Saturday, October 06, 2018

MKUU WA MKOA SINGIDA AMEZITAKA HALMASHAURI ZOTE MKOANI SINGIDA KUTUMIA CHAKI ZINAZOZALISHWA NDANI YA MKOA WA SINGIDA


Mkuu wa Mkoa Singida Dkt. Rehema Nchimbi ametoa rai kwa Halmashauri zote za mkoa wa Singida kutumia Chaki (Chalk) zinazotengenezwa mkoani Singida kwa sababu mkoa unaviwanda ambavyo vinazalisha chaki nzuri na bora ambazo zinatosheleza mahitaji ya shule zote mkoani hapa ili kuendeleza viwanda  na kukuza uchumi wa halmashauri na mkoa kwa ujumla.

Rai hiyo imetolewa jana alipokuwa kwenye hafla ya kukabidhi nyaraka za mikopo kwa vikundi vya vijana, wanawake na walemavu wilayani Ikungi, sambamba na kukagua na kujionea shughuli  mbalimbali zinazofanywa na wanavikundi hao wa halmashauri ya Ikungi mkoani Singida.

“Chaki zinazozalishwa ndani ya Ikungi na ndani ya mkoa wa Singida lazima zipate soko la kwanza ndani ya Ikungi na ndani ya mkoa wa Singida, tuna shule nyingi za kuweza kutumia chaki zote zinazozalishwa kutoka kwenye viwanda vilivyopo ndani ya mkoa vikiwemo viwanda vyetu vya vijana wa halmashauri ya Ikungi mkoa wa Singida”.

“Mkoa wa Singida tunaviwanda vya chaki vya kututosheleza na tunaziada ya kuuza nje ya mkoa wa Singida”. Alisema Dkt. Nchimbi.

Aidha, Dkt. Nchimbi amewataka Wakuu wa wilaya mkoani hapa kusimamia masoko ya bidhaa mbalimbali yanayozalishwa na vijana, wakinamama na wenye uhitaji maalum (walemavu) na wananchi wote wa Singida ili kuinua uchumi wa viwanda kwa wananchi wa mkoa wa Singida.

Pia, ameipongeza Halmashauri ya Ikungi kwa kuweza kukusanya vizuri mapato ya ndani na kufikia uwezo wa kuwakopesha mikopo iliyotokana na asilimia kumi ya mapato ya ndani vikundi mbalimbali ndani ya halmashauri hiyo ya Ikungi na amewasisitiza wale wote wanaohusika katika ukusanyaji wa mapato kuwa wakali katika ukusanyaji huo wa mapato ya ndani ya halmashauri.

“Nawashukuru sana halmashauri kwakuweza kujipanga vizuri kwa kuweza kukusanya mapato ya ndani hadi kufikia kutoa mikopo kwa vikundi. Kusanyeni tena na tena, Muwe wakali sana kwa wale mliowaweka katika ukusanyaji wa mapato ya ndani na lazima vifaa vya kielektroniki vitumike katika ukusanyaji wa mapato” alisema Dkt. Nchimbi.
  
Kwaupande wao wanavikundi wa halmashauri ya Ikungi waliopatiwa mikopo hiyo isiyo na riba wameishukuru Serikali ya halmashauri hiyo ambapo wamesema kupitia mikopo hiyo itawasaidia kuinua uchumi wa wananchi wa Ikungi pamoja na kuibua viwanda vidogo vidogo ndani ya halmashauri ya Ikungi mkoani Singida.

Naye, Mwenyekiti wa kikundi cha Mshikamano walemavu halmashauri ya Ikungi Bw. Donald Adam Bilali, ameishukuru Serikali ya awamu ya Tano kwa kuwajali, kuwathamini na kuwaweka pamoja na kusema kupitia mikopo hiyo familia zao kwasasa zimeongeza furaha kutokana na wakinamama kuendesha miradi yao  midogomidogo inayopelekea jamii kuwapokea kwa shangwe.

“Mheshimiwa mkuu wa Mkoa naomba ufikishe salamu zetu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Joseph Magufuli, pamoja na kwamba sisi watu wenye ulemavu tumepungukiwa maumbile  lakini tunashusha pumzi ya faraja tunapoona Serikali ya awamu ya Tano inapotuthamini na kuona utu wetu”. Alisema Donald A. Bilali.

