Na Glory Kimaro,
"Tunataka kuandaa wasifu wa Virusi vya Ukimwi (VVU) na UKIMWI wa Mkoa wa Singida ambao utakuwa na manufaa makubwa kwa jamii ya Singida na Tanzania kwa ujumla,"Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Bw. Stanislaus Choaji, wakati wa ufunguzi wa kikao cha kuandaa wasifu wa VVU na Ukimwi kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida. Akizungumza katika ufunguzi Bw. Choaji amepongeza jitihada za kuandaliwa kwa wasifu huo mkoani Singida na kutoa wito kwa washiriki kutoa ushirikiano akisisitiza kuwa wasifu huo utatoa taarifa za kina kuhusu mwenendo wa maambukizi, kuongoza maamuzi yanayozingatia takwimu na ushahidi, kubaini mapungufu yaliyopo katika utoaji huduma, kupendekeza afua stahiki, kusaidia uhamasishaji wa rasilimali, pamoja na kurahisisha ufuatiliaji na tathmini kimkoa.
Naye Mratibu wa TACAIDS Kanda ya Kati, Bw. Ericko Kawanga, ameeleza kuwa uratibu madhubuti wa masuala ya UKIMWI unahitaji tathmini ya hali halisi ya eneo husika ili kuchukua hatua stahiki za kudhibiti maambukizi mapya na kuzuia vifo. Bw. Kawanga amebainisha kuwa kiwango cha maambukizi mkoani Singida kimeshuka kutoka asilimia 3.6 (katika utafiti wa mwaka 2016/2017) hadi kufikia asilimia 3.0 (mwaka 2022/2023).
Ameongeza kuwa takribani watu 29,000 wanaishi na VVU kati ya wakazi zaidi ya milioni 2 katika mkoa wa Singida, jambo linalothibitisha kuwa jitihada za kupambana na maambukizi mapya zinaendelea kuzaa matunda. Amesema, kuandaa wasifu huo kutawezesha mkoa kutathmini ulipotoka na unakokwenda, ambapo katika mchakato huo wadau wataangazia masuala ya upimaji wa hiari, kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, ufuasi wa matumizi ya dawa za kufubaza virusi (ARVs), pamoja na kupiga vita unyanyapaa.
Mchakato huo unatekelezwa na Mkoa wa Singida kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Wizara ya Afya, pamoja na Ofisi ya Rais - TAMISEMI, ukiwa ni nyenzo muhimu ya kimkakati katika kuimarisha mapambano dhidi ya maambukizi mapya na kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.

























No comments:
Post a Comment