Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida wamepatiwa elimu kuhusu Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa (NHIF) ili kuwajengea uelewa utakaowawezesha kuwa mabalozi wa kuhamasisha jamii kujiunga na mfumo huo.
Mafunzo hayo yamelenga kuonyesha umuhimu wa bima ya afya katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za matibabu, huku ikielezwa kuwa bima ni ngao muhimu inayookoa familia dhidi ya gharama kubwa za dharura za matibabu.
Aidha, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida (RMO) Dkt. Jesca Lebba, amewasihi wananchi wote kujitokeza kwa wingi siku ya kesho katika kituo cha Sokoine kilichopo manispaa ya Singida, ambapo utafanyika uzinduzi rasmi wa Bima ya Afya kwa Wote. Uzinduzi huo utatoa fursa kwa wananchi kupata elimu ya kina, kutoa maoni, pamoja na kusajiliwa ili kuwezesha kila familia kuwa na ulinzi wa kiafya.
Sambamba na hayo, Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) Mhe. Rodrick mpogolo alisema, Dira ya Taifa inalenga kutoa huduma bora za kiafya kwa wananchi wote, hivyo kujiunga na bima ya afya ni hatua muhimu na ya kimkakati katika kufikia azma hiyo ya serikali.

















No comments:
Post a Comment