Wednesday, January 10, 2024

HOTUBA YA MGENI RASMI, MHE. BALOZI DKT. PINDI HAZARA CHANA (MB) WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA KWENYE UZINDUZI WA KAMPENI YA HUDUMA YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA


HOTUBA YA MGENI RASMI, MHE.  BALOZI DKT. PINDI  HAZARA  CHANA (MB) WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA  KWENYE UZINDUZI WA KAMPENI YA HUDUMA YA MSAADA WA KISHERIA YA  MAMA SAMIA(MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN) KATIKA UWANJA WA STENDI YA ZAMANI- MANISPAA YA SINGIDA

 10 JANUARI, 2024 

Ninawasalimu kwa Salaam ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kazi Iendelee

 Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa fursa hii ya kuwepo mahali hapa Viwanja vya Stendi ya Zamani, Manispaa ya Singida siku ya leo. Nashukuru pia kwa heshima niliyopewa kuwa Mgeni Rasmi kwenye hafla hii muhimu ya uzinduzi wa Kampeni ya Mama Samia ya Msaada wa Kisheria inayojulikana kwa jina la “Mama Samia Legal Aid Campaign.” Nawashukuru sana wote mlioweza kuhudhuria mahali hapa pamoja na Watanzania wote wanaotusikiliza kupitia vyombo vyetu mbalimbali vya habari.

Ndugu Wananchi na Wageni Waalikwa,

Naomba pia kuchukua fursa hii  kipekee kumshukuru Mhe. Mkuu wa Mkoa  na Kamati yake yote Ulinzi ya Mkoa wa Singida kwa kuridhia Kampeni hii  ifanyike mkoani kwako ikiwa ni Mkoa wa Sita tangu izinduliwe na kutekelezwa katika mikoa mingine ikitanguliwa na mikoa ya Dodoma, Manyara, Shinyanga, Ruvuma na Simiyu. Mkoa wako  umekua bega kwa bega katika maandalizi ya tukio hili muhimu. Asanteni sana.

Ndugu Wananchi na Wageni Waalikwa;

Kampeni ya hii ya  Msaada wa Kisheria inatokana na Azma ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuhakikisha kwamba  kila mwananchi anafahamu masuala ya kisheria ikiwemo haki na wajibu wake na kwamba kila mwananchi anaifikia haki na wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za mawakili basi waweze kufikia haki kupitia huduma za msaada wa kisheria. Kwa muktadha huu, Mhe. Rais ametuelekeza kuhakikisha msaada wa kisheria  unatolewa kwa wananchi wote hususani kundi la wanyonge na wasiokuwa na uwezo ili kupata haki, usawa, amani na maendeleo. Kama mnavyofahamu, nchi yetu imeendelea kupiga hatua kubwa katika utekelezaji wa Haki za Binadamu na Msaada wa Kisheria nchini;

Hivyo, Mhe. Rais anataka kuendelea kuona kuwa Tanzania inaendelea kuwa nchi tulivu na yenye amani kwa kuwawezesha Wananchi sio tu kupata msaada wa kisheria bali kuwaelimisha kuhusu haki zao na wajibu wao kwa Taifa. Kila mmoja wetu akifahamu vizuri haki zake na wajibu wake, ndipo nchi yetu itasonga mbele kiuchumi.

Ndugu Wananchi na Wageni Waalikwa,

Wizara ya Katiba na Sheria ninayoiongoza  imepewa dhamana ya kutekeleza majukumu ya Serikali yanayohusu masuala ya Katiba na Sheria za nchi. Katika utekelezaji wa majukumu haya, Wizara  imeendelea kuzingatia miongozo mbalimbali ya kisera ya Kitaifa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha  kunakuwa na usawa  mbele ya sheria,  na kuwa wananchi  wanapata  haki kwa wakati kupitia vyombo vya haki, wanaishi bila ya ubaguzi wowote,  na wanalindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.

