Thursday, May 02, 2019

SERIKALI YA MKOA WA SINGIDA YATAMBULISHA RASMI SOKO LA MADINI

Serikali mkoani Singida imetekeleza kwa kishindo agizo la Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, la mikoa yenye madini kuanzisha soko ndani ya siku 7 alizotoa, kwa kushuhudia uuzaji na ununuzi rasmi wa dhahabu ndani ya soko hilo la dhahabu katika mkoa wa Singida.

Akizungumza jana 01 Mei, 2019 akiwa katika soko hilo la madini mkoani Singida mara baada ya kukagua shughuli zitakazofanyika ndani ya soko hilo, Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amesema, soko hilo litabadili uchumi wa mkoa wa Singida.
“Soko hili litabadili kabisa sio uchumi tuu wa dhahabu lakini pia uchumi wa Singida, na hii itadhihilisha usemi unaosemwa kuwa Singida ni njema tena ni njema sana” Dkt. Nchimbi.
Amesema, Serikali ya mkoa wa Singida ipo tayari, inauwezo na imejiandaa kikamilifu kushiriki na kutimiza haki na wajibu wake wa kuhakikisha soko hilo linakuwa endelevu na lenye heshima kubwa nchini.
Akisisitiza zaida amesema, wadau wote wanaotakiwa kuwepo kwenye mnyororo wa biashara ya madini ya dhahabu ndani ya soko hilo wapo tayari, wakiwemo wauzaji, wanunuzi, taasisi za kifedha (benki), Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, pamoja na vyombo vyote vinavyohusika.
“Kwahiyo hapa ndipo penyewe na pamekamilika, muuzaji au mnunuzi ataingia hapa atatoka hana fedha lakini fedha zake zitakuwa kwenye mfumo wa kibenki” Dkt. Nchimbi.
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa wa Singida amewashukuru wachimbaji pamoja na wauzaji wa dhahabu mkoa wa Singida kwa ushirikiano walioutoa kwa Serikali ya mkoa katika kufanikisha kukamilika kwa soko hilo la madini mkoa wa Singida.
“SOKO LA DHAHABU KIMKOA NI HILI HAPA”
“Na wote wanaohusika na dhahabu wapo tayari kuuza dhahabu hapa, na wakati wote tuwe pamoja kuwawezesha ndugu zetu hawa ili waweze kulitumia soko hili vizuri zaidi” Dkt. Nchimbi.
Dkt. Nchimbi ametoa wito kwa wakurugenzi, watendaji pamoja na watumishi wote mkoani Singida kwa kulitangaza soko hilo kwa wahusika wote ili wajue kuwa soko la dhahabau lipo ndani ya mkoa wa Singida.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima, ametoa rai kwa wachimbaji wadogo mkoani Singida kutumia fursa hiyo ya upatikanaji wa soko la madini ndani ya mkoa ili kuinua uchumi wao, na kuwa chachu ya maendeleo yao binafsi, mkoa na taifa kwa ujumla.
“Leo tunaona juhudi za mheshimiwa mkuu wetu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi za kuhakikisha kwamba tunapata hili soko la madini”
“Nitoe rai kwa wachimbaji wadogo kwamba hii ni fursa na fursa hii lazima tuitumie vizuri, fursa hii ndio itakayotutoa hapa tulipo kwenda sehemu nyingine zaidi kiuchumi. Na huko tunako elekea tunahitaji kuelekea mahali ambapo mkoa huu wa Singida ndio utakaokuwa chachu ya maendeleo ya Tanzania” Mhe. Sima
Nao, Wachimba wa madini mkoa wa Singida wameishukuru Serikali kwa ujio wa soko hilo la madini mkoani Singida kwani kupitia soko hilo litapelekea ulipaji sahihi wa kodi za Serikali chini ya usimamizi makini wa Serikali ya Awamu ya Tano tofauti na hapo awali. 
Aidha, wamempongeza Mheshimiwa mkuu wa mkoa wa Singida kwa kuliweka soko hilo mahali salama na panapostahili.
“Ujio wa soko hili kwetu sisi wachimbaji imekuwa ni muhimu sana kwa sababu tumepata sehemu ya uhakika na mizani iliyohakikiwa” Amesema, Mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara wa madini mkoa wa Singida.
Naye, Makamu mwenyekiti wa chama cha wachimbaji wadogo mkoa wa Singida amesema, walikuwa na hamu kubwa sana ya kuwa na soko la madini ndani ya mkoa ili kuondokana na adha waliyokuwa wanaipata hapo awali ya kutokuwa na mahali salama pa kufanyia biashara hiyo ya madini.
“Kitendo kilichofanyika leo cha kushuhudia rasmi uuzaji na ununuzi wa dhahabu ndani ya soko jipya mkoani Singida, kinatupa sisi wachimbaji wadogo mwanga wa kuanza kuleta dhahabu ili kuuziwa hapa ili kukuza uchumi wa mkoa na taifa letu”.
“Tunaahidi dhahabu zote zinazopatikana ndani ya mkoa wetu wa Singida zitauzwa hapa, na wachimbaji wetu wapo tayari kuuza hapa, hivyo hakutakuwa na utoroshwaji wa dhahabu tena.” Amesema, Makamu mwenyekiti wa chama cha wachimbaji wadogo mkoa wa Singida.
Wamesema, awali palikuwa na utaratibu mbaya katika biashara ya dhahabu. Kuitoa mkoani Singida kupeleka mikoa mingine iliyokuwa ikisababisha baadhi ya wafanyabiashara hao wa madini kutumia njia zilizokuwa kinyume cha sheria na taratibu, lakini sasa wachimbaji wamefurahi sana kwa kuwa na soko la madini ndani ya mkoa wa Singida. 
MATUKIO KATIKA PICHA

 Kaimu Afisa Madini mkoa wa Singida Bw. Chone Lugangizya Malembo (kushoto) akitoa maelezo mafupi kwa baadhi ya viongozi wa Serikali ya mkoa wa Singida waliojitokeza kushuhudia uuzwaji na ununuzi wa dhahabu rasmi ndani ya soko la madini mkoani Singida.





PICHA YA PAMOJA
Imetolewa na;
Kitengo cha Habari na Mawasiliano 
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
SINGIDA

No comments:

Post a Comment