mine (4) na unategemewa kutoa huduma kwa miaka isiyopungua 25, alimalizia bwana   Safiel Msovu

Wafanyabiashara mkonia Singida kwa umoja wao wamesema kwamba wamejipanga kutumia fursa hiyo ila wameomba Serikali kuendelea kutengeneza mazingira wezeshi ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za mara kwa mara  kuhusiana na maendeleao ya mradi huo.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment