Friday, October 20, 2017

‘HALMASHAURI ZIMUUNGE MKONO RAIS MAGUFULI KWA KUNUNUA VITANDA VYA KUJIFUNGULIA’, DKT NCHIMBI.



Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akifungua moja kati ya vitanda 14 vya kujifungulia vilivyotolewa na Rais Magufuli mapema leo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida.

Wauguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida wakifurahia mara baada ya kukabidhiwa vitanda vya kujifungulia vilivyotolewa na Rais Magufuli mapema leo katika viwanja vya hospitalini hapo.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Aisharose Mattembe akizungumza na wauguzi, madaktari na Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) mkoa wa Singida kabla hajakabidhi vitanda 14 alivyopewa na Rais Magufuli ili avifikishe kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Emmanuel Kimario akimshukuru Rais Magufuli kwa kuwapatia vitanda vya kujifungulia ili kupunguza uhaba wa vitanda kwa Mkoa wa Singida.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akisaidiana na wataalamu wa afya pamoja na Mbunge wa Viti maalumu Aisharose Mattembe kufunga moja kati ya vitanda 14 vya kujifungulia vilivyotolewa na Rais Magufuli mapema leo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida.

Halmashauri saba za Mkoa wa Singida zimeagizwa kununua vitanda kumi kwa ajili ya akina mama kujifungulia ili kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli za kuboresha afya ya mama na mtoto.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi ametoa agizo hilo mapema leo katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida mara baada ya kupokea vitanda vya kujifungulia 14, magodoro 20 na mashuka 50 vyenye thamani ya zaidi ya milioni 121 kutoka kwa Rais Magufuli.

Dkt Nchimbi amesema halmashauri zinatakiwa kuiga mfano wa Rais Magufuli anayojali afya kwa ajili ya wananchi hivyo wanapaswa kutenga kiasi cha shilingi milioni kumi na tatu kwa ajili ya kununua vitanda hivyo kwa mwaka huu wa fedha.

“Tumezoea kupokea tu na tumepokea sana vifaa tiba kutoka kwa rais wetu mpendwa Magufuli, hebu tujifunze upendo wake kwa wananchi, hivyo naagiza kila halmashauri inunue vitanda kumi vya kujifungulia nadani ya mwaka huu wa fedha”, amesisitiza Dkt Nchimbi.

Amengeza kuwa akina mama wajawazito wanatakiwa kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya kwakuwa kuna huduma bora zaidi huku akiwataka wakunga wa jadi wawasaidie wajawazito kufika katika vituo hivyo.

Aidha Dkt Nchimbi amemshukuru Mbunge wa Viti Maalumu Singida Aisharose Mattembe aliaminiwa na Rais Magufuli na kumtuma kufikisha vitanda hivyo Mkoani Singida huku akimtaka kuanzisha tunzo ya wakunga watakaosaidia kufikisha akina mama wajawazito katika vituo vya kutolea huduma za afya.

“Natoa shukrani zangu za dhati kwa niaba ya wananchi wa Singida kwa Rais Magufuli kwa kuendelea kutujali wana Singida, pia nakushukuru kwa uaminifu wako mbuge wetu Mattembe kwa kufikisha vifaa hivi salama ila naomba uanzisishe tunzo ya wakunga wa jadi watakaowashauri vizuri na kuwafikisha katika vituo vya kutolea huduma za afya akina mama wajawazito”, amesema Dkt Nchimbi.

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Emmanuel Kimario amemshukuru Rais Magufuli kwa vitanda hivyo vitakavyosaidia kupunguza uhaba wa vitanda, hasa kwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa ambapo wajawazito wengi wanapenda kujifungulia kwakuwa na imani napo kutokana huduma bora zinazotolewa.

Dkt Kimario amesema mpaka sasa bado kuna akina mama wanajifungulia nyumbani na kwa wakunga wa jadi jambo linalohatarisha afya ya mama na motto hivyo wafuate ushauri wa kufika katika vituo hivyo mara tu wanapo hisi kuwa na ujauzito.

‘Takwimu za kuanzia kipindi cha mwezi wa saba mpaka wa tisa mwaka huu zinaonyesha kuwa akina mama waliojifungulia ni 12,431 ambapo kati yao 190 wamejifunguliwa nyumbani, akina mama 78 wamejifunguliwa kwa wakunga  na wengine 258 wamejifungulia njiani”, amesema Dkt Kimario.

Kwa upande wake Naibu Meya wa Manispaa ya Singida Yagi Maulidi Kiaratu amewapongeza wauguzi na madaktari wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa huduma nzuri wanazotoa hadi kusababisha wagonjwa wengi kukimbilia hapo.

Amesema, “unakuta mgonjwa anaacha aspirini pale kituo cha afya Sokoine na kuja hapa Hospitali ya Mkoa akiwa na imani kubwa hata akipewa dawa ile ile hapa atapata nafuu, hivyo nawapongeza sana na muendelee na moyo huo wa kuwahudumia vizuri wagonjwa hata kama tunapata changamoto akati wa kuwalaza wanapokuwa wengi”, amesisitiza Kiaratu.

Ameongeza kuwa Mbunge wa Viti maalumu Singida Aisharose Mattembe amekuwa mstari wa mbele katika kusimamia afya ya mama na mtoto inaboreka Mkoani Singida huku akijitolea vifaa mbalimbali kama vitanda na mashuka,  jambo ambalo ni faraja kwa akina mama na wananchi wote. 

No comments:

Post a Comment