Thursday, October 02, 2014

WATUMISHI WA HOSPITALI YA MKOA WAASWA KUTUMIA CHANGAMOTO WANAZOKUMBANA NAZO KUIBUA FURSA ZA MAFANIKIO.
Watumishi wa Hospitali ya Mkoa wa Singida wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni rasmi ambaye ni mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Bi. Fransisca Mmari.

Watumishi wa Hospitali ya Mkoa wa Singida wameaswa kutumia changamoto wanazokabiliana nazo katika utendaji kazi wao kama fursa ambazo zitawaongezea ufanisi na mafanikio makubwa.

Kauli hiyo imetolewa na mgeni rasmi ambaye ni mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Bi. Fransisca Mmari wakati akisoma hotuba ya kuwapongeza watumishi hao kwa kupata tuzo tano, katika kikao kilichofanyika hospitalini hapo jana asubuhi.

Mmari amesema tuzo walizopata zimetokana na juhudi wanazozifanya hivyo tuzo hizo ziwe chachu ya kuongeza bidii zaidi ili hospitali ya Mkoa iwe mfano wa kuigwa nchi nzima.

Mgeni rasmi ambaye ni mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Bi. Fransisca Mmari akisoma risala katika kikao cha kuwapongeza watumishi wa hospitali ya Mkoa wa Singida.

Aidha Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dokta Deogratius Banuba ametaja mafanikio na tuzo walizopata kuwa ni tuzo ya mradi wa MAISHA katika kuboresha huduma za afya ya uzazi wa mpango, tuzo ya utendaji bora katika huduma ya dharura kwa wajawazito na watoto wachanga, tuzo ya 5s, tuzo ya KAIZEN na tuzo ya kukinga na kudhibiti maambukizi eneo la kazi.

Dokta Banuba ameongeza kuwa mafanikio mengine ni pamoja na kuongezeka kwa mapato  upande wa bima ya afya kutoka milioni 19 kwa mwezi katika kipindi cha mwaka jana hadi kufikia milioni 33 kwa mwezi kuanzia mwezi Januari mwaka huu.

Moja ya tuzo za hospitali ya Mkoa wa Singida.

Amesema hospitali imefanikiwa kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano kutoka 119 mwaka 2012 hadi kufikia 32 mwaka 2013, aidha kwa upande wa wajawazito vifo vimepungua kutoka 29 mwaka 2012 hadi kufikia 12 mwaka 2013.

Dokta Banuba amewapongeza watumishi wa hopitali hiyo  kwa ushirikiano na kujituma kwao na hivyo kupelekea kuanzishwa kwa maabara maalumu kwa ajili ya wajawazito na watoto pamoja na kuanzishwa chumba maalumu cha watoto mahututi.


Mgeni rasmi ambaye ni mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Bi. Fransisca Mmari  akimpongeza mtumishi wa hospitali ya Mkoa Monica Alute.

Naye Mwakilishi wa timu ya kudhibiti ubora Jadil Abas kutoka hospitali hiyo amesema huduma zitolewazo hospitali hapo zimeboreshwa  na kuifanya hospitali ya Mkoa wa Singida kutambulika nchi nzima kwa tuzo walizopata.

Abas ameongeza kuwa kutokana na mafanikio hayo hospitali hiyo imetajwa kuwa ya mfano wa kuigwa na hivyo kupelekea mikoa, wilaya na wadau mbalimbali wa sekta ya afya kuitembelea ili kujifunza mafanikio yao.Mgeni rasmi ambaye ni mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Bi. Fransisca Mmari akiimba na kufurahia tuzo pamoja na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Singida Dokta Dorothy Gwajima mbele ya watumishi wa hospitali hiyo.
 

Timu ya Kudhibiti ubora ya Hospitali ya Mkoa wa Singida wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni rasmi ambaye ni mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Bi. Fransisca Mmari.


 Kamati ya Uendeshaji ya Hospitali ya Mkoa wa Singida wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni rasmi ambaye ni mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Bi. Fransisca Mmari.Tuzo mbalimbali za hospitali ya Mkoa wa Singida.

No comments:

Post a Comment