Serikali ya mkoa wa Singida imepongezwa kwa kusimamia na
kutekeleza kikamilifu Ilani ya Chama ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa utekelezaji
wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi kwa kiwango cha juu ikiwemo miradi
ya maji, afya, elimu na miundombinu mkoani humo.
Pongezi hiyo zimetolewa na Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dkt.
Emmanuel Nchimbi katika ziara yake ya kikazi ya Siku Mbili mkoani Singida wakati
anazungumza na wananchi kwenye mikutano ya hadhara katika Wilaya ya Manyoni na
Ikungi pamoja na kusikiliza na kutatua papo hapo kero ambazo zilitolewa na
wananchi.
Balozi Nchimbi amesema ushirikiano imara kati ya Viongozi wa
Serikali na wa CCM mkoani Singida umepelekea miradi mingi ya maendeleo
kutekelezwa kwa wakati na kwa kiwango cha juu.
Amesema taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM aliyopatiwa na
Mkuu wa mkoa wa Singida Mheshimiwa Halima Dendego, imeonyesha wazi kasi kubwa
ya Maendeleo ambayo imepigwa mkoani Singida kwa kuboresha na kuimarisha huduma
mbalimbali za Kijamii ikiwemo huduma za maji, afya, elimu, miundombinu, umeme, pamoja na sekta kilimo kwa
usalama wa chakula.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego akitoa salamu za Serikali ya Mkoa huo juu ya utekelezaji wa Ilani kwenye mkutano wa Katibu Mkuu Chama Cha Mapinduzi.
Naye, Mkuu wa mkoa wa Singida Mheshimiwa Halima Dendego, akitoa
taarifa ya mkoa wa Singida kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi amemhakikishia
Katibu Mkuu huyo wa CCM wataendelea kusimamia kikamilifu fedha ambazo
wanapatiwa na Serikali ya awamu ya Sita katika utekelezaji wa miradi mbalimbali
ya maendeleo ili wananchi waweze kupata huduma bora na za uhakika za maendeleo
karibu na maeneo yao.
Halima Dendego amesema mpaka sasa mkoa wa Singida tayari umepokea
zaidi ya shilingi Trilioni Moja kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo
hali ambayo imeufanya mkoa wa Singida kung’aa kimaendeleo katika sekta
mbalimbali.
Mkuu huyo wa mkoa wa Singida amemwomba Katibu Mkuu huyo wa
CCM kumfikishia Salamu za pongezi na shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendeleo kuupatia mkoa wa
Singida fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya
wananchi.
Amesema mkoa wa Singida kwa sasa unaendelea na mipango na
mikakati ya kuwavutia wawekezaji katika sekta mbalimbali wa ndani na nje ya nje
kuja kuwekeza mkoani humo ikiwa ni sehemu ya kuongeza pato la mkoa na la taifa
kwa ujumla kupitia vivutio vya uwekezaji kwenye masuala mbalimbali ikiwemo
kilimo na utalii.
No comments:
Post a Comment