Aidha, ametoa wito kwa wanavikundi wote waliopatiwa mikopo hiyo kuendesha vikundi hivyo kwa tija kwa kuzingatia mambo makuu matatu; TARATIBU, MIONGOZO na SHERIA ili kuweza kukopesheka tena.

Kwaupande wake, Mkuu wa wilaya ya Ikungi Mhe. Miraji Jumanne Mtaturu amemwakikishia mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi, kuwa wataendelea kukusanya mapato ya ndani ya kutosha ili  kufika malengo yaliyowekwa ndani ya halmashauri hiyo pamoja na kusimamia viwanda vidogovidogo vyote vinavyozalisha bidhaa katika halmashauri ya Ikungi ili kutumika ndani ya halmashauri hiyo pamoja na mkoa kwa ujumla ili kulinda soko la wananchi wa Ikungi na mkoa wa Singida.

Halmashauri ya wilaya ya Ikungi imetoa mikopo ya shilingi 44,200,000 kwa vikundi 23, ikiwa vikundi vya wanawake ni 17 vimekopeshwa shilingi 31,700,000, vijana vikundi 4 vimekopeshwa shilingi 8,500,000 na walemavu vikundi 2 vimekopeshwa shilingi 4,000,000.

MATUKIO KATIKA PICHA





 Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akikagua bidhaa na shughuli mbalimbali zinazofanywa na baadhi ya vikundi katika halmashauri ya Ikungi wakati wa hafla ya kukabidhi nyaraka ya mikopo isiyo na riba kwa wanavikundi vijana, wakinamama na walemavu wilayani Ikungi mkoa wa Singida.

 Sehemu ya wanavikundi katika halmashauri ya Ikungi wakati wa hafla ya kukabidhi nyaraka ya mikopo isiyo na riba kwa wanavikundi vijana, wakinamama na walemavu wilayani Ikungi mkoa wa Singida.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ikungi Mhe. Ally Mwanga akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi nyaraka ya mikopo isiyo na riba kwa wanavikundi vijana, wakinamama na walemavu wilayani Ikungi mkoa wa Singida.

 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ikungi Bw. Justice Laurence akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi nyaraka ya mikopo isiyo na riba kwa wanavikundi vijana, wakinamama na walemavu wilayani Ikungi mkoa wa Singida.

 Mwenyekiti wa kikundi cha Mshikamano walemavu halmashauri ya Ikungi Bw. Donald Adam Bilali akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi nyaraka ya mikopo isiyo na riba kwa wanavikundi vijana, wakinamama na walemavu wilayani Ikungi mkoa wa Singida.

 Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi (katikati), Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ikungi Mhe. Ally Mwanga (kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ikungi Bw. Justice Laurence wakifurahia jambo mara baada ya Mwenyekiti wa kikundi cha Mshikamano walemavu halmashauri ya Ikungi Bw. Donald Adam Bilali alipomaliza kuzungumza wakati wa hafla ya kukabidhi nyaraka ya mikopo isiyo na riba kwa wanavikundi vijana, wakinamama na walemavu wilayani Ikungi mkoa wa Singida.


Mkuu wa wilaya ya Ikungu Mhe. Miraji Jumanne Mtaturu akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi nyaraka ya mikopo isiyo na riba kwa wanavikundi vijana, wakinamama na walemavu wilayani Ikungi mkoa wa Singida.

  Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi ambaye ndiye mgeni rasmi akihutubia wakati wa hafla ya kukabidhi nyaraka ya mikopo isiyo na riba kwa wanavikundi vijana, wakinamama na walemavu wilayani Ikungi mkoa wa Singida.








 Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi ambaye ndiye mgeni rasmi akikabidhi hati za nyaraka ya mikopo isiyo na riba kwa wanavikundi mbalimbali vijana, wakinamama na walemavu wilayani Ikungi mkoa wa Singida.




 Mkuu wa wilaya ya Ikungi Mhe. Miraji Jumanne Mtaturu akimpongeza kijana Godfrey Raphael Mange, mmoja wa vijana aliopatiwa mkopo usio na riba uliomuwezesha kununua pikipiki kwaajili ya kufanyia biashara ya bodaboda ili kuongeza kipato.

  Chaki zinazozalishwa na kiwanda kilichopo katika halmashauri ya Ikungi mkoani Singida.


IMETOLEWA NA;
KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO
OFISI YA MKUU WA MKOA
SINGIDA

No comments:

Post a Comment