Ndugu Wananchi na Wageni Waalikwa,

Mwaka 2017 Serikali ilipitisha Sheria ya Msaada wa Kisheria, Sura ya 21 kwa lengo la kuratibu na kusimamia shughuli za msaada wa kisheria nchini. Na katika hili, huuduma za msaada wa kisheria zimeendelea kuimarishwa nchini na wananchi wengi wameendelea kupata huduma za msaada wa kisheria kwa uhakika. Kupitia Sheria hii, Wizara yangu imewasajili watoa huduma za msaada wa kisheria takribani  250 na wasaidizi wa kisheria takribani 1800 wamesajiliwa na wanatoa huduma hizi za msaada wa kisheria katika mikoa yote Tanzania Bara. Hii yote ni kuhakikisha upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wakati na kwa ufanisi kwa wananchi hususani katika maeneo ya pembezoni.

Ndugu Wananchi na Wageni Waalikwa,

Wizara yangu imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali kutoka katika taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali katika kuhakikisha mipango na shuguli za msaada wa kisheria zinabuniwa na kutekelezwa kwa lengo la kuwafikia wananchi wengi. Mipango hii ndio imetupelekea kuanzishwa  kwa Kampeni hii ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia. Lengo  likiwa  ni kulinda na kukuza upatikanaji wa haki kwa wote kupitia huduma ya msaada wa kisheria nchini ambayo ni utekelezaji wa Katiba yetu ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania hususani  ibara ya 8 (1)  (b) na Ibara ya 13 (1) zinazoweka msingi wa haki na usawa na ustawi wa wananchi.  

Pamoja na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, masuala haya ya msaada wa kisheria yapo katika Ibara ya 231(k) ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 ambayo imetambua umuhimu wa upatikanaji haki kwa wananchi  na inatuelekeza  kuimarisha huduma za msaada wa kisheria  hususan kwa Wanawake na Watoto katika maeneo yote. Wajibu wa Wizara yangu na kuwa kupitia Kampeni hii, ni kuhakisha kuwa inakidhi matarajio ya Mhe. Rais kwa kuweka mazingira wezeshi ya wananchi kupata haki kwa usawa, uzingatiwaji wa haki za binadamu na utawala bora. Mheshimiwa Rais anataka kuona kuwa  Tanzania inaendelea kuwa nchi tulivu na yenye amani kwa kuwawezesha wananchi, sio tu kupata msaada wa kisheria bali wanaelimishwa waelimisha kuhusu haki zao na wajibu wao kwa Taifa.  Tunaamini kwamba, kila mmoja wetu akifahamu vizuri haki zake na wajibu wake, ndipo nchi yetu itasonga mbele kiuchumi na kutuletea maendeleo.

Ndugu Wananchi na Wageni Waalikwa,

Niwathibitishie kuwa,  Wizara yangu imejipanga  kikamilifu katika kuhakakisha kuwa wananchi wa Tanzania wananufaika na Mama Samia Legal Aid Campaign na kuhakikisha kuwa inawafikia wananchi wote hapa nchini.Kupitia huduma hii, msaada wa kisheria unatolewa bure katika Halmashauri zote za Mkoa wa Singida  kuanzia  kesho tarehe 11 Januari , 2024 hadi tarehe 19 Januari, 2024. Malengo ni kufikia jumla ya Kata 70 na vijiji 210 vya mkoa wa Singida.  Wito wangu  kwa Wananchi wote  wa Mkoa wa Singida na maeneo jirani kuitumia vizuri fursa hii kwa kuhakikisha kuwa mnashiriki kikamilifu  kwa kupata elimu na huduma za masuala mbalimbali ya kisheria  zitakazotolewa bure. Aidha, niwasihi viongozi katika ngazi ya Mkoa, Wilaya, Kata na Vijiji kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wataalamu wetu watakapokuwa katika maeneo yenu, muhamasishe wananchi wajitokeze kwa wingi kupata huduma hii.

