Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi wakiwa na Viongozi wa Mkoa na Wilaya pamoja na Baraza la Madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Manyoni wakati walipotembelea mradi wa kilimo cha Korosho (Masigati) 12 June, 2019.
MKUU wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amezipongeza Halmashauri zote za mkoa wa Singida kwa kupata hati safi, kutoka kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Dkt. Nchimbi, ametoa pongezi hizo wakati
akizungumza katika kikao Maalum cha Baraza la Madiwani cha hoja za ukaguzi
kilichofanyika katika ukumbi wa zamani wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba mkoani
Singida.
Amesema, Watumishi na Watendaji
ni waajiriwa wa Serikali iliyoko madarakani, ni lazima wawe
waaminifu na waadilifu kwani ndiyo inayowalipa mshahara.
‘’Ukiona mahali kuna hoja za
ukaguzi, ujue kiwanda cha kuzalisha hoja ni watumishi na watendaji,
sisi watumishi na watendaji tukikaa vizuri hakutakuwa na hoja, ninyi
ambao hamkuwepo wakati hoja za ukaguzi zilipokuwa zinazalishwa na watendaji
waliopita onyesheni mfano basi msiwe na dhana ya kukariri, kunakilishwa halafu
ninyi wenyewe hamuonyeshi mabadiliko, hivyo inawapasa kuonyesha kwamba sisi
hatuna hoja ndipo hapo tutakapokutana na kujipongeza kwamba tumepata hati
safi’’ Dkt. Nchimbi
Amesema, ni lazima watumishi na
watendaji wazingatie hasa kwa utumishi wa awamu ya tano, awamu ambayo si ya
maslahi binafsi bali ni ya kutekeleza agenda za kitaifa.
‘’Sisi sote ni
wasaidizi wa Mheshimiwa. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais ambaye hafanyi kazi kwa maslahi
yake, hivyo inawapasa kuwa makini sana katika utendaji wenu”. Amesisitiza
Dkt. Nchimbi
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa wa Singida
amezipongeza kwa dhati Halmashauri zote za Mkoa wa Singida kwa kupata hati na
kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii katika kuwatumikia Wananchi na Taifa
kwa ujumla.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa
Mkoa wa Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi, amesema kuwa kuna hoja
zingine hazikuwa za lazima bali ni uzembe wa watendaji ambao
hawakuwa makini katika kutekeleza majukumu yao.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya wilaya ya Iramba Bw. Linno Mwageni, aliwasilisha hoja za ukaguzi
64 na kutoa taarifa ya Halmashauri hiyo kupata hati safi kwa mwaka wa
fedha 2017/2018.
MATUKIO KATIKA PICHA
WAKATI WA ZIARA YA MKUU WA MKOA WA SINGIDA KUTEMBELEA MASHAMBA YA KILIMO CHA KOROSHO, WILAYANI MANYONI.
IMETOLEWA NA,
KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO,
OFISI YA MKUU WA MKOA
SINGIDA
No comments:
Post a Comment