Mkandarasi anayejenga
bwawa la Rungwa katika Halmashauri ya Itigi amepewa siku saba na Serikali
Mkoani Singida kuhakikisha anapeleka vifaa muhimu vitakavyoongeza kasi na
ufanisi wa ujenzi wa bwawa hilo.
Katibu Tawala Msaidizi
Sehemu ya Serikali za Mitaa Mwajabu Nyamkomola ametoa agizo hilo mapema jana
mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa bwawa hilo na kukuta ukiwa katika
asilimia 35 wakati ulitakiwa kuwa asilimia 60 huku baadhi ya vifaa muhimu
vikikosekana.
Nyamkomola amemueleza
Mhandisi mwakilishi wa kampuni ya Proactive Independent Group Ltd Elias Gamba
kuwa wananchi wa Rungwa hawana maji na juhudi za serikali kuwapatia maji
kupitia mradi huo wenye thamani ya zaidi ya milioni mia saba unatakiwa
kufanyika kwa kasi na ufanisi wa hali ya juu.
Ameeleza kuwa baada
ya kufanya ukaguzi katika bwawa hilo wamebaini kuwa baadhi ya kazi zimekuwa
zikifanywa kwa kasi ndogo kutokana na kutokuwepo kwa mashine na badala yake
kazi hizo kufanywa na vibarua huku vifaa vingine vikiwa pungufu tofauti na
makubaliano katika mkataba.
“Kuna kazi ya kutengeneza
zege kwa ajili ya kujenga ukuta katika bwawa hili, ile zege tumeona inachanganywa
na vibarua badala ya mashine tuliyokubaliana, mkandarasi unapunguza ubora na
kasi inakuwa ndogo, unatuchelewesha kuwapa wananchi maji, hata huu mchanga unaotumika
haufai uache kutumika mara moja”, amesisitiza Nyamkomola na kuongeza kuwa,
“Sasa hivi mlitakuwa
kuwa mmeshachimba mtaro wa bomba la kusafirisha maji kwenye matenki kwahiyo ndani
ya siku saba hakikisheni kijiko cha kuchimba mtaro huo, mabomba na vifaa vyote
vitakavyotumika katika kujengea viwe vimewasili hapa Rungwa”, amefafanua.
Naye Mhandisi wa Maji
Mkoa wa Singida Lydia Joseph amesema ujenzi wa bwawa hilo unatakiwa kukamilika kabla
ya mwezi Februari mwakani ili serikali na Mkandarasi wapate muda wa matazamio
na kurekebisha dosari endapo zitajitokeza pamoja na kuwahi msimu wa mvua ili
kuvuna maji hayo.
Mhandisi Lydia
amemueleza mhandisi mwakilishi wa Mkandarasi kuwa anatakiwa kuzingatia
makubaliano ya mkataba ikiwemo ubora wa vifaa vya kujengea pamoja na kuleta
mashine zote zinazotakiwa ili kazi ifanyike kwa ubora uliokusudiwa.
Kwa upande wa Mhandisi
mwakilishi wa kampuni ya Proactive Independent Group Ltd Elias Gamba amekiri
kutumia vibarua kuchanganya zege pamoja na kutumia mchanga tofauti na
makubaliano kutokana na mvua zilizonyesha huku akiahidi kurekebisha dosari
hizo.
Mhandisi Gamba
amesema kampuni hiyo italeta vifaa hivyo kama walivyoelekezwa na serikali ili
kuharakisha kazi hiyo na kuifanya iwe na ubora wa juu kwa kuwa na wao wangependa
kuona bwawa linakamilika ndani ya muda waliopewa na likiwa na ubora mzuri.
Ameeleza kuwa wamekuwa
na changamoto ndogondogo ambapo hakuna ambazo zimesababishwa na serikali na
kueleza kuwa changamoto hizo ni pamoja na mvua kunyesha na kusababisha kazi
kusimama huku mchanga na mawe vikipatikana mbali kutoka eneo la bwawa na huku
vibarua wengi wakipungua kutokana na kuanza msimu wa kilimo.
Kaimu Mtendaji wa
Kijiji cha Rungwa Mashaka Juma ameishukuru serikali kwa kufanya jitihada za
kutatua kero ya maji kwa wananchi wa kijiji hicho ambao wamekuwa wakinunua maji
shilingi mia tano kwa dumu au ndoo yenye ujazo wa lita ishirini.
“Wananchi wana hamu
kubwa kuona bwawa hili linakamilika, maji ni ya shida sana sio wananchi wote
wenye uwezo wa kununua maji kwa shilingi mia tano kwa lita ishirini, ndio maana
utaona wananchi wengi wanakuja huku bwawani mara kwa mara kuangalia hali ikoje hivvyo
tunaomba huyu mkandarasi aongeze kasi”, amesisitiza Juma.
Mhandisi wa Maji
halmashauri ya Itigi Evaristo Mgaya ameeleza kuwa ujenzi wa bwawa la Rungwa
lenye mita za ujazo milioni 1.7 umeanza mwezi Septemba 2017 na unatarajiwa
kukamilika mwezi Februari 2018 kwa fedha za serikali zaidi ya milioni mia saba
na bwawa hilo linajengwa na kampuni ya Proactive Independent Group Ltd kwa
kushirikiana na Bahati Investment and Supply.
Mgaya amesema maji kutoka
katika bwawa hilo yatasafirishwa katika matenki matatu ya kuhifadhia maji
ambapo matenki mawili yenye ujazo wa lita laki moja na nusu yatatumiwa na
wanakijiji wa Rungwa na tenki moja lene ujazo wa lita elfu 22 litatumika katika
hifadhi ya wanyamapori ya Rungwa.
No comments:
Post a Comment