 

Ndugu wananchi na Wageni waalikwa;

Kama mnavyojua,  nchi yetu ni kubwa, na idadi ya wananchi pia ni kubwa kama matokeo ya Sensa yanavyoonyesha kuwa zaidi ya watu milioni 61. Ziko jitihada nyingi sana za Serikali za  kulinda na kukuza haki za binadamu zilizofanyika na zinazoendelea kufanyika. Serikali imeweka Mikakati ya Kitaifa ikiwemo ya kutokomeza ukatili wa kijinsia;   kuimarisha Ulinzi wa Mtoto na kuweka mifumo ya kisheria ya kulinda haki za wanawake na watoto..

 

Ndugu wananchi na Wageni waalikwa;

 Wote ni mashuda kuwa kwa muda mrefu sasa,  vyombo vya habari vimekuwa vikitoa taarifa za unyanyasaji na ukatili wa kutisha dhidi ya wanawake na watoto. Matukio yanayoripotiwa yanaleta tafsiri nyingi; lakini moja la msingi ni umuhimu wa kujenga uelewa wa jamii katika masuala ya haki za binadamu na sheria; kuhamasisha wananchi wote kuzingatia haki na wajibu wao wa kikatiba na wa kisheria katika maisha yao ya kila siku. Aidha, tunatakiwa  kulinda watoto wetu dhidi ya ukatili ili tuwe na Taifa lenye staha, maadili na  lenye kuheshimu na kuthamini utu wa mtu. Huu ndio urithi tuliopewa na wazee wetu waliotutangulia kuanzia kwenye uongozi wa kitaifa hadi kifamilia, na hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kutimiza wajibu wake  na kuzingatia sheria za nchi zilizopo.

 

Ndugu wananchi na Wageni waalikwa;

Kwa namna ya pekee naomba, nitumie hadhara hii  kumshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo anatuongoza kwa kuzingatia Katiba, Sheria na taratibu tulizojiwekea kama nchi. Kila Mtanzania analo jukumu la kusimamia na kuzingatia  haki za binadamu, utawala wa sheria, utii wa sheria na elimu ya kikatiba na ya kisheria kwa umma.  Haya yote yanafanikiwa kwa uwepo wa sheria zinazotekelezwa, uwepo wa sheria nzuri peke yake hakutoshi, bali pia wananchi  wanatakiwa  kuelimishwa kuhusu sheria hizo na kuzifahamu, wananchi waelimishwe juu ya masuala ya haki za binadamu ili wafahamu haki na wajibu wao. 

 Vitendo vya ukatili wa kijinsia bado ni changamoto katika jamii zetu. Wanawake na watoto wameendelea kuwa ni wahanga wa vitendo hivi. Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna baadhi ya maeneo bado tunaendelea kusimamia mila na desturi zilizopitwa na wakati, tunaendelea kuchukua hatua mkononi na kutokusheshimu sheria zilizopo. Na katika hili niwakumbushe wajibu wa kutoa taarifa juu ya vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia na uvuinjifu wa sheria. Na hapa nisisitize vyombo vyetu vya utoaji haki tusimamie haki na kuhakikisha haki inatendeka kwa wakati kwa washukiwa wote wa vitendo hivi wanachukuliwa hatua stahiki.  Na Jeshi letu la Polisi litusaidie kuchunguza na kupeleleza kwa kina ili kukomesha mnyonyoro wote wa wahalifu katika masuala ya ukatili wa kijinsia. Sisi kama Serikali tutaendelea kusimamia misingi ya sheria na kufanya maboresho ya sheria zetu ili kuendana na mazingira ya sasa hususani katika maendeleo ya teknolojia.

 

Ndugu wananchi na Wageni Waalikwa;

 Utekelezaji wa Kampeni hii umekuwa na mafanikio makubwa. Naomba nieleze kwa uchache mafanikio tuliyoyapata hadi kufikia Oktoba, 2023. Kama nilivyoeleza hapo awali kwamba Kampeni hii imeanza kutekelezwa mapema mwezi Aprili, 2023. Hadi kufikia tarehe 30 Oktoba, 2023, Mama Samia Legal Aid Campaign imefikia mikoa mitano (05) ya  Dodoma, Manyara, Shinyanga, Ruvuma  na Simiyu ambapo jumla Halmashauri 35, Kata 397 na Vijiji/ Mitaa 1,046 imefikiwa katika utekelezaji wa Kampeni hii. Katika mikoa hii mitano, jumla ya wananchi 362,488 (Wanaume 179,874  wananwake 182,615 ) wamefikiwa kupitia elimu ya kisheria na huduma nyingine za kisheria.

