Tuesday, November 29, 2016

RC SINGIDA AHIMIZA WATUMISHI KUWAJIBIKA



Mkuu wa Mkoa wa Singida Mheshimiwa Mhandisi Mathew John Mtigumwe (picha ya maktaba).

Mkuu wa mkoa wa Singida Mhandisi Mathew Mtigumwe, amewahimiza watumishi wa umma hasa wa ngazi ya Vijiji na Kata kuwajibika  na kutimiza vyema majukumu yao kwani wao wako karibu zaidi na Wananchi, ili kutimiza adhma ya Serikali ya awamu ya tano ya kumpunguzia kama si kumuondolea kabisa kero zinazozuilika Mwananchi wa kawaida.

Mh. Mtigumwe ameyasema hayo leo katika Kijiji cha Kamenyanga kilichopo Kata ya Aghondi, Halmashauri ya Itigi, Wilayani Manyoni akiwa katika ziara yake ya kujitambulisha na kusikiliza kero za Wananchi, ambapo Wananchi wa Kata hiyo walimlalamikia Mkuu wa Mkoa juu ya utendaji mbovu wa Mtendaji wa Kata yao hasa ubadhirifu wa fedha za Kijiji na uuzaji wa maeneo ya Kijiji bila kufuata taratibu.

Kufuatia malalamiko hayo ya Wananchi, Mkuu huyo wa Mkoa ameagiza kusimamishwa kazi mara moja, ili kupisha uchunguzi kufuatia tuhuma mbali mbali zinazomkabili Bw. James Sylvester, Afisa mtendaji wa Kata ya Aghondi iliyopo halmashauri ya Itigi, Wilayani Manyoni, mkoani Singida, ambaye kwa  kushirikiana na Mwenyekiti wa Kijiji cha Aghondi Bw. Mrisho Mbaruku, walikiuka taratibu za umilikishwaji wa maeneo ya Kijiji, na kumilikisha ardhi kwa baadhi ya watu kinyume na taratibu za Kijiji kwa manufaa yao binafsi.

“Nimekua nikipokea taarifa za utendaji kazi usioridhisha wa Bw. James Sylvester ambaye ni mtendaji wa Kata hii, hususani kwenye uwasilishaji wa mapato ya Halmashauri, hivyo kutokana na kashfa zinazo mkabili Mtendaji huyu, mbali na kilio cha wananchi ni vyema sasa akae pembeni na tukimkuta na hatia , sheria itachukua mkondo wake” Alisema Mh. Mtigumwe.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa wilaya ya Manyoni Mh. Geoffery Mwambe ambaye ameambatana na Mkuu wa Mkoa katika ziara hiyo amesema, kutokana na tuhuma zinazomkabili Bw. Mrisho Mussa, Mwenyekiti wa kijiji cha Kamenyanga ambacho pia kipo katika Kata ya Aghondi, kushindwa kuitisha mikutano ya Kijiji kwa muda  muafaka kama miongozo ya kijiji inavyoelekeza, pia wananachi kuonesha kutoridhishwa na utendaji kazi wake, ameagiza kufanyika mkutano wa Kijiji mwishoni mwa mwezi huu, ili  Mkutano huo utoe maazimio dhidi ya Mwenyekiti huyo.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mh. Mathew Mtigumwe yupo kwenye ziara maalumu akizunguka Mkoa mzima wa Singida, wenye Wilaya tano, zenye halmashauri saba, leo ikiwa ni siku ya tatu tangu kuanza kwa ziara hiyo, katika Halmashauri ya Itigi, Wilaya ya Manyoni, Mtigumwe ametembelea miradi mbali mbali ya maendeleo, na kuhimiza ushirikiano baina ya Viongozi na Wananchi katika kufanikisha malengo na mikakati inayowekwa na Serikali kwa mandeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment