Sunday, September 15, 2019

WALIMU MKOANI SINGIDA WAPONGEZWA KWA KUSHIKA NAFASI YA PILI KITAIFA KATIKA MATOKEO YA KIDATO CHA SITA MWAKA HUU 2019.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akikabidhi zawadi kwa Mkuu wa shule ya Sekondari ya Mwanamwema Shein Mwalimu Zainabu Mtinda kwa kushika nafasi ya kwanza kimkoa katika matokea ya kidato cha Sita mwaka huu.

SERIKALI ya Mkoa wa Singida imewapongeza walimu na wanafunzi kutoka shule mbalimbali zilizopo mkoani Singida kwa kufanya vizuri katika matokeo ya kidato cha sita mwaka huu 2019 hadi kupelekea kushika nafasi ya pili kitaifa kati ya shule 29 zilizopo Tanzania bara na Visiwani. 

“HONGERA SANA KWA MAFANIKIO MAKUBWA HAYA AMBAYO MUNGU AMETUWEZESHA”. Dkt. Rehema Nchimbi

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amesema, uwalimu ni wito, ni lazima uwe na uhusihano wa moja kwa moja na Mungu, kazi ya ualimu ni kazi Takatifu na sio kila mtu anaweza kuwa mwalimu.

Amesema, Mwalimu lazima awe mwenye huruma, mwalimu wakati wote lazima awe mlinzi katika nafasi pana. Mwalimu ni kiunganishi, anaunganisha ubao na darasa, anaunganisha yaliyopo kichwani kwake na wanafunzi.

 “Ualimu ni usuruhishi, mwalimu ni mpatanishi, ukimuona mtoto hajapatanishwa vizuri na mazingira yanayomzunguka ujue kuna changamoto ya uwalimu” Dkt. Nchimbi

Amesisitiza kuwa, Saikoloji inasema hakuna binadamu asiyefundishika, hivyo, kufeli kwa mwanafunzi ni kufeli kwa mwalimu, “Mwalimu hata siku moja hafurahishwi na matokeo mabaya ya mwanafunzi wake bali hufurahishwa na matokeo mazuri (chanya) ya mwanafunzi wake”.

Aidha, ametoa wito kwa Wakurugenzi na Maafisa Elimu wa ngazi mbalimbali mkoani Singida kuwa karibu na walimu kwa kutenga muda wa kuwasikiliza  pindi wafikapo maofisini kwao. 

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi, amesema Walimu ndio wanaoweza kututengenezea Taifa au kutuharibia, kwa sababu ndiyo wanaoshiriki katika malezi ya mtoto katika nyakati zote za makuzi yake. 

Aidha, Dkt Angelina Lutambi, ametoa wito kwa walimu kujitokeza kwa wingi katika kushiriki mashindano mbalimbali ya kitaaluma pindi yanapoandaliwa ili kuongeza tija katika sekta ya elimu mkoani Singida na Taifa kwa ujumla.


Naye, Afisa Elimu wa Mkoa wa Singida Mwl. Nelasi Mulungu amesema, mikakati iliyotumika na kuendelea kufanya vizuri katika mitihani ya kidato cha sita kila mwaka ni kufanya vikao vya pamoja na wakuu wa shule ambapo kila mkuu wa shule hueleza na kuwasilisha mikakati waliyojipanga kwa kila shule ambayo inahakikisha kuwa ufaulu unakuwa ni daraja la kwanza na la pili.

Aidha, Kufanya Majaribio kwa kila wiki, na baadhi ya shule wana wastani wa shule ambapo asiyeufikia wastani huo hupewa adhabu zenye kuwasukuma kuhakikisha kuwa kila mmoja anafanya vizuri mfano, kupewa mazoezi ya kutosha ili kuwafanya muda mwingi wawe wanajisomea.

Akisisitiza zaidi amesema, Wamefanikiwa kudhibiti utoro kwa kuhakikisha kuwa wakati wote wanafunzi wapo shuleni  na darasani wanajifunza. Kuhakikisha kila mwalimu anakamilisha mada zote kwa wakati.


"Mkakati mwingine ni Kudumisha nidhamu kwa walimu na wanafunzi ili ufundishaji na ujifunzaji uweze kwenda vizuri na kwa kujituma". Mwl. Mulungu

MATUKIO KATIKA PICHA
Afisa Elimu wa Mkoa wa Singida Mwl. Nelasi Mulungu akizungumza

Kikao kikiendelea


 Afisa Elimu wa halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Mwl. Ngwano Ngwano akizungumza

Mkuu wa shule ya Sekondari ya Mwenge Mwl. Samweli Kasnshema akizungumza

Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi (kulia) akimpongeza Mkuu wa shule ya Sekondari Mwanamwema Shein Mwl. Zainabu Mtinda, kwa kufanya vizuri katika matokeo ya kidato cha sita mwaka huu 2019.

Imetolewa na;
Kitengo cha Habari na Mawasiliano
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
SINGIDA

Habari zaidi tembelea tovuti  http://www.singida.go.tz/

No comments:

Post a Comment