 

Kwa kuwa Kampeni hii pia inashiriki katika utatuzi wa migogoro katika ngazi za kijamii, jumla ya  migogoro 6,365 iliyohusu  masuala ya ardhi, ndoa, mirathi na matunzo ya watoto ilipokelewa ambapo  kati ya hiyo migogoro  488 ilitatuliwa na kuhitimishwa katika kipindi cha Kampeni. Migogoro 5,877 inaendelea kushughulikiwa katika mamlaka  mbalimbali za kimahakama na kiutawala na Wizara kupitia waratibu na wasajili wa mikoa na wilaya imeendelea kufuatilia utekelezaji wake.

 

Kampeni hii inawezesha pia huduma za usajili wa matukio mbalimbali ikiwemo usajli wa vyeti wa kuzaliwa na vifo kupitia Ofisi ya Kabidhi Mkuu RITA. Jumla  wananchi 2,055 (Wanaume1,035 Wanawake 1,020) walisajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa kupitia Ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu – RITA katika mikoa hii mitano. Kwa upande wa maeneo ya vizuizi, Kampeni pia iliweza kufikia Vituo vya Polisi 22 na Magereza 17 yametembelewa na huduma kutolewa na katika hili jumla ya Wafungwa na Mahabusu 4,763 wamefikiwa na kupatiwa  elimu na huduma mbalimbali za kisheria.

 

Ndugu wananchi na wageni waalikwa

 Kampeni imewezesha wananchi wengi kufahamu masuala ya kisheria yaliyopo kwenye maisha yao ya kila siku ikiwemo masuala ya ndoa, ukatili wa kijnsia, ardhi na mirathi. Kupitia Kampeni hii,  wananchi  wameongeza uelewa katika  masuala ya mirathi na wosia ambapo sasa kumekuwepo na ongezeko la wananchi wanaofika  Ofisi za RITA kwa ajili ya kuandika wosia; na mwisho kumekuwepo na ongezeko la   uelewa na uwajibikaji wa viongozi (watendaji wa vijiji, kata,  halmashauri, viongozi wa kidini na kimila, wanafunzi na walimu wa Shule za Msingi na Sekondari) katika kuwahudumia wananchi na kuwasaidia kudai na kupata haki zao baada ya kujengewa uwezo katika masuala ya sheria mbalimbali, haki za binadamu na utawala bora.

 

 Ndugu wananchi na Wageni waalikwa;

Kabla ya kuhitimisha hotuba yangu naomba kutoa wito kama ifuatayo:

Kwanza; Naomba niwapongeze na kutoa wito kwa viongozi wote wa dini hapa nchini, bila shaka kwa nyakati tofauti tofauti, viongozi wetu wa dini wamekuwa  wakikemea vitendo vya uvunjifu wa sheria, mmomonyoko wa maadili katika jamii hususan ukatili uliokithiri dhidi ya wanawake na watoto.  Hakika huduma yenu kwa jamii ina nafasi kubwa sana ya kubadili tabia, mitizamo hasi na kujenga maadili mema. Niwaombe muendeleze jitihada hizi  ili  kujenga jamii yenye maadili na yenye kumhofia Mwenyezi Mungu ambapo chanzo chake ni kuheshimu haki za binadamu, kuzilinda haki hizo na kuzingatia wajibu wetu wa kikatiba na kisheria.   Niwathibitishie kuwa  Wizara ya Katiba na Sheria iko tayari kushirikiana na viongozi wa dini kwa namna yoyote ambayo itafaa katika kampeni hii hata kama itahusisha kutumia majukwaa yao kutoa elimu kwa umma juu ya haki na wajibu  wa Kikatiba na Kisheria. Na niwaombe tena kushiriki kikamilifu kikamilifu wakati wa utekelezaji wa Kampeni ili muweze kuendelea kujengewa uwezo katika masuala ya kisheria.

