Monday, September 30, 2019

WAZIRI MKUU KUANZA ZIARA YA KIKAZI YA SIKU NNE MKOANI SINGIDA

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani).

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Singida ambapo atatembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na uwekaji wa Mawe ya Msingi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa Septemba 30, 2019 Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amesema ziara hiyo ataianza Oktoba 4, 2019 hadi Octoba 6, 2019 na Oktoba 7, 2019 atafungua rasmi maonesho ya Pili ya SIDO Kitaifa mkoani Singida.


Amesema katika ziara hiyo pia, Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa (MB) atazungumza na Wananchi pamoja na Watumishi katika mikutano ya hadhara katika kila Wilaya na halmashauri zote za mkoa wa Singida.

” Maonesho haya yatafanyika sanjari na maadhimisho ya wiki ya chakula Duniani ambayo Kitaifa yatafanyika mkoani Singida kuanzia Oktoba 10 hadi 16 mwaka huu katika Viwanja vya Bombadier”. Dkt. Nchimbi.

Amesema kufanyika maonesho hayo mkoani Singida ni fursa kwa wananchi wa mkoa wa Singida ambao unakuwa kiuchumi kwa kasi kutokana na shughuli za kilimo, ufugaji, biashara na viwanda.

Pia amesema Serikali ya mkoa wa Singida unajivunia kwa kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa maonesho hayo Kitaifa na hii itawapa hamasa kubwa wananchi katika kuanzisha viwanda vidogo vya usindikaji kutokana na mazao yanayolimwa mkoani hapa.

Dkt. Nchimbi ametumia nafasi hiyo kuwakaribisha wananchi wote wa mkoa wa Singida na Tanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kupokea ugeni huo na kushiriki katika maonesho hayo.


Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akizungumza na waandishi wa habari.

Katika ziara hiyo Mheshimiwa Kassim Majaliwa atatembelea miradi mbalimbali ya kimkoa na miradi mikubwa ya kitaifa, ambapo miradi ya kitaifa ni mradi wa kupokea na kupozea umeme uliopo katika halmashauri ya Manispaa ya Singida pamoja na mradi wa daraja Sibiti linalounganisha mkoa wa Singida na Simiyu lililopo wilaya ya Mkalama mkoani Singida.


HABARI NA MAWASILIANO
OFISI YA MKUU WA MKOA
SINGIDA
Habari zaidi tembelea tovuti  http://www.singida.go.tz/

No comments:

Post a Comment