 

Pili, kwa ndugu zangu wanahabari na vyombo vya Habari; niwakumbushe kuwa  jukumu kubwa na muhimu katika Kampeni hii, ninawaomba mjipange vyema kama sekta ili tushirikiane katika  kutekeleza suala hili muhimu kwa mustakabali wa heshima ya nchi na wananchi wetu. Muhakikishe wananchi wanapata elimu kwa wakati na msaidie kuibua changamoto mbalimbali za wananchi na kuhakikisha mnafuatilia ufumbuzi wake hadi mwisho.

 

Tatu, kwa wanasiasa wenzangu, wito wangu kwenu naomba  tujitahidi kutumia uzoefu na weledi wetu katika kumuunga mkono Kiongozi wetu, Mama yetu, Mlezi wetu na Mtetezi wa Wananchi  kuondoa kadhia ya ukatili  wa kijinsia na uvunjifu  wa haki za binadamu katika jamii yetu. Tunatambua mchango mkubwa ambao unatolewa  katika jamii.

 

Nne, kipekee niwashukuru sana asasi za kiraia kwa mchango wenu mkubwa  mnaoendelea kutoa katika katika nyanja mbalimbali  kwa  watanzania. Niwathibitishie kwamba  Serikali  inatambua mchango wenu na itaendelea kuunga jitihada zenu, tunaamini kuwa Kampeni hii inaongeza nguvu katika jitihada  zinaendelea. Niwaombe viongozi wenzangu kutoa ushirikiano wa kutosha kwa watoa huduma za msaada wa kisheria hususan kwa Wasaidizi wa Kisheria  wanaotoa huduma ya msaada wa kisheria bure katika maeneo yenu katika ngazi ya Kata, Vijiji na mitaa.

 

Tano, kwa upande wa Jeshi la Polisi,  Ili kuchochea upatikanaji haki na kwa wakati natoa wito kwa Kamanda wa Polisi  Mkoa (RPC) wa Singida,  kushughulikia kesi zote za ndoa, mimba za utotoni na ubakaji ambazo zimekaa muda mrefu katika upepelezi bila kushughulikiwa kwa kuhakikisha watuhumiwa wanapatikana na wanashughulikiwa ili kuondoka changamoto ya kutoroka kwa watuhumiwa pindi wanapopewa dhamana ama wanaposikia wanatafutwa na Jeshi la Polisi.   Kampeni hii inatukumbusha uwajibikaji na usimamizi wa maamuzi yenye kuleta haki, hivyo niwakumbushe watumishi wote kutojihusishwa na masuala ya rushwa inayopelekea kudhorotesha upatikanaji haki kwa wakati; na

 

Mwisho, ingawa sio kwa umuhimu, nimuombe Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Singida kuweka mipango endelevu ya upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi katika ngazi za kijamii. Uendelevu wa Huduma hii ndio utakamilisha adhima yetu ya Kampeni. Kwani bila mipango ya uendelevu wa huduma Kampeni hii haitakuwa imefikia malengo yake.

 

Ndugu Wananchi na Wageni Waalikwa,

Napenda kuhitimisha  hotuba yangu kwa kuwashukuru uongozi na wananchi wa Singida kwa mapokezi mazuri na kutufanya tujisikie tuko nyumbani. Aidha, kipekee niwashuru wadau wa maendeleo na asasi za kiserikali waliounga mkono katika kufanikisha shughuli hii.

 

Niwashukuru sana Vyombo vyetu vya habari, vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa dini na kimila na wananchi kwa ujumla. Tunawashuruku  sana kwa kutambua umuhimu na kufanikisha shughuli hii. Tunawashukuru kwa ukarimu wenu na Mungu aendelee kuwabariki.

 

Sasa baada ya  kusema maneno  maneno haya, kwa heshima kubwa niliyopewa naomba kutangaza rasmi kwamba  utekelezaji wa Kampeni ya Mama Samia ya Huduma za Msaada wa Sheria “Mama Samia Legal Aid Campaign”  Mkoa wa Singida  imezinduliwa rasmi .

Asanteni